Facebook

PESA ZA SHEMEJI SEHEMU YA SABA 07

https://shimazone.blogspot.com/2021/01/pesa-za-shemeji-sehemu-ya-sita-06.html


Esther alilifikia gari la Boss France huku akiangua kilio kikubwa na kizito sana wakati huo wafanyakazi wenzake na watu wangine waliofika katika eneo lile walikuwa wakifanya juhudi za kumuwahisha Boss France hospital kwa ajili ya kuokoa maisha yake Naye Esther ambaye ndiye aliyekuwa Sekretari wa Boss France aliwataka wampandishe Boss France katika gari lake kwani kwake ilikuwa ni ngumu kuweza kuendelea kusubiria gari la wagonjwa lifike katika eneo lile huku akiona hali ya Boss wake kuwa mbaya zaidi.

Na hatimaye watu waliokuwepo katika eneo la tukio walimpandisha Boss France katika gari ya Esther huku Esther naye akiwa ni msaada tosha katika hilo kwani naye alikuwa amembeba Boss wake na kumpandisha ndani ya gari huku akiendelea kububujikwa na machozi. Alimuomba mmoja wa wafanyakazi wenzake aliyekuwepo katika eneo lile kumtaka kumsindikiza    

kuelekea Hospital ingawa umati mkubwa uliokuwa eneo lile ulitamani kufanya hivyo kama sehemu ya kumkarimu Boss France ambayd alikuwa ni kipenzi cha wengi. na mara moja bila ya kutaka kupoteza muda Esther aligeuza gari lake na kuliondoa kwa mwendo wa haraka huku shauku yake kubwa ni kuhakikisha anafanya kila uwezekano wa kuokoa maisha ya Boss wake.

Basi kulingana na mwendo aliokuwa nao Esther haikuwachukua muda sana kuikaribia Hospital Looh! Kwa kadri walivyozidi kusogea walianza kuyaana maandishi ya AGA-KHANI HOSPITAL kwa ukaribu zaidi. Kwa bahati mbaya  hiyo ndiyo hospital iliyokuwa imemlaza Vicky mmoja wa wafanyakazi wa Hyatt Regency The Kilimanjaro Hotel aliyekuwa akihusika na kitengo cha uhasibu. Esther aliingiza gari hadi ndani ya geti na mara moja wahudumu wa huduma ya kwanza waliweza kufika kwa ajili ya kumpokea Boss France na kuanza kumpatia huduma za kitabibu. “Ooooh! My God sikuweza kutaraji jambo kama hili” Esther alinena huku akishusha pumzi kwa uzito wa tukio lile.

Wakati huo Esther pamoja na yule mmoja ya wafanyakazi aliyeambatana naye walikuwa wakiendelea kufuatilia kwa ukaribu juu ya huduma alizokuwa akipatiwa Boss France.

Esther alikuwa mwenye kuhaha na mwenye hofu kubwa juu ya Boss wake mpaka kufikia hatua ya kutamani kumuuliza kila daktari na nesi aliyekuwa akikatiza mbele ya macho yake juu ya hali ya Boss France. Esther na mwenzie waliendelea kuketi kwenye moja ya sofa za wageni waliokuwa wakiwasindikiza wagonjwa wao pale hospital. Kwa mbali kuna daktari mmoja aliyekuwa akitembea kuja katika eneo alilokuwa ameketi Esther na mwenzie, na baada ya hatua chache aliweza kuwasili mahala pale “Habari za Asubuhi, naitwa  Dr.Adamu ni Dkt mkuu msaidizi wa AGA-KHANI  HOSPITAL” aliyasema hayo Dr. Adam naye Esther alidakia “Esther hapa sekretari mkuu wa Hyatt Regency The Kilimanjaro  Hotel” aaaah! Kumbe ndiyo wewe, aliitikia Dr.Adam kwa mshangao mkubwa na akiwa na imani kwamba Esther na mfanyakazi mwenzie walikuja pale kwa ajili ya kumuona Vicky aliyeletwa na Boss France na kulazwa  hapo usiku wa kuamkia siku hiyo pasipo kufahamu kilichomkuta Boss France.

Dr.Adamu aliendelea kuwasemesha akina Esther “Nadhani bila shaka mtakuwa mmeshafuata taratibu zote basi mnaweza kwenda kumuona mgonjwa wenu na amelazwa wodi namba 5 V.I.P” maneno hayo ya Dr. Adamu yaliwashtusha akina Esther kwani wodi namba tano ilikuwa ikihusika kuwalaza wagonjwa wa jinsia ya kike. “Mmmmh,  Kwani Dr.Adam mbona mgonjwa wetu kama vile ameingizwa upande mwengine na bado yumo kwenye matibabu” aliyasema hayo Esther huku akimtolea macho Dr.Adamu kwa mshangao mkubwa,  Alaaah! Naye Dr.Adam alishtuka na kuanza kufikiri huenda akawa ni mtu mwingine muhimu ndani ya Hyatt Regence The Kilimanjaro Hotel.

Kwani uwepo na sekratari ulimpa maswali mengi zaidi. Aliendelea kufikiri kwa muda huku akijiuliza kwamba mtu huyo huenda angekuwa ni nani maana masaa machache nyuma alikuwa na Boss France pale Hospital hivyo hakutaka kuamini kama angekuwa ndiye lakini ghafla alikumbuka lisaa limoja nyuma mpaka kufikia muda huo namba ya Boss France haikuwa ikipatikana akataka kulithibitisha hilo kwa kuendelea kuipigia namba ya Boss France. “Asante kwa kutumia mtandao wa Vodacom namba unayoipigia haipatikani kwa sasa tafadhali jaribu tena badae” na hayo ndiyo majibu aliyoambulia Dr. Adamu kutoka kwenye simu yake. Looh....! Weee.

Mapigo ya moyo yalimwenda mbio Dr.Adamu na alipomtazama Esther kwa wakati huo alimuona amejiinamia huku akiendelea kutokwa na machozi. Dr. Adamu aligeuka kwa Haraka dizaini ya Mwanajeshi aliyekuwa akikwepa risasi na kukimbilia katika chumba cha wagonjwa wa dharura na alipofika alitizama kulia na kushoto kwa haraka haraka Daaah!.. Alifanikiwa kumuona Boss France aliyekuwa amejeruhika katika eneo lake la usu pamoja na mguu wa kulia,  alijisikia huzuni sana na hapo kumbukumbu ya usiku wote wa jana ikamjia juu ya namna ambavyo Boss France alikuwa akipambana kuhakikisha Vicky anarejea katika hali yake. Alitoka nje bila ya kumsemesha mhudumu yeyote aliyekuwa ndani ya eneo lile nao walibaki kumshangaa Dr.Adamu pasipo kupata majibu sahihi juu ya jambo lile

Dr.Adamu alielekea katika eneo alilokuwa amekaa Esther na mwenzie na ghafla Esther alisimama haraka na kumsogelea Dr.Adamu na kutaka kujua juu ya hali ya Boss France. “Kuna nini kwani?, Kipi kinachoendelea Dr.Adamu” Aliuliza Esther aliyeonekana kuwa na wimbi kubwa la moyo wa majonzi. Dr. Adamu alieendelea kukaa kimya huku akimtazama Esther machoni. Kitendo hicho kisichokuwa na majibu kiliendelea kuongeza jeraha ndani ya moyo wa Esther na kumfanya aendelee kulia kwa uchungu.

Kuna nini jamani? Ilisikika sauti nzito iliyotekea upande wa kushoto wa eneo walilokuwa watatu hao Sauti hiyo nzito ambayo ilikuwa ya kwanza kutambulika na Dr. Adamu haikuwa ya mwingine tofauti na Dr. Justine ambaye ndiye alikuwa ni Daktari mkuu wa pale AGA-KHANI HOSPITAL. Wote walishtuka na kutizama sauti ile ilipokuwa inatokea “Ahaah! Karibu Boss” alikuwa ni Dr. Adamu aliyeyasema hayo huku akipeleka mkono wake wa kulia mbele kutaka kumsalimia Dr. Justine. “Asante sana... mbona mko katika hali hiialiendelea kuuliza Dr. Justine huku akimtizama Dr. Adamu. Baada ya kimya kidogo Dr. Justine alimtaka Dr. Adamu aweze kuambatana naye kuelekea katika ofisi yake ili kuweza kufahamu zaidi juu ya tukio lile. Wakati huo naye Esther aliyekuwa katika hali ya majonzi na wimbi la kusongwa na mawazo kichwani mwake alianza kufikiria juu ya kile kilichotokea asubuhi na mapema wakati Boss France alipompigia simu na kumuuliza juu ya kikao cha siku hiyo. “Nakumbuka aliniuliza juu ya kikao lakini nadhani hakutaka kuishia hapo kwani kuna jambo jingine alilotaka kunijuza wakati nilipokata simu yakealijiuliza Esther katika fikra zake na kuhisi huenda palikuwa na kitu za ziada asubuhi ile alipopigiwa simu na Boss wake.

Ndani ya ofisi ya Dr. Justine yaliendelea mahojiano baina yake na Dr. Adamu juu ya yale yote yaliyokuwa yametokea naye Dr. Adamu alisimulia matukio yote kuanzia usiku aliompokea na kumlaza Vicky aliyekuwa chini ya uangalizi wake kwa maagizo ya Boss France. Aseee! Dr. Justine alihuzunika sana kwani Boss France alikuwa ni mmoja wa marafiki zake wakubwa aliyesoma naye chuo kimoja huku kila mmoja akisomea fani tofauti na pia alikuwa ni m,bia mwenzake waliokuwa wanashea hisa katika kampuni ya Vodacom.

Na hapo hakutaka kupoteza muda kwani alihitaji kuelekea moja kwa moja katika chumba alichokuwemo Boss France. Alitoka ndani ya ofisi yake huku akioneka mwenye haraka ya kutaka kuwahi kumuona rafiki yake Boss France. Alifika ndani ya chumba alichokuwemo Boss France na wakati huo naye Esther alisimama na kukimbilia katika eneo la chumba hicho. Kwa bahati mbaya Esther alizuiliwa kuingia ndani ya chumba hicho na kitendo kile kiliendelea kuivuruga sana akili yake kiasi cha kutamani kuuvunja mlango ule ili aingie ndani walau kumwona Boss wake. Dr. Justine alimtizama Boss France ambaye kwa wakati huo alianza kurejesha fahamu zake huku akiita “Vicky... Vicky... Vicky... Maneno hayo aliyokuwa yakimtoka Boss France kwa sauti kubwa yaliweza kumshtua Esther aliyekuwa amesimama pale mlangoni kisha akajiziba mdomo wake uliokuwa ukitaka kutoa sauti ya mshtuko ule na kuanza kupata picha halisi ya tukio lile la asubuhi kuhusu simu ya Boss wake.

 Papo hapo bila ya kufikiri sana Esther alianza kutoka mbio kukimbilia katika wodi namba 5 ili kujua  na kuthibitisha ni mgonjwa gani aliyekuwemo mule V.I.P lakini wakati akianza kuyafanya hayo kichwa chake kiligeuzwa na sauti iliyokuwa ikimuita kwa msisitizo mkubwa,  Boss,  Boss,  Boss. Sekretari” alikuwa ni yule mfanyakazi aliyekuja naye pale hospital kumleta Boss France aliuliza Esther “Khaa! Mbona hivyo umenishtua sana wewe kwani kuna nini?” “kuna namba ngeni imepiga hapa lakini inaonekana kama vile niya taasisi fulani” alizungumza yule mfanyakazi huku akiikabidhi simu kwa Esther ambaye alipokea namba ile moja kwa moja bila ya kufikiri juu ya jambo lolote. “Hello! Unaongea na Inspekta Nyawenga hapa, nipo katika eneo la tukio la ajali pamoja na timu yangu nzima. hivyo tunakuhitaji haraka sana.” Na ndicho alichokutana nacho Esther punde tu baada ya kupokea simu ile. Loooh! Mapigo ya moyo wa Esther yalimwenda kasi kiasi cha moyo wake kutaka kumchomoka na mbaya zaidi hapakuwa na nafasi ya yeye kuhoji juu ya suala lile zaidi ya kufuata maelekezo. Mwili wake ulikufa ganzi na kudhoofu ghafla,  mithili ya mti uliopigwa na radi na asijue ni nini cha kufanya kwa wakati huo.

***Mwisho***

 

Je ni nini kitakachoendelea na kipi atakachokifanya Esther baada ya kuanza kupata majibu ya kile alichokuwa anakihisi juu ya simu ya asubuhi ya Boss france na baada ya kupata simu ya dharura kutoka kwa inspecta nyawenga.?

Endelea kufuatilia miendelezo ya tamthiliya pendwa ya pesa za shemeji. Sehemu ya nane 8 jumamosi ijayo.


MWANDISHI SEBASTIN SEBA

MAWASILIANO: 0746445197

EMAIL;masabaseba123@gmail.com





Post a Comment

0 Comments