Facebook

PESA ZA SHEMEJI SEHEMU YA SITA (06)


Looh! Almanusura Vicky agongeshe kichwa chake ukutani lakini zilikuwa ni Juhudi za Boss France aliyeruka kama mwewe

aliyeona kifaranga cha kuku kikiteatea na kukinyakua mara moja. Kwa mikono yake Boss France Vicky alipata usalama usiokuwa na malipo. Ilibidi wamlaze na kuendelea kumpatia matibabu chini ya uangalizi wa Dr. Adam. Kiza cha usiku wa manane kilikuwa kimeshatanda na ngurumo za upepo kutoka bahari ya Hindi zilikuwa zikisikika, Minazi nayo ilikuwa ikiyumba kuelekea kulia na kushoto,  JiJi la Dar-es-salaam lilikuwa tuli huku liking'arishwa na Mianga ya taa zilizoonekana kila upande.

Basi Kutokana na uchovu aliokuwa nao Boss France alianza kusinzia pale kitandani naye Dr. Adam hakuwa na neno baada ya kumhudumia Vicky alitoka na kuelekea katika ofisi yake. Majira yalizidi kusonga huku kimya cha kutosha nacho kikiwa kimetawala kwani hapakuwa na hata mmoja wa kumsemesha mwingine kwa wakati huo huku kila mmoja akiwa katika wimbi zito la usingizi. Mara ghafla Boss France alishtushwa na Sauti ya Vicky   iliyosikika kuhitaji msaada wake “Boss France nisaidie” “Boss France hauwezi ondoka” “Boss France nisaidie”  sauti hiyo iliendelea kusikika mara kadhaa ingawa ilikuwa ya ladha yake lakini ilimtia uwoga Boss France na kumfanya amtolee macho Vicky, mapigo ya moyo yakamwenda kasi huku jasho jembamba likianza kumtiririka. Lakini Baada ya muda mfupi Boss France aligundua kuwa ile ilikuwa ni ndoto ambayo Vicky alikuwa akiiota huku akiweweseka , ikamlazimu Boss France aheme kwa kushusha pumzi na mapigo ya moyo yakaanza kupungua taratibu.

Alisimama na kuangaza kulia na kushoto na hakuweza kubaini chochote kile cha tofauti zaidi ya kuona mandhari iliyokuwemo mule ndani. Haikuchukua masaa mengi mwangaza ulianza kuonekana kwa nje na kiza kilianza kutokomea wakati huo Vicky alikuwa bado katika hali ya usingizi mzito,  Naye Boss France alifikiri zaidi juu ya shughuli za kiofisi. Alimsogelea Vicky kisha akamshika katika mkono wake wa kulia na kupeleka mdomo wake ulioachilia busu zito huku akijisemea moyoni mwake kwamba “Usijali Mamaa lazima nihakikishe unakuw salama siku zote” zilikuwa ni hisia nzito na zenye kusisimua kutoka kwa Boss France ambazo zingemfanya Vicky ajione yupo katika Dunia ya tofauti lakini haikuweza kuwa hivyo kwani Vicky kwa wakati huo, hakuweza kutambua chochote kilichofanywa na Boss France kutokana na hali ya kuwepo katika wimbi zito la usingizi.

Boss France aligeuka na kuanza kuujongelea mlango kisha akaufungua na kotoka nje huku macho yake yakimtazama Vicky aliyeoshesha uso wa tabasamu na wenye kuvutia ingawa bado alikuwa amelala. Alielekea moja kwa moja katika ofisi ya Dr. Adamu akabisha hodi kisha akaingia ndani, Alimsalimu kama ilivyoada na tamaduni zetu sisi Watanzania naye Dr.Adamu hakusita kuichangamkia salamu ile ya Boss France. Baada ya salamu Boss France alizamisha mkono katika mfuko wake wa nyuma na kuchomoa wallet yake kisha akiifungua na kutoa kiasi kingi cha noti za elfu kumi akampatia Dr.Adamu na kumtaka amhakikishie juu ya usalama wa Vicky naye Dr. Adam alimhakikishia hilo Boss France. Walipokwisha kukubaliana waliagana kisha Boss France akatizama saa yake ya mkononi na kuona kwamba ilikuwa imekwisha kutimia majira ya saa kumi na mbili kasoro Asubuhi. Laaah! “Sijui leo itakuwaje kuhusu kikao sidhani kama nitawahi kweli” alijisemea Boss France huku akitembea haraka kuelekea nje alipopaki gari lake na alipofika kama kawaida yake hakusita kuanza kulikagua kwa macho na baada ya kujiridhisha akaingia ndani ya gari na kuliwasha huku akiwa na hesabu za kuelekea kwanza nyumbani kwake Oyster bay alianza safari  na kabla hata ya kufika mbali alipokea simu yake ya mkononi iliyosikika kwa sauti ya mtu aliyetaka kufahamu alipolazwa Vicky.

Ilikuwa ni vigumu sana kwa Boss France kuweza kutoa majibu ya moja kwa moja kwa sababu alihofu sana juu ya usalama wa Vicky na alifikiri mbali zaidi kwa sababu hakuweza kuitambua sauti ile ilikuwa niya nani. “Samahani naongea na nani?” alihoji Boss France “naitwa Calvin mmoja ya wale waliokuwa wameambatana na Vicky kuja kule HAVOC NIGHT SPOT CLUB”…. “Ohooh!...” aliitikia Boss France kwa mshangao. Hakuweza kuendelea kujadili sana kwa ajili ya hilo kwani alikuwa na safari ya kuwahi kuelekea nyumbani kwake Oyster bay kwa kufikiri hilo alimuelekeza ni wapi alipolazwa Vicky lakini kabla ya kuendelea na safari yake alikumbuka juu ya Erick mmoja wa mabamnsa wa HAVOC NIGHT SPOT CLUB aliyeambatana naye siku ya usiku wa jana wakati wakimpeleka Vicky Hospital. Ila Kwa bahati mbaya hakuweza kuwa na mawasiliano yake kwa wakati huo hivyo ikambidi asijali sana kwa kuhisi kwamba lazima Erick atakuwa salama na hasa akizingatia uzoefu wa kazi yake. Aliendelea na safari ya kuwahi nyumbani kwake ingawa palikuwa na umbali wa kiasi chake lakini hakujali hilo,  njiani alikuwa ni mtu mwenye wingi wa mawazo hasa akiwaza zaidi kuhusu Vicky pamoja na kikao cha siku hiyo. Na mbaya zaidi Vicky naye alikuwa ni mmoja ya wakuu wa vitengo mbalimbali ndani ya HYATT REGENCY HOTEL hivyo Boss France aliwaza ni majibu gani hasa angeyatoa mbele ya wajumbe wengine wa kikao kile juu ya kile kilichomkuta Vicky. La hasha!.. Ulikuwa ni mtihani mzito.

Safari ya kwenda nyumbani kwake Oyster bay  ilianza kusuasua akafikiri kwamba ni bora zaidi aelekee moja kwa moja eneo lake la ofisi kwani angeweza kupata huduma zote ingawa ilikuwa ni mapema mno tofauti na mda wake uliozoeleka wa kuingia kazini. Lakini  zuri zaidi palikuwa na duka la nguo aina ya suti ambapo kwake yeye isingeweza kuwa changamoto kuweza kuzipata kulingana na uwezo aliokuwa nao ingeweza kuwa rahisi kwake kukubaliana na mawazo yake hasa akizingatia na ugumu wa foleni ya magari yaliyokuwa mbele yake kwa muda huo.

 Aligeuza gari na kuelekea kazini kwake, wakati akiwa njiani alichukua simu yake na Kumpigia Sekretari wake  Esther lakini simu yake iliita kwa muda mrefu bila ya majibu hivyo hakuwa na budi kupiga kwa mara nyingine na baada ya mda mfupi ilisikika sauti ya Mrembo Esther aliyekuwa akizungumza kwa mapozi ya usingizi La hasha!.. Ilikuwa ni sauti nyororo nayakuvutia kiasi kwamba asingetamani kukata simu hata baada ya kueleza jambo lake. “Hello Boss France Kwema kweli mbona leo simu ya mapema sana…..? Alizungumza kwa kuvuta maneno “Yes ahaah… no yeap ni kwema kiasi” “Yeap yeap ni kwema” Boss France aliendelea kuzungumza huku akiwa na kigugumizi kikali lakini Esther aligundua kwamba kuna jambo la tofauti kwa hali ile aliyoibaini kutoka kwa Boss wake.  “Kuhusu kikao maandalizi yako vipi?” aliuliza Boss France “Ndiyo Boss hakuna kilichokaa vibaya mambo yote yako sawa” lilikuwa ni jibu la Esther baada ya swali la Boss wake.

 Boss France alitamani kumjuza Esther juu ya kile kilichomkuta Vicky lakini mdomo wake ulikuwa mzito dizaini ya mtu aliyewekewa gunzi mdomoni hivyo hakaona isingeweza kuwa sahihi kwa wakati huo kumjuza Esther juu ya tukio lile. Basi  Esther aliamua kukata simu baada ya kuona kimya cha muda naye Boss France alisikika akiita “Eeesther wewe Eee…..” Aliishia kusema hivyo. Looh! Kuna namna ambavyo Boss France alianza kuchanganyikiwa na msongo wa mawazo,  aligongagonga mikono yake kwenye ustelingi wa gari huku akionyesha hali mithili ya mtu mwenye mgogoro na nafsi yake. Lami ilikohoa vumbi kwa namna ambavyo Boss France alikuwa akiendesha lake na haikumchukua mda alikuwa amekaribia kufika katika eneo la HYATT REGENCY HOTEL lakini siku hiyo ilikuwa ni siku ya kutimia kwa msemo kwamba “Asiye na bahati habahatiki kamwe” kwani kutokana na msongo wa mawazo aliyokuwa nao Boss France ulimpelekea kufanya vitu visivyo sahihi. Aliendeshe gari kwa mwendo wa kasi mno na ghaflaa… alipokuwa akikata kona kuingia katika geti la HYATT REGENCY HOTEL huku akijaribu kushika breki ya gari kwa haraka alijikuta akilivaa geti na gari kujigonga na mkito wa sauti ile ulisikika kwa sehemu kubwa ya eneo hilo na kuwashtua wengi.

Na hapo Boss France alipoteza Fahamu na kishindwa kuelewa kilichokuwa kikiendelea kwa wakati huo. Kelele kubwa ya “Uwiiiiiiii jaman Boss France… Boss France…” iliyosikika kwa nguvu iliendelea kuwashtua wengi na kukimbilia eneo la tukio na ilikuwa niya mmoja wa wafanyakazi wa usafi aliyebahatika kushuhudia tukio lile lililomkuta Boss France ili kutaka msaada wa haraka. Watu wengi sana walijazana katika eneo lile huku kila mmoja akiwa na taharuki ya tukio lile. Haikuchukua mda kwa Esther aliyekuwa akielekea kazini kufika katika eneo lile kwani naye aliamua kuwahi kazini siku hiyo na ni baada ya kuhisi hapakuwa na utimamu kwa Boss France. Alishuka mara moja katika gari lake na kutupa pochi yake kutokana na mshtuko alioupata huku akilikimbilia gari la Boss France na kulia kwa sauti ya huzuni “Mungu wangu jamani Boss France Mamaa Boss wangu jamani…….”

Je,  ni nini kitakachotokea Baada ya tukio lile lililomkuta Boss Fance ambaye alimwacha Vicky Hospital na kuahidi kumhudumia kwa kila hali?


MWANDISHI: SEBASTIAN SEBA 
                                            +255 746 445 197

Post a Comment

1 Comments