Simu ya Inspekta Nyawenga ilimchanganya
sana Esther na kumfanya asitishe jambo lile alilokuwa akilifuatilia. Ikabidi
arudi katika eneo alilokuwa ameketi mwanzo pamoja na yule mfanyazi mwenzake.
Wakati huo naye Dr. Adamu alikuwa akitoka nje ya ofisi ya Dr. Justine ambaye
ndiye Daktari mkuu wa AGA KHANI Hospital.
Alielekea moja kwa moja upande
alipokuwa amekaa Esther pamoja na mwenzake. Esther alipomuona Dr. Adamu
alisimama na kumnyookea huku kila mmoja akimtizama mwenzake lakini macho na uso
wa Esther uliokuwa umekunja ndita uliashiria moja kwa moja yakuwa alikuwa ni
mtu mwenye hasira na aliyepaniki kwa wakati huo. “Vipi Mbona kama hauko
sawa” aliuliza Dr. Adamu “Ndiyo.. yeap yeap kuna… kuna jambo”
alijibu Esther “Kwani utakuwa na ubaya kwa mimi kufahamu jambo hilo” aliendelea kuhoji Dr. Adamu “Usijali Dokta
waeza endelea na majukumu yako” Esther alijibu kama vile mtu aliyekuwa
ahitaji ushirikiano kutoka kwa Dr. Adamu lakini hilo halikuweza kumsumbua wala
kumkatisha tamaa Dr.Adamu ambaye alikuwa na mpango wa kuanza kuseti tageti zake
kwa Esther.
Kulikuwa na kimya kidogo lakini
haikuzidi dakika moja simu ya Esther ikaanza kuita alipotaka kupokea akashtuka
kuona kwamba ilikuwa ni ile namba aliyotumia inspekta Nyawenga kumpigia kwa mara ya kwanza na kumtaka afike eneo la tukio
la ajali ya Boss France. Alisita kidogo nayo simu iliendelea kuita akaona
hakuna namna nyingine zaidi ya kupokea simu ile. “Haroo... Vipi
umeshaanza kuja tunakusubiri tuanze majukumu yetu” alisema inspekta
nyawenga kwa ukali kidogo “Abee… nakuja Afande” aliitikia Esther aliyekuwa akionyesha hali ya
uoga kiasi kwamba Dr. Adamu alishindwa kuelewa ni kipi kulichokuwa kinamsibu Esther.
Basi Esther alibeba pochi yake na kutoa kiasi cha noti nyekundu kisha akampatia
yule mfanyakazi aliyekuwa amekuja naye pale hospital na kumtaka aendelee kubaki
kwa ajili ya kumpa taarifa zitakazoendelea juu ya Boss wake.
Alimpungia mkono Dr. Adamu na kuanza
kuondoka lakini ghafla alijikuta akizuiliwa na kuvutwa na mkono wa Dr. Adamu
Kisha akajiwahi “Aaah! Samahani Esther kwa kukuzuia lakini nafikiri ni
vema ukanipa namba yako ili tuweze kuwasiliana juu ya hali ya mgonjwa wako” “utampatia
taarifa huyu mfanyakazi alafu atanijuza mimi” looh…! Mwanadada Esther
alikuwa na majibu yaliyomchoma sana moyo Dr. Adamu na kumfanya ashindwe kuelewa
ni wapi alipokosea.
Wakati hayo yote yalipokuwa yakiendelea
naye Dr. Justine aliweza kuyashuhudia kwani alikuwa akitoka nje ya ofisi yake
lakini baada ya kuona mwanzo wa jambo lile alisimama kwa mda nje ya mlango wa
ofisi yake na kulitolea macho. Alitingisha kichwa na kucheka kidogo kwa
tabasamu kisha akaondoka kuelekea katika wodi aliyokuwa amelazwa Vicky. Wakati
huo Esther alikuwa akielekea sehemu alikopaki gari huku akitembea kwa mwendo ya
madaha, mavazi ya Esther aliyokuwa
ameyavaa siku hiyo ukichanganyia na uzuri wake uliochagizwa na rangi yake ya
mvuto na iliyo asilia ilimfanya Dr. Adamu kuingia mzima, mzima kwa Esther
kifikra bila hata ya kugonga hodi. Loooh! Alichanganyikiwa bila ya kujua ni wapi
alipokuwa akipakimbilia. Esther aliingia ndani ya gari lake na kuanza kuondoka
kuelekea katika eneo la tukio la ajali ya Boss France. Kichwa chake kilikuwa
resi na kikiwaza juu ya hali aliyokuwa nayo Boss wake na huko aendako “Sijui
kuna nini cha zaidi na sijui ni kipi hasa ninachoenda kukijibu huko” alijihoji Esther katika fikra
zake wakati alipokuwa njiani kuelekea sehemu ya tukio la ajali.
Aliyakanyaga mafuta ya gari na kumfanya
atumie mda mchache kuwasili eneo hilo. Kabla hajashuka kutoka kwenye gari lake
aliliona jopo la maaskari kadhaa waliokuwa wamevalia reflekta nyekundu. Alishuka
na kuelekea katika kundi lile na askari na kabla hajasema chochote alisikia
sauti ile ya inspekta Nyawenga ikimkaribisha “Habari! Bila shaka wewe ndiye sekretari
Esther” “Ndiyo haujakosea afande” alidakika Esther kwa
haraka haraka. “Sisi ni timu ya askari wapelelezi na usalama hivyo
tumefika hapa kwa ajili ya kuchunguza ajali iliyotokea hapa na kuchukua taarifa
zake, kikubwa tunaomba ushirikiano
katika hili” alizungumza inspekta nyawenga naye Esther hakusita
kuwapatia ushirikiano juu ya tukio lile.
Mmoja wa askari aliyekuwa ameshikilia
kijitabu kidogo cha kuchukulia maelezo pamoja na kalamu alianza kumhoji Esther
aliyekuwa akijibu kwa sauti ya mapozi. Zoezi lile lililopaswa kuchukua dakika
kumi na tano ilibidi ligharimu muda wa nusu saa kwani sauti ya mapozi iliyokuwa
ikitoka kwenye kinywa cha Esther pamoja na mavazi yake aliyokuwa amevalia siku
hiyo yalianza kumhamisha kamanda aliyekuwa akihoji juu ya suala zima la ajali
na kujikuta akihoji juu ya masuala mengine yasiyohusika. Kamanda huyo
alimalizia mahojiano hayo kwa kumuuliza Esther kama ameolewa au lah! … kwa
ufupi kamanda naye alianza kujikuta akiingia katika mtego wa Esther bila ya
kujielewa. Muda kidogo baada ya
mahojiano inspekta nyawenga alitoa shukrani zake kwa Esther juu ya ushirikiano
aliouonyesha katika zoezi lile bila ya kutambua yakuwa askari aliyehusika
kufanya kazi hiyo alikuwa ameshaanza kumtamani Sekretari Esther.
Inspekta nyawenga pamoja na na jopo lake walimuaga Esther na kisha
wakaondoka kuelekea kutimiza majukumu yao. Naye Esther alielekea moja kwa moja
ndani ya HYATT REGENCE HOTEL. Kila mfanyakazi ikiyemuona siku hiyo alikuwa na
shauku ya kutaka kufahamu juu ya hali ya Boss France, na kutokana na haraka aliyokuwa nayo ya
kutaka kurudi hospital kwa ajili ya kuhakikisha uangalizi wa karibu wa Boss
wake ilimuiwa vigumu kuzungumza na kila mfanyakazi. Alitembea haraka haraka
kuelekea katika ofisi yake na kuandika taarifa juu ya hali ya Boss France
pamoja na kuahirisha kikao kilichopaswa kufanyika siku hiyo “Hali ya Boss
wetu siyo mbaya na madaktari wanaendelea kupambana ili kuhakikisha anakuwa
salama na pia kikao kilichopaswa kufanyika siku ya leo kimehairishwa mpaka pale
kitakapoitishwa tena, Ahsanteni!” la hasha! Ulikuwa ni ujumbe ambao
ungewafanya wafanyakazi washindwe kufanya kazi zao kwa ufanisi ndani ya siku
kadhaa.
Baada ya kuandika ujumbe huo alinyoosha
mkono mpaka kwenye pochi yake akaibeba
na kuelekea upande wa sehemu iliyokuwa na kioo cha kujiweka sawa. Alijitazama
kwa muda kidogo kupitia kioo kile na kubaini ya kuwa hata macho yake
yanayoonekanaga kuwa na mvuto wa aina yake yalimsaliti kwa siku hiyo kwani sura
ya kupooza na uso wenye wimbi la huzuni vilimgubika. Hatukata kupoteza muda alijifanyia
make up ya dakika chache kisha akabeba pochi na simu yake, alipotaka kutoka nje ya ofisi yake akakumbuka
yakuwa aliuacha ujumbe wa taarifa juu ya hali ya Boss France. Alirudi
akauchukua kisha akaupeleka moja kwa moja katika moja ya ofisi za kusambaza
taarifa. Baada ya kufanya hivyo Esther alitembea kuelekea nje ya jengo hata
hivyo ilikuwa ni ngumu kwa baadhi ya wafanyakazi wenzake waliomuona kuweza kumsemesha
kwani hata uso wake ulikuwa ukisema wenyewe yakwamba hakuwa katika hali nzuri.
Wakati huo ndani ya AGA KHANI Hospital
ulikuwa ni wakati maalumu kwa ajili ya kuonana na wagonjwa naye mfanyakazi
aliyekuwa ameachwa na Esther pale Hospital kwa ajili ya kumpatia taarifa juu ya
hali ya Boss France alielekea katika ofisi ya Dr. Justine na kabla ya kubisha
hodi aliitwa na Dr. Adamu aliyehitaji kumuuliza jambo. Ilikuwa ni muda wa saa
nane kasoro mchana ambapo hata naye Dr. Adamu alipaswa awe amekwisha kuelekea
nyumbani kwake kwa ajili ya mapumziko. “Samahani dada, kuna jambo nahisi kama vile halijakaa sawa
kwa Esther kwani nini kilimsibu tofauti na hili la Boss wake kupata ajali” aliuliza
Dr.Adamu “Kiukweli mimi mwenyewe sifahamu chochote kinachoendelea” alijibu
mfanyakazi yule huku nafsi yake ikimsuta dhairi yakuwa alikuwa akizungumza
uongo lakini kama ilivyokuwa ada kwa Dr.Adamu naye hakusita kuendelea kuhoji. “Kwani
wewe unahisi kuna nini?, Ama kuna tatizo kazini kwake? na pia unaitwa nani?”
Looh! Yalikuwa ni maswali magumu kwa mfanyakazi huyo kuweza kuyajibia yote kwa
wakati huo kwani Dr.Adamu aliuliza maswali matatu kwa mfululizo. “Naitwa
Grace” Dr. Adamu akadakia kwa mkazo Gracee… “Ndiyo
Grace na ndilo jina langu kuhusu mengine sifahamu chochote” Grace alimjibu Dr. Adamu kana kwamba alikuwa
ni mtu aliyepandikiziwa kiburi na Esther.
Naye Dr. Adamu aliweka mkazo juu ya
jina la Grace kwa vile jina hilo halikuwa ni geni kwake kwani lilikuwa ni jina
sawa nala mpenzi wake walieachana wiki chache zilizopita. Grace alitaka kugonga
hodi katika ofisi ya Dr. Justine lakini Dr. Adamu alimtaka kuendelea kusubiri
kwanza ili akamilishe adhma yake. Dr. Adamu aligeuka na kukielekeza kichwa
chake juu kisha akaanza kugongagonga kwa kukikutanisha kidole chake cha Gumba na cha Ada dizaini ya
mtu alikuwa akifikiri kutaka kupongeza juu ya jambo fulani. Aligekuka tena na
kumtizama Grace ambaye naye alikuwa akimtizama Dr. Adamu kwa umakini
mkubwa, “Ahaaaaaah…! Alafu
nafikiri huu ni muda sahihi kwa ajili ya kuwaona wagonjwa sindivyo” alihoji
Dr. Adamu huku akimtolea macho Grace aliyeanza kumjibu “Mimi sijui ndo
mara yangu ya kwanza kuwepo hapa” Dr. Adamu alijaribu kutumia mbinu
mbalimbali za kumfanya Grace aweke umakini mkubwa kwake lakini ilikuwa ni
sawasawa na bure kwani kila mbinu iligonga mwamba huku lengo lake hasa ni
kutaka kupatiwa namba na Esther.
Basi hakuwa na namna zaidi ya kuwa muwazi
kwani alimuomba Grace ampatie namba za Esther naye Grace alikuwa mbishi, akajaribu kumuomba kwa mara nyingine lakini
ikawa ni jambo gumu tena. Na hapo ilimbidi apeleke mkono wake katika mfuko wa
nyuma wa suruali yake na kutoa kiasi cha pesa kilichokuwa kimesheheni noti
nyekundu kisha akamnyooshea Grace Loooh! Pesa ni pesa tu. Kwani Grace akusita
kuachia tabasamu zito na kuanza kuitafuta namba ya Esther katika simu yake bila
ya kuambiwa chochote kile na Dr. Adamu. Grace alimtajia Dr. Adamu namba za Esther na zakwake pia na kisha
wakaangaliana kwa muda na wote wakatabasamu.
Wakati huo akili ya Grace ilisahau hata
juu ya kile alichokuwa akitaka kukifanya, akajikuta akielekea Restaurant kwa ajili ya
kupata chakula naye Dr. Adamu alielekea katika ofisi yake . muda huo alionekana
kuwa mwingi wa tabasamua na furaha ilifikia hatua akawa anajitazama kwenye kioo
cha simu yake na kujicheka juu ya kile alichokuwa akikifanya. Hakutaka kupoteza
muda na mara moja alitaka kuipigia namba ile lakini alikuwa na dalili za
uoga, uoga. Alijikaza kisabuni na kisha akaipigia
namba ya Esther nayo simu ikaanza kuita na haikuchukua sekunde kadhaa simu ile
ikapokelewa. “Hallo.. hallo..” “Yes Hello!” aliitikia Esther kisha
akauliza “nani mwenzangu?” “A’m a’m Dr. Justine.. Justine… hapa
sijui umenisikia.. uko wapi” aliongea kwa utata mwingi kiasi kwamba
hata naye Esther alishtukia jambo lakini hakusita kumwambia kwamba yupo njiani
amekaribia kufika Hospital.
Baada ya kukata Simu Esther alijaribu
kupiga namba ya Dr. Justine aliyoichukua kwenye chumba cha mapokezi pale
hospital na namba hiyo ilikuwa hewani lakini iliita tu kwa muda bila ya majibu.
Kumbe wakati huo Dr. Justine alikuwa ametoka kidogo katika ofisi yake na kuacha
simu ndani, naye Dr. Adamu moyo wake
ulianza kumwenda mbio na kujijutia juu ya uongo aliojikuta ameuzungumza bila ya
kujielewa. Laah.. hasha!! Mawazo yake yalitofautiana na akili yake. Alibaki
kuwa mtu wa kuchungulia upande wa chini kupitia kwenye dirisha lake na ghafla..
alibahatika kuliona gari la Esther lililoingia kwa kasi kwenye geti la Hospital
Hoooh! Alijitolea macho kwa hofu na mashaka na hapo hakuwa tayari kusubiri
timbwili na mwanadada Esther kwani alitoka haraka haraka ndani ya ofisi yake na
kukumbilia upande wa mlango wa pili kuelekea Restaurant.
Mwisho
Je,
ni nini kitakachoendelea baada ya Esther kwenda kujua ukweli juu ya simu
ya Dr. Adamu aliyedanganya yakuwa yeye ni Dr.Justine?
Usikose mwendelezo wa sehemu ya tisa 09
Mwandishi: Sebastiani Masaba
Phone: 0746445197
0 Comments