Hatimaye ikawa ni moja ya siku mbaya na isiyobahati kwa Mijanja na hata kwa familia ya Mzee Magoti kwa ujumla wao kwani kila mmoja alipopata taarifa hizi alibaki akiduwaa na kustaajabu kwa yaliyotokea na mbaya zaidi Msichana yule alitoweka usiku kwa usiku katika mazingira ya kutatanisha pasipo wao kuweza kumfahamu hata kwa jina.
Baada
ya usiku huo wa kizaazaa kupita Mzee Magoti aliamua kukaa pamoja wa familia
yake ili kuweza kujadili kidogo juu ya lile tukio kwani lisingeweza kuwa la
kawaida hasa kwa mtu aliyeweza kusaidiwa na kupewa hifadhi kisha akatoweka hata
kabla ya mawio kuwia. Mzee Magoti alihoji huenda binti yule alikuwa ni kiumbe
kisicho cha kawaida Mzee Magoti: “Isije ikawa tulitoa msaada na
kukaribisha jini ndani ya nyumba yangu” . Lakini hakukuwa na hata mmoja
wa wanafamilia wake aliyeweza kutoa jawabu juu ya tukio hilo huku hofu na uoga
ukiwatanda katika fahamu zao.
Jambo
lile likaendelea kubaki kuwa la siri ndani ya familia ya mzee magoti bila hata
ya mmoja ya wanakijiji wengine kuweza kufahamu. Mijanjaa alirejea ndani ya
chumba chake na kujitupa kitandani mwake alikuwa mwenye sononeko la moyo na
aliyekosa amani akajiuliza ndani ya nafsi yake “ “Hivi kweli
inawezekanaje mtu kuweza kufanya jambo hili la kutoweka tena ikiwa ni mtoto wa
kike, na giza lote lile, mvua yote na
radi yate ile iliyokuwa ikinitisha hata mimi hapana kwakweli bado hainiingii
akilini” Aliendelea kuwaza na baada ya sekunde chache akakumbuka juu ya
rafiki yake mkubwa aitwaje Mwagani.
Huyo
alikuwa ni rafiki mkubwa wa mijanja na ambaye amekuwa akimshirikisha mara
nyingi juu ya mambo yake hata wakati wa kuwinda pamoja na kuteka maji mtoni
hupenda kuwa pamoja naye. Hatimaye siku hiyo mada kuu iliyotawala katika vijiwe
mbalimbali ndani ya kijiji cha korona ilikuwa ni kuhusiana na radi kubwa na
hali ya ajabu ambayo haijawahi kutokea katika kijiji hicho kwa miaka mingi.
Zuena
mama wa familia na mke wa Mzee magoti alikuwa akifagia,fagia katika eneo la
nyumba yake, na mara tu alipogeuka na kuangusha macho yake mbele alibahatika kuona cheni yenye rangi ya dhahabu
iliyokuwa imetepeta kwa damu nzito lakini kila alipojaribu kuisogelea kwa
ukaribu zaidi, aliona ile rangi na kile
kiwango cha damu kikizidi kutoweka katika cheni ile. “Kheeeh! Hichi ni
nini tena? mbona sijapata wahi kuona katika maisha yangu yote” alijuuliza
Zuena huku akipigwa na butwaa na asijue afanye nini kwa wakati huo lakini
wakati akiendelea kuduwaa na fahamu zake kudhoofu kutokana na tukio lile kwa
mbali alisikia mluzi ukipigwa, mluzi huo
ulipigwa mara tatu ikiwa ni alama ya kuashiria jambo fulani.
“Hodi
hodi hodi” “karibu” hiyo ilikuwa ni sauti ya Mwigani rafiki yake na Minjaa
iliwepewa heshima ya kakaribishwa na Zuena.
Mwigani: Shikamoo Mama
Zuena:
Marhaba
mwanangu karibu
Mwigani:
Ahsante
mama, Nimekuona tokea mbali ukiwa unaangaza chini kwa muda mrefu
sana tena kwa mshangao mkubwa Je, kuna
nini?
Zuena:
hakuna
lolote mwanangu hata usijali, rafiki
yako yuko ndani unaweza ukamuona. Majibu ya Zuena yalimfanya Mwigani achezwe na chale na
kuhisi huenda kuna jambo alililofichwa na Zuena hivyo akaamua kupitiliza moja
kwa moja hadi kwenye chumba cha mijanja na kumkuta rafiki yake akiwa katika
hali ambayo hakuwahi kuizoea. Siku hiyo Mijanja hakutaka rafiki yake Mwigani aweze kubaini jambo lolote juu ya lile
lililoikumba familia yake. Alijichangamsha na kujifanya mwenye furaha kila
wakati ilihali tu kumfanya rafiki yake asiweze kugundua jambo lolote. Muda
ulikwenda mpaka kufikia majira ya saa kumi na mbili jioni huku wawili hao
wakiwa katika wimbi la stori mbalimbali zilizohusiana na kijiji chao. Mwigani alifikiri
kidogo na kumtaka rafiki yake Mijanja walau waweze kutoka nje kwa mda kwani
walikaa ndani kwa muda mrefu mpaka kufikia majira ya jioni. Mijanja alifikiri
juu ya wazo la rafiki yake huku vidole vyake vikiendelea kuburudisha udevu wake
kwa kuukunakuna. Baada ya sekunde chache aliapata wazo alilolihisi huenda
lingefaa zaidi “nafikiri ni kheri tukatweke maji mtoni” alisema
mijanja huku akiendelea kumchagiza rafiki yake mwigani kwamba huko wangeweza
kupata upepo mzuri na tulivu pamoja na sauti nzuri na zenye kuvutia za ndege wa
aina mbalimbali. Mwigani hakuwa na shaka wala ubishi wowote juu ya wazo la
rafiri yake hivyo walibeba mitungi ya maji na kuelekea katika mto yambwa.
Wakati
huo ilikuwa ni jioni tulivu ambayo haikuwa na purukushani za watu wengi
kuelekea wala kutoka mtoni. Upepo tulivu na wenye kiubaridi chenye ushawishi
nayo ulikuwa ukiyanong'oneza masikio yao, sauti za kuvutia za ndege mbalimbali
na zilizokuwa na uwezo wa kuyashibisha masikio yao nazo zilikuwa zikivuma kwa
ustadi wa aina yake,
Maua
mazuri ya kupendeza pale uyatazamapo na yenye rangi mbalimbali zenye uwezo wa
kuyalisha macho na kuyafanya yaweze kushiba nayo yalishamiri pembezoni mwa njia
iliyokuwa ikielekea mtoni. Mijanja alisogea pembeni na kuchuma moja ya ua
lililokuwa limemvutia kisha akalinusa. Ua lile lilikuwa na harufu nzuri sana lakini
kitendo kile kiliweza kupelekea mwili mzima wa mijanja kusisimka kama mtu aliyepigwa
na shoti lakini hakujali kuhusu hilo kwani alilitupa ua lile na kuendelea na
safari yao.
Walitembea kwa muda kidogo na wakawa
wamekaribia kufika katika mto yambwa. Kwa mbali kidogo Mijanja aliona Kama kuna
mtu mmoja aliyekuwa akiogoa pale mtoni, alimgusa rafiki yake begani na
kunyoosha kidole chake kimoja kule mtoni ikiwa ni ishara ya kumjuza juu ya
jambo lile. Mwigani alishtuka na kujiziba mdomo wake ili asiweze kupiga kelele
kwani alipomtazama vizuri mtu yuke aligundua ya kuwa alikuwa ni msichana.
Mwigani alishtuka zaidi maana pia kwake lilikuwa ni jambo geni kulishuhudia.
Walisogea pembezoni mwa mti mrefu na kujibanza ili kuendelea kumtizama yule
msichana.
Hawakuweza
kumuona msichana yule vizuri kwa kadri ya matamanio ya hisi zao ikabidi wapende
juu ya ule mti ili waweze kuyafurahisha macho yao zaidi. Walipofika juu ya mti
ule kila mmoja aliweza kumuona na kumtizama msichana yule vizuri zaidi. Laaah!
Mash allah!... Hakuna hata mmoja aliyeweza kutaraji wala kuwahi kufikiri kumuona
msichana wa dizaini ile katika maisha yao pale kijijini Kwani alikuwa ni msichana
aliyejikamilisha kwa kila kitu kuanzia juu mpaka chini.
Msichana
huyo alionekana kuwa na rangi nyeupe katika mwili wake, kichwa chake
kilifunikwa na nywele ndefu za singasinga zilizokolea weusi mtupu na zilizokuwa
zimetanda katika mgongo wake, Miguu ya bia balimi iliyokuwa imeungana na paja
zenye chirizi za mbali, shepu lake matata lilijichora umbo namba nane isiyokuwa
katikati ya sita wala saba, huku Kilimanjaro mlima ukimea pale zilipoishia
nywele zake. Loooh....!!! Kwa ufupi alikuwa ni msichana mzuri sana ambaye angeweza
kuzikonga hata nyoyo za wavuvi kulima mpunga pale akatizapo mbele ya macho yao.
“Mhhhh...! Kwakweli sijapataona jambo kama hili tangu nimezaliwa” Alitoa
ghuno Mwigani ambaye pia aliendelea kuwa na kiwewe cha kustaajabu juu ya jambo
lile.
Mijanja
alitamani ashuke juu ya mti na kumfuata msichana yule pale mtoni lakini rafiki
yake alimzuia kwani bado alikuwa na moyo wa shaka kwani haikuwa ni jambo la
kawaida kumuona msichana mzuri kama yule akiwa pale mtoni peke yake kwa muda
kama ule. Lakini ilikuwa ni ngumu kwa mijanja kuweza kuelewa akisemacho rafiki
yake kwani akili na fahamu zake zilishapaa juu zaidi. “Hapana Mwigani
nadhani ni msichana wa kawaida kama walivyokuwa wasichana wengine hapa kijijini
ila tu kawazidi kwa uzuri” alisema Mijanja huku akiendelea kushuka
kwenye mti kuelekea mtoni alipo yule msichana. Mwigani naye aliona kuna haja ya
kushuka na kumfuata rafiki yake.
Mijanja
alikuwa wa kwanza kuteremka na kuanza kujongea kumfuata yule msichana, lakini kila alipoendelea kusogeza hatua zake
mapigo ya moyo yalimwenda kasi na mwili ulizidi kumsisimka kwa ouga ambao
hakuweza kutambua ulitoka wapi. Wakati huo giza jembamba lilianza kushamiri na
punjepunje za baridi nazo ziliendelea kukolea pale mtoni.
Mijanja
aliendelea kujongea na kufika karibu zaidi kwa yule msichana aliyekuwa
amegeukia upande wa pili na kuucha wazi mwili wake wote kwa upende wa nyuma. “Muyara..
awee muyara...” aliita muyara akimaanisha msichana kwa lugha yao lakini
msichana yule hakuweza kugeuka wala kusema chochote zaidi na kuendelea kuyachezea
maji kwa mikono yake. Naye Mijanja hakukata tamaa bali aliendelea kuita huku
akiwa na shauku ya kutaka kumtambua msichana yule pindi atakapogeuka.
Ghafla msichana yule aligeuka huku akitabasamu
bila ya kusema chochote na ilikuwa ni baada ya mijanja kumuita mara tatu tatu
mfululizo “Muyara, muyara, muyara” loooh! Mijanja alijikuta
akishtuka kwa uoga uliomuingia na kuteleza kuangukia ndani ya mto alipokuwa yule
msichana. Mwigani rafiki yake na Mijanja
aliyekuwa na hofu tangu mwanzoni alipiga mbiu kwa nguvu iliyoweza kusikika kule
kijijini kisha akaanza kukimbia baada ya kushuhudia tukio lile lililomkuta
rafiki yake. Alikimbia kwa kasi huku mwili mzima ukimtetemeka na jasho zito
likimmwagika mara ghafla alijikuta akikitwa na kitu kizito kisichofahamika
kichwani mwake, akaanguka chini na kupoteza fahamu zake.
**MWISHO**
Endelea
kufuatilia miendelezo ya tamthiliya hii ili uzidi kuburudika na kuelimika
Mtunzi na mwandishi- Sebastian masabha
Mobile no: 0758-162527
Whatsapp 0746-445197
0 Comments