Kile
kibao kizito alichokipokea dkt. Justine kutoka kwa Esther ilikuwa ni ishara
tosha ya kwamba hakuwa katika matazamio yoyote ya kihisia kwa Esther. Aliokota
miwani yake na kuelekea katika gari lake huku akitoa maneno yenye vitisho kwa Esther
ya kwamba ipo siku utakuja kunipigia magoti naye Esther aliyekuwa mwingi wa
hasira na mawazo kwa wakati huo hakusita kumjibiza Dkt. Justine na kwa
kumwambia “Nadhani pengine utaanza wewe na mimi ndo nitafuatia kufanya
hivyo” ikawa hivyo na hatimaye
hakukuwa na namna ilibidi Esther kuwabeba akina Vicky na Boss France kwa pia
kwa ujumla wao walikuwa wakikaa maeneo ya jirani ambapo Boss France aliishi
Oysterbay, naye Esther pamoja na Vicky waliishi Masaki tofauti ilikuwa ni majengo
tu. Kabla ya kuanza kuondoka Esther alimsihi Vicky aje akae eneo la mbele kwa
pembeni yake na kumuacha Boss France akae peke yake kwenye siti ya nyuma ya
gari. Boss France na Vicky walitizamana na kisha wote wawili wakatingisha
vichwa vyao kuonesha kukubaliana na ombi la Esther ambaye kwa wakati huo
alikuwa ameegemea na kuinamisha kichwa chake katika usukani wa gari. Basi zoezi
hilo lilifanyika na kisha safari ya kuelekea majumbani ikaanza.
Ukimya ulitawala kwani hakukuwa na hata mmoja aliyeweza kumsemesha mwenzake ingawa kila mmoja alikuwa na dukuduku zito ndani ya moyo wake juu ya mwingine. Esther alijitahidi kuendesha gari kwa kasi ili wawahi kufika licha ya uwepo wa foleni kubwa iliyokuwa ikiwakabili njiani. Hatimaye waliingia mtaa wa Oyster bay naye Boss France kwa kuvunja ule ukimya uliokuwa umetawala mule ndani ya gari akasema “Thank you God niliumisi sana huu mtaa hasa nyumbani kwangu” alizungumza maneno hayo ikiwa ni ishara ya kwamba walikuwa wamekaribia kufika katika jumba lake.
Pia akajifanyisha kujinyoosha huku shingo yake na macho yake yakiwa mbele kumtizama Vicky ambaye alikuwa akitabasamu tu kwani alikwisha kuona vituko vyote vya Boss France kupitia kwenye kioo kulichokuwa mbele ya upande wa juu wa ndani ya gari. Esther alimtaka Boss France kumuelekeza njia iliyokuwa ikienda moja kwa moja hadi nyumbani kwake kwani alikuwa apafahamu mbali na kufahamu tu ya kwamba Boss wake alikuwa akiishi katika mtaa huo. Naye Boss France alifanya hivyo wakati hivyo wakati huo Esther na Vicky walikuwa wakiikodolea macho mijengo mbalimbali yenye hadhi ya aina yake iliyokuwa imepangika ndani ya mtaa huo. Ilichukua dakika mbili wakawa wamefika nje ya jumba la Boss France na kisha wote wakashuka na kuinua macho mbele yao.
Looh! Lilikuwa ni jumba hasa lenye ukubwa wa
aina yake na muonekano mzuri uliowavutia na ambao ungeweza kumvutia yoyote yule
kila alitazamapo. Boss France aliwakaribisha waingie ndani wakati huo geti la
jumba lake lilikuwa likifunguliwa na Malila Mwanajogini baada ya Boss France
kubonyeza switch iliyokuwa ukutani na kufanya mlio wa alamu isikike upande wa
ndani wa jumba lake. “Karibuni sana, karibuni ndani na haka ndiko kajumba
kangu” maneno haya yalitoka kinywani mwa Boss France huku akijichekesha.
Mmh! Ilikuwa ni kauli ya kujikosha kwelikweli kwani kwa hadhi na heshima ya
jumba lile hakupaswa kutoa maneno yale. Maneno yale yalikuwa si mali kitu kwa
Esther na Vicky ambao hawakusita kuendelea kuonyesha namna ambavyo walikuwa
wamekoshwa na muonekano wa mjengo ule. “Wow! ama kweli Boss wangu unaishi
katika falme ya aina yake maana siyo kwa mjengo huu, Hongera zako” alizungumza
Esther huku akiendelea kupepesa macho yake kushoto na kulia mwa jumba lile.
Boss France alitabasamu na kuachia kicheko chepesi kisichokuwa na sauti kisha
akasema asante. Vicky aliyekaa kimya kwa muda kidogo naye alidakia kwa maneno
yake “Looh! Kwa mara ya kwanza naingia ndani ya mjengo wa Boss” Ewaah!
Mapigo ya moyo wa Boss France yalipiga shwangwe kwani alifurahia jambo lile
kimya kimya ndani ya moyo wake huku akili na hisi zake zikitoa majibu “Yes
yajayo yanafurahisha” lakini haikuwa bahati kwa Boss France kwa wakati
huo kwani hisi zile zilikatishwa na maneno ya Esther aliyedakia kwamba “Asante
sana Boss Kwa ukaribisho wako nadhani tutakuwepo hapa kwa wakati mwingine,
uzuri tushapafahamu wala usijali nitakuja sana acha kwa sasa tuwahi majumbani
mwetu” kila mmoja alionyesha kucheka kidogo na kutabasamu ingawa kauli
hiyo ya Esther yenye umimi iliacha maswali kadhaa katika kichwa na Boss France
na Vicky. Lakini kabla ya moja kwisha la pili likajitokeza kwani Esther alimsogelea
Boss France na kumpa kumbato zito lililokuwa joto la kimahaba ambalo ilikuwa ni
vigumu kuweza kuzipima nyuzi joto zake hata kwa matumizi ya kipima joto. Baada
ya hapo Esther alimshika Vicky kwa mkono mmoja huku mwingine akiubusu na
kumpungia Boss France ikiwa ni ishara na kumuaga.
“Twende
zetu shoga yangu muda umetutupa mkono” alikuwa ni Esther aliyeyasema hayo huku
akielekea ndani ya gari lake. Wote walipanda na kuelekea Masaki yalipo makazi
yao lakini Vicky alikuwa mwenye hasira na asiye na furaha kwa wakati huo juu ya
kile kilichofanywa na Esther mbele ya macho yake alijisemea moyoni mwake “ama
kweli leo umeniweza ila nitalipiza hili” ilikuwa ni tofauti sana kwa
upande wa Esther kwani yeye alionekana kuwa na furaha kana kwamba kuhisi dunia
ni yake ya peke yake na aliyempenda. Vicky alizidi kuchukia sana na kubaki na
lake la moyoni juu ya Esther.
Ilichukua
dakika kadhaa wakawa wamefika maeneo ya masaki lakini kutokana na hasira
alizokuwa nazo Vicky hakutaka hata Esther afahamu alipokuwa akiishi. “Naomba
nishushie hapo dukani kwa Mangi nadhani nitakuwa nimefika” alizungumza
vicky huku Esther akimjibu “Noo... Vicky usijali nitakufikisha hadi nje
ya jumba lako” maneno hayo yaliyokuwa ya kejeli kutoka kwa Esther
yalizidi kumkwaza sana Vicky naye hakusita kujibu “Hapana nishushe hapo
panatosha maana kuna vitu pia nahitaji kuchukua hapo dukani na kwangu siyo
mbali na hapa” Esther hakuwa na Budi kukubaliana na ombi
la Vicky lakini kabla ya kufanya hivyo alimtaka Vicky aweze kumuazima masikio
yake kwa dakika chache “ Vicky najua wewe ni mwanamke kama mimi na
isitoshe ni mwanamke mzuri sana na mwenye mvuto kwa mwanaume yoyote yule ...” kabla
ya Esther kutaka kumaliza alichokuwa amekikusudia ikiwa kama ni ujumbe kwa Vicky
alikatishwa na sauti ya Vicky aliyezungumza kama vile mtu aliyekwisha
kulitambua lengo la Esther “ Kwa hiyo Esther unataka kusema nini? Labda
uzungumze kingine nitakuelewa lakini siyo kuhusiana na Boss France” “Nashukuru kama utakuwa umeanza kulipata
picha lake hivyo ninachomaanisha ni kwamba ukae mbali na Boss France” Esther
alizungumza kwa kufoka lakini ilikuwa ni sawa na kazi bure kwani Vicky naye
alimjibu kibabe “Kikubwa ni Boss wetu sote. upo mwanadada, hivyo kila
mmoja acheze kwa muda wake alaaah! Kisha akashuka na kubamiza mlango wa
gari kwa nguvu na kufyonza kwa sauti. Hakukuwa na namna kwani walishindwa
kuelewana ikabidi Esther awashe gari na kuondoka kuelekea nyumbani kwake.
Vicky
hakufurahishwa hata kidogo na kauli za Esther kwani aliitafsiri
kama zilikuwa ni kauli za dharau na zenye kuwekeana masharti mahala pasipo
hitajika kuwa na masharti. Vicky alikuwa mwenye uchovu wa aina yake kwa siku
hiyo kwani pia alikuwa ametoka katika hali ya kuumwa ambapo alilazwa AGA
KHAN hospital ndani ya siku kadhaa. Alitembea na kuelekea nyumbani kwake
akiwa mwenye fungu zito la mawazo.
Upande
wa Boss France ambaye aliachwa katika wimbi zito la hisi zilizoambatana na
maswali kichwani mwake, alikuwa akitembea tembea kulia na kushoto mwa nyumba
yake pamoja na Malila mwanajogini ambaye alikuwa na furaha kubwa ya kuona Boss wake
amerejea nyumbani. Walipiga stori mbili tatu lakini kutokana na uchovu mwingi
aliokuwa nao Boss France alionelea kwamba wangeendelea na mazungumzo yao kwa
siku ya kesho kwani alikuwa akihisi usingizi.
Malila
mwanajogini aliuliza kwamba naweza nikakuandalia chochote kitu Boss wangu naye
akamjibu kwamba asijali kwani angeweza tu kuchukua juice kwenye friji na
kuinywa. Aliingia ndani ya jumba lake na kuelekea katika moja ya friji yake ya
kuhifadhia vinywaji na kuchukua juisi ya embe iliyokuwa katika pakti na kuingia
ndani ya chumba chake kisha akayavua mavazi aliyokuwa nayo. Alifunga taulo lake
kiunoni na kuelekea bafuni kujimwagia maji walau kuweza kupunguza kasi ya
uchovu aliokuwa umeubeba mwilini mwake. Baada ya dakika chache alitoka bafuni
na kurejea katika chumba chake kisha akabadili taulo kwa kuvaa mavazi ya
kulalia. Alijiachilia na kujitupa kitandani mwake, kitendo ambacho kilimfanya
anesenese mara kadhaa kulingana na namna ambayo kitanda chake kilivyokuwa
kimetengenezwa. “Ahooooh! Ahaaah!...” alipiga mihayo huku
akijinyoosha pale kitandani, punde kidogo aligeukia upande wa pili na kujilaza
kifudifudi, alinyoosha mkono wake na kushika simu yake ya mkononi. Mmmh!
Alighuna na kuitolea macho simu yake baada ya kukutana na missed calls tatu
kutoka kwa Sekretari wake Esther.
Alitaka
kumpigia lakini akasita kidogo kisha akawaza kwa muda “Lakini si
sekretari wangu huenda kuna jambo linalohusiana na masuala ya kikazi zaidi” akajaribu
kupiga simu lakini kwa bahati mbaya Esther aliyekuwa na kiwewe cha kukosa
usingizi kwa kuwaza sana juu ya kumbato zito alilompatia Boss France na
kuegemea kifuani mwake kwa muda kidogo kiasi cha kuzidi kumpa uchizi katika
fahamu zake.
Kutokana
na wenge alilokuwa nalo kwa wakati huo alijikuta akibonyesha sehemu ya kukatia
simu badala ya kupokea “Oooh! Mungu wangu, sasa hichi ni nini nimekifanya
tena? Alibaki akijiuliza huku Boss France akipata taarifa ya kwamba “Namba
unayoipigia inatumika kwa sasa tafadhali jaribu tena badae” Boss France aliamua kumuandika Vicky ujumbe wa
meseji uliosomeka “Hello! Natambua ya kwamba utakuwa umechoka sana lakini
pia naomba unisamehe kwa yote yaliyoweza kutokea kwani huikuwa ni dhamira wala
kusudio langu hivyo usinichukie wala kunifikiria tofauti, uwe na usiku mwema na
ulio tulivu” ujumbe ule ulionyesha kufika lakini hapakuwa na majibu
yoyote kutoka kwa Vicky baada ya Boss France kusubiri kwa dakika kadhaa.
Aliamua kuitelekeza simu yake na kutojali juu ya kupiga tena simu kwa Esther.
Wakati
huo aliikumbuka juice yake ya embe aliyoingia nayo chumbani kisha akaamka pale
kitandani mwake na kwenda kuifungua kisha akajipigia pafu kadhaa na kujiegemeza
tena kitandani mwake. Punde si punde usingizi mzito ukamzoa, Ilikuwa imekwisha
kutimu majira ya saa tatu kamili usiku.
Baada
ya Esther kuona kimya kimetawala na hapakuwa na dalili yoyote ya kupigiwa tena simu na Boss France ilimlazimu
amuandikie ujumbe kwa njia ya meseji “Bila shaka utakuwa umechoka na
pengine umekwisha kulala lakini nilitaka kukuarifu kwamba kila kitu kiko vizuri
ofisini na kama kesho utakuwa vizuri unaweza ukaendesha kikao na mimi nipo
kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa, nakutakia usiku mwema Boss mwenye jumba
lake” Looh..! Ama kweli kila shetani na mbuyu wake. Na waswahili walishasema
Unachokisusa wewe cha mnyima usingizi mwenzio... Esther aliusoma mara
tatu tatu ule ujumbe wake aliouandika kabla ya kuutuma kwa Boss France kitendo
ambacho kilimpotezea si chini ya dakika tano na baada ya kujiridhisha ya kwamba
uko sawa aliamua kuutuma.
Hivyo
ilimpasa kujipumzisha kulingana na majukumu mazito aliyoweza kuhangaika nayo siku
hiyo. Alichukua moja wa mito yake na kuukumbatia kisha akavuta blanketi lake na
kuuchapa usingizi. Usiku huo ulikuwa wa aina tofauti kati ya watatu hao hasa
kwa Boss France pamoja na Vicky kwani Boss France aliyejihakikishia usingizi
wake mapema ya saa tatu za usiku aliweza kushtuka mnamo majira ya saa tisa za
usiku kulingana na ndoto iliyomdanganya kwamba alikuwa amelala pamoja na Vicky
kitu ambacho hakikuwa na uhalisia wowote. Alishtuka na kujikuta akiita “Vicky...
Vicky... Vicky...” akatizama huku na huko hakuweza kuona nyongeza ya
mtu yoyote tofauti na yeye jambo ambalo lilikuwa ni gumu kwake kuweza
kuliamini.
Alisimama
na kutembea kwenye kona zote za chumba chake lakini hakuweza kubaini lolote
lile na mwishowe alitikisa kichwa chake na kupikicha macho kwa vidole vyake
pengine labda alihisi kama bado hayamtoshi kuona bila ya kufanya hivyo lakini
bado ilikuwa ni bilabila. Alisogea mpaka kwenye dirisha kisha akavuta pazia
pembeni na kutizama nje aliona jiji likiwa limemeta kwa mataa na baada ya kuyaridhisha
macho yake kwa uzuri wa jiji alilazimika kurudi kitandani mwake akavuta shuka
na kuendelea kujipongeza kwa usingizi.
Esther
naye aliyekuwa amejawa na mawenge ilikuwa ni ngumu sana kwake kwa siku hiyo
kupita bila ya kukumbwa na njozi kwani hisia zilizidi uwezo wa fikra zake kwa
siku hiyo. Yalikuwa ni majira takribani yaleyale ambapo naye alikitwa na njozi
iliyokuwa haielezeki kwa mtazamo wa kawaida. Looh! Jambo lilikuwa jambo kweli. Wakati
akiwa katika fikra alisikia mlango wa jikoni ukijibamiza kwa nguvu na kishindo kizito
kusikika kisha kukawa kimya kitendo kilichomfanya Esther kuingiwa na wasiwasi
pasipo kujua kulikuwa na nini.
MWISHO
ENDELEA
KUFUATILIA MIENDELEZO YA TAMTHILIYA HII PENDWA.
Mwandishi: Sebastian Seba
Mawasiliano: 0758162527
0 Comments