Facebook

PESA ZA SHEMEJI SEHEMU YA KUMI NA TATU (13)

SEHEMU YA KUMI NA TATU

Ilikuwa ni saprize nzito naya aina yake ndani ukumbi wa kikao na kila mmoja asiweze kupata picha varanguti ambalo lingeweza kutokea hata Boss france mwenyewe alihisi ni kama ndoto.

Samahani Vicky naomba utoke nje ya ukumbi wa kikao. Boss france alimtaka vicky kusubiri nje mpaka  kikao kitakapokwisha kwa maana isingeweza kuleta picha nzuri kwa wafanyakazi wenzie, ilihali alikuwa akitambua taratibu zote na uzito wa kikao kile.

Vicky hakutaka kujibu chochote kile kwani ilimbidi kufanya kile alichoamuriwa na Boss wake. Alitoka nje ya ukumbi wa kikao ingawa nafsi yake haikuridhia kwa kuhisi kama kitendo kile kilichofanywa na Boss wake kilikuwa nicha kumuaibisha kwa haiba iliyokuwepo pale ndani.

Sidhani kama ni dhamira yake nahisi amefanya vile tu kwa sababu ya uoga wa awara wake. Vicky alijisemea huku mishipa ya ghadhba ikimpanda taratibu

Wakati huo ndani ya ukumbi wa kikao kilichokuwa kikielekea tamati. Kasheshe zilitaka kuibuka baada ya Esther kujikuta akichekelea kile kilichomkuta Vicky. Kitendo hicho kilichoonekana sicho cha kiungwana kilimfanya Boss france kuanza kupaniki na kuuliza kwa hasira.

Kitu gani kilichokuchekesha Esther?  Mapigo ya Esther yalishtuka kidogo na fahamu zake kuweka umakini. Mmmh! Hapana Boss mimi sijacheka ila nimefurahi kwa kuona umefanya maamuzi ya Busara kwa kutambua taratibu za kikao chetu.

Esther alitoa jawabu zuri lenye uwezo wa kuzichanga karata kwa kutumia macho, naye Boss france alijikuta akiwa mpole kama mboga iliyokosa matumizi ndani ya mgahawa.

Kikao kilifikia tamati na Boss france aliwaomba wafanyakazi wote kurejea katika ofisi zao na kuendelea na majukumu. Wote walianza kutawanyika na kuelekea katika maeneo yao ya kazi lakini wazee wa mbaga walikuwa wa mwisho kutoka pale ukumbini kwa kuhisi kwamba pengine kungeweza kuwa na kikao baada ya kikao.

Nilitegemea kuona marudio ya lile pambano la vitasa kati ya Twaha kiduku na dullah mbabe hahahaa... Bwana jeshi alilianzisha huku kicheko kikimpalia

Msodoki: Mimi nilijiandaa kuwa refa ili niweze kufaidi vingi kwa ukaribu. Wote walicheka huku Bwana kichuya akiwasihi wenzie kuelekea ofisini mwao kwani siku hiyo alianza kuonekana mbaya baada ya uwanja kuonekana umeinama.

Baada ya Boss France kutoka nje ya ukumbi wa kikao akakutana na Vicky akiwa amesimama kwa masikitiko nje ya mlanago. Alimvuta mkuku mkuu hadi ofisini kwake na bila ya kujali kuwa Vicky alikuwa bado hajapona vizuri.

Niache tafadhali hakuna mbuzi wala punda hapa wa kumpeleka peleka hovyo kama unavyotaka. Vicky aliongea kwa hasira na kwa uchungu huku akiendelea kuvurutwa mpaka ndani ya ofisi ya Boss france pasipo kuelewa Boss France alikuwa na lengo gani.

Naomba niache tafadhali, achana na mimi. Mbwa wewe usiyekuwa na huruma wa haya. Looh! Kauli hizo za Vicky zilizojilimbika kashfa na dhihaka kwa Boss wake hazikuweza kufua dafu kwani alijikuta akiambulia kibao kizito kilichosikika kama gari lililokumbwa na pancha.

Paaah! Mwanamke mshenzi sana wewe, usitake kuniharibia siku yangu wewe ni wakunitukana mimi kwa hadhi ipi uliyonayo. Boss france alijikuta akifanya maamuzi ambayo hakuwahi kuyataraji katika maisha yake pengine jambo hilo lingemjaza wimbi la majuto hapo baadae.

Wakati hayo yakiendelea ndani ya ya ofisi ya Boss france. Bwana jeshi, Msodoki na Bwana kichuya nao walikuwa wakija katika eneo la ofisi ya Boss france ili kutaka kujua nini kilichoweza kutokea baada ya kusikia kibao kile na sauti za malumbano baina ya Boss France na Vicky.

Walifika nje ya ofisi ya Boss ya Boss France na kusikia sauti ya Vicky akiwa anajlia, nao waliendelea kubishana kwamba ni nani kati yao angeweza kujilipua kugonga mlango ili waingine ndani.

Eeeeh! Esther naye huyo anakuja nadhani atakuwa amesikia lile bomu lililokuwa limelipuka humo ndani. Bwana jeshi alizungumza maneno yake yaliyokuwa yamejaa mizaha kama ilivyokuwa kawaida yake lakini Msodoki alimsihi kuacha masihara na kungalia namna ya kufanya kilichowavuta mpaka pale.

Mimi nafikiri tumsubiri Esther ili tuingie naye maana naona kama  anakuja uelekeo huu. Yalikuwa ni maneno yenye busara na hekima ndani yake ya Msodoki. Wote walikubaliana na mawazo hayo na kuendelea kusubiri.

Jamani kuna nini kimetokea ndani ya ofisi ya Boss? eti mbona kama sielewi elewi au Vicky kalizua tena. Esther aliwasili eneo walipokuwa wakina Bwana jeshi na wenzake nakuuliza maswali ambayo hayakuweza kupata majibu yoyote.

Alishtuka na kujiziba mdomo wake mara moja baada ya kusikia sauti ya kilio cha Vicky ndani ya ofisi ya Boss france. Papo hapo akaanza kugonga mlango na kuingia ndani pasipo kuruhusiwa. Nalo kundi la wanambaga lilijiunga na kuwa sehemu ya msafara wa Esther kisha wakaingia ndani

Vicky, Boss jamani kuna nini mbona hivi? Kila mmoja aliuliza swali ambalo halikuweza kujibiwa. Kitendo cha Esther kumkuta Vicky akiwa amekaa chini, kashika tama na kujiinamia huku machozi yakimtiririka kwa maumivu, kilimfanya aingiwe na moyo wa huruma kiasi cha yeye kuhisi maumivu aliyoyapata Vicky licha ya tofauti na chuki walizokuwa nazo.

Wakati huo Boss france alikuwa amekaa kwenye kiti chake na kuinamia meza kiasi ambacho kiliweza kuufanya uso wake kujificha.  Esther aliendelea kumbembeleza Vicky  na kumtaka asiendelee kulia kwani jambo hilo lilimpelekea Esther naye kulengwa lengwa na machozi.

Bwana kichuya alimsogelea Esther na kumnong’oneza sikioni mwake kwamba angependelea kumuona akifanya mazungumzo na Boss France pengine ingeweza kuwa rahisi kujua namna ya kukabili madhila yaliyoweza kujitokeza na kazi ya kumbembeleza Esther ingewafaa sana wao.

Sawa nimekuelewa vizuri nadhani ni jambo zuri na lenye busara na ukizingatia kesho tuna safari ya kwenda Zanzibar hivyo tunapaswa kulimaliza hili mapema ili kila mmoja aweze kuwa na amani. Esther alikubaliana na maneno ya bwana kichuya wakati huo bwana jeshi hakuwa mbali na Vicky.

Esther alisogea karibu na Boss france aliyekuwa ameinamisha kichwa chake juu ya meza na kuwa kimya kwa wakati wote tangu ujio wa akina Esther ndani ya ofisi yake. Boss, Boss, Boss... Esther alimuita Boss France mara tatu tatu huku mkono wake wa kulia ukilazimika kupapasa kichwa cha Boss france. Aliendelea kumsihi Boss wake kwamba angejaribu kuzungumza ili waweze kuyaweka mambo sawa huku akimkumbusha juu ya safari yao ya siku ya kesho kwenda Zanzibar.

Mmh! Amenikosea sana ila namuachia tu Mungu. Boss france alianza kufunguka kwa sauti ya chini chini na kuzidi kutoa manung’uniko yake juu ya Vicky kwamba ndiye aliyeweza kusababisha yote hayo.

Mara ghafla Vicky naye alikurupuka kwa hasira baada ya kusikia Boss france akimtupia lawama zote juu ya kile kilichoweza kutokea. Yaani tena bora ukae kimya kabisa, kati ya mimi na wewe nani aliyemkosea mwenzake, unawezaje kunipiga kibao kizito kama kile ilihali unafahamu yakuwa mimi bado ni mgonjwa, huo ni utu kweli? Yaan... ooh! Vicky aliongea kwa uchungu huku akizidi kumwaga machozi ya hasira

Yalaaah! Bwana jeshi aliamua kudakia baada ya kusikia maneno yale kutoka kwa Vicky kwani yalimgusa sana katika ubongo wake. Ndio maana tulisikia kitu kizito kama vile mlipuko wa bomu, Daah! Kumbe kilikuwa ni kibao aseee! Hii haijakaa sawa kabisa ama mnasemaje wenzangu? Bwana jeshi alitoa yake ya moyoni ingawa alijificha katikati ya kivuli cha wenzie na kisimtoshe kumsitiri. Wote walikubaliana na kauli ya Bwana jeshi lakini hakuna hata mmoja aliyeweza kutoa sauti yake nje bali walitikisa tu vichwa vyao kwa sababu Boss France hakuweza kuwaona kwa wakati huo. Mara ghafla Boss france akakurupuka na kusimama kama upepo wa kisulisuli. Tafadhali Bwana jeshi naomba ukae kimya tena ikibidi utoke ofisini kwangu. ilikuwa ni wazi kwamba Boss france hakupendezwa na kauli za Bwana jeshi, kauli hizo zilipenya vilivyo katika ufahamu wa Boss france kufanya kazi dizaini ya kumtoa mlevi ndotoni.

Ama kweli “mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchunguBwana jeshi hakuwa na budi kutoka nje lakini baada ya muda mfupi wote waliokuwepo ndani walau walifikia muafaka mzuri na kila mmoja kuanza kutawanyika. Vicky alipewa ruhusa ya kwenda kupumzika nyumbani kwake na mara moja aliondoka hapo bila ya kusema chochote baada ya ruhusa aliyopewa na Boss France.

Ikiwa ni mda mchache baada ya Vicky na wengine kuondoka ndani ya ofisi ya Boss France. Kilichoendelea kuusumbua ubongo wa Boss France kilikuwa ni majuto ni mjukuu kwani aliwaza na kuwazua sana juu ya kili kichoweza kutoea. Aaah! Mbona kama nimeikosea sana nafsi yangu, imekuaje leo nimefikia maamuzi haya juu ya Vicky. Mwanamke ambaye nilishaanza hata kumpenda, leo imekuwa hivi? Hapana, hapana kabisa nahisi kuna mtu kaniloga.

Boss france aligonga meza na kushusha pumzi zake huku akijutia sana juu ya kilichotokea kati yake na Vicky. Aliona hakikuwa kitendo cha busara cha yeye kufanya vile, alijihisi kwamba yeye ndiye aliyekuwa na makosa na hasira zake ndo zilizoweza kumponza.

Ofisini kwake hapakuweza kukalika na maana kila jukumu la kiofisi alilojaribu kulifanya lilikuwa gumu kwako siku hiyo. Aliwaza nini angeweza kufanya Ooh! Nafikiri nami ningeenda kujipumzisha tu nyumbani na kufanya maandalizi ya safari ya kesho.  Alitoka ofisini mwake na kuelekea kwenye ofisi ya sekretari wake Esther ili aweze kumuaga. Lakini Esther naye alikuwa akija katika ofisi ya Boss France.

Yes Esther, ulikuwa ukija katika ofisi yangu? Esther aliitikia abee Boss

Boss france: Vipi kuna jambo jipya la kikazi? maana naona kama vile kichwa changu hakiko sawa.

Esther: Usijali, nilitaka tu nikushauri kwamba ni vema ungeenda kupumzika na kujiandaa na safari ya kesho.

Boss France: Ohooh! Hata na hivyo nilikuwa nikija kukuaga

Esther: Basi sawa, alafu ticket zetu zimeshakuja, tutasafiri na usafiri wa majini kwa Boti ya Azam Marine inayoondoka saa sita.

Boss France: Sawa kabisa, usafiri wa majini utafaa zaidi walau hata kuweza kurefresh macho kidogo. Kisha akacheka hahahaa. Boss france alijitahidi kuongea kama vile alikuwa ameshasahau mambo yote yaliyoweza kutokea masaa machache hapo nyuma kwani aliongea akiwa na uso uliojaa furaha na tabasamu.

Esther: Basi ngoja nikuletee ticket yako

Boss France: Hahahaaa Esther, hapana usisumbuke kwenda ofisini. Safari yetu ni moja hivyo kaa nazo tu hamna tatizo

Esther: Sawa Boss nimekuelewa, uwe na muda mwema. Esther mrembo mwenye madaha hakusita kumgusa kidogo bega Boss wake wakati akimuaga na akaondoka kuelekea ofisini kwake.

Boss france alipiga hatua moja na kugeuka tena upande aliokuwa akielekea Esther na kuongeza neno. Esther Aaamm hakikisha nawe leo unaondoka mapema ili kujiandaa na safari.  Sawa Boss usijali. Esther alisimama kidogo akajibu kisha akaendelea na mwendo kuelekea ofisini mwake.

Boss france aliondoka na kuanza safari ya kuelekea nyumbani kwake Oyster bay Lakini kiuhalisia akili yake haikuwa sawa kabisa siku hiyo toka alipovurugana na vicky. Ilimbidi asogeze gari pembeni ya barabara kisha akasimama. Alifanya hivyo kwa lengo la kuwasiliana na Vicky ili amuombe msamaha kwa kile alichokifanya kwa sababu moyo wake haukuwa na amani kabisa.

Aliamua kumpigia simu Vicky lakini simu yake iliita tu pasipo kupokelewa. Akajaribu tena mara ya pili naya tatu lakini mambo hayakuweza kubadilika kwani simu haikupokelewa. Alijishika tamaa na kufikiri kidogo kisha alipata wazo kwamba ingefaa kumuandikia ujumbe wa simu

Hello! Vicky, kiukweli nimejaribu kukaa kimya lakini nimeshindwa kotokana na kile nilichokufanyia, Moyo wangu hauna amani kabisa ya kufanya chochote kile kwani nakiri na kujutia kosa langu. Ila usisahau yakuwa mimi ni binadamu na nimeumbiwa udhaifu hivyo naomba unisamehe sana Vicky. Wakati huo Vicky hakuwa mbali na simu yake kwani alishuhudia yote tangu Boss France alipokuwa akimpigia. Lakini baada ya SMS kuingia katika simu yake aliona siyo mbaya kujaribu kuisoma labda pengine ingeweza kumshawishi.

Haaaaaa! Vicky alishusha pumzi na kunywa glass moja ya maji. Ilikuwa ni wazi kuwa ujumbe ule wa simu kutoka kwa Boss France uliweza kumshawishi. Akili yake ilikubali kumsamehe Boss France ingawa mwili wake haukutaka kujishughulisha kujibu ujumbe ule.

Boss france alizidi kujisikia vibaya baada ya kuona kimya lakini taswira ya rafiki yake Meneja Tinno ilimjia machoni pake na kukumbuka yakuwa wote walipaswa kusafiri siku ya kesho kuelekea zanzibar. Mara moja alinyanyua simu yake na kumpigia

Tiiiiiiii.... tiiiiiii.... tiiiiii..... simu iliita kwa muda kidogo kisha ikapokelewa

Meneja Tinno: Naam Boss wa maboss

Boss France: Yes

Meneja Tinno: Vipi rafiki yangu, mbona kama kinyonge tena?

Boss France: Aaah! Nahisi kama siko sawa vile, then kuna jambo natamani tuweze kulizungumza siku ya leo tukiwa ana kwa ana.

Meneja Tinno: Sawa haina shida, na mimi najiandaa hapa kutoka kazini. Hivyo sijajua tutakutaniana wapi vile?

Boss France: oooh! Nadhani ingekuwa vema kama ungepanga wewe Boss

Meneja Tinno: Eeeeh! Mmmh! Vipi pale HAVOC NIGHT SPOT CLUB naona kama kumekaa vizuri kwa hadhi yetu

Boss France: Mmmh! Pale sawaa lakiniii... sidhani kama patatufaa zaidi, maana kuna tatizo lilishawahi kutokea pale siku za nyuma kidogo. Hivyo tungepata sehemu nyingine tofauti na hiyo.

Meneja Tinno: Basi tukutane New maisha club muda wa saa tatu.

Boss France: Hapo sawa, bila shaka tutaendelea kuwasiliana

Meneja Tinno: Ok, ok

Boss France na meneja Tinno walifikia makubaliano kwamba ni wapi wangeweza kukutana hapo baadae kisha Boss France aliendesha gari kuelekea nyumbani kwake.

Ilikuwa imeshatimu majira ya saa tisa alasiri na kenda na alitumia mda usiopungua nusu saa hadi kufika nyumbani kwake.

Piiii... piiii...piiii... sauti ya honi ililia ili geti liweze kufunguliwa ikiwa ishara tosha kwamba Boss France alikuwa ameshafika nyumbani kwake

Aaaaah... Boss mwenyenye, hahahaa karibu sana. Malila mwanajogini alipokea begi la Boss wake ambaye alikuwa akiishi naye kama ndugu na kama sehemu ya familia yake maana Boss france hakuwa na mke wala mtoto hata mmoja licha ya kuishi katika mjengo mkubwa nawa kifahari.

Boss France: Ahsante, bila shaka utakuwa umeshinda salama.

Malila mwanajogini: Ndiyo mkuu, vipi majukumu?

Boss France: aaah! Kheri kabisa, sasa malila mimi naingia ndani ila badae nitatoka mida ya saa mbili na nusu hivi

Malila mwanajogini: Sawa Boss, mimi ni nani mpaka nikupinge

Boss France: Hahahaaa, acha habari zako. Then angalia ndani ya begi kuna zawadi yako huko

Malila mwanajogini: Daah! Asante sana Boss wangu, Mwenyezi Mungu akuzidishie kila uchao.

Boss france aliitikia haya huku akielekea ndani. Alisogea karibu na friji akavuta kinywaji cha juisi ya embe na kukimimina mdomoni haraka haraka.

Yani leo sijala kabisa alafu sihisi hata njaa, basi nitakuwa nimeshiba. Alijiuliza swali na kujijibu kisha akaelekea chumbani mwake. Alijiangusha kitandani bila hata ya kuvua viatu na kama mzaha vile wimbi zito la usingizi likamchukua.

Boss france alilala fofofo kwa masaa kadhaa kutokana na uchovu aliokuwa umemjaa siku hiyo.

Muda ulisogea na kufika mpaka saa mbili na nusu usiku lakini Boss france alikuwa bado yupo usingizini.

Wakati huo malila mwanajogini alikuwa sebuleni akitizama taarifa ya habari.  Heeheh! Mbona kama muda umeenda lakini sioni dalili yoyote ya Boss kutoka ndani. Malila mwanajogini alijihoji baada ya kuona kimya kirefu na muda ukizidi kwenda. Ikabidi asogee karibu na chumba cha Boss France na kugonga mlango.

Ngo, ngo, ngo,... ngo, ngo, ngo.

Boss France alishtuka kutoka usingizini huku akilambalamba midomo yake na alipotizama saa yake ya ukutani ilikuwa imeshatimia saa mbili na dakika arobaini. Na hapo usingizi wote ulimuisha akadogea hadi mlangoni.

Aaaaah! Ooooh! Alijinyoosha na kupiga mihayo mingi kisha akafungua mlango

Boss France: Alaaah! Vp malila

Malila mwanajogini: Safi Boss, muda umekwenda uliniambia utatoka au umeghairi.?

Boss France: Hapana, nilikuwa nimesinzia kidogo ila asante kwa kunikumbusha.

Malila mwanajogini: Sawa mkuu

Malila mwanajogini alirudi sebuleni kuendelea na taarifa ya habari naye Boss France alivua nguo zake za kazini, akafunga taulo, akachukua mswaki wake na kuingia bafuni mara moja. Aliswaki na kuoga bila ya kupoteza nyakati akarudi chumbani mwake na hapo ilikuwa imekwisha timu saa tatu kamili

Ahahaa! Asee... Niko nje ya mda kweli.. na ndugu yangu huwa yuko vizuri sana kwenye kuzingatia muda ilihali mimi ndiye niliyemualika.

Alivaa haraka haraka mavazi yake ya ujana na kutupia bareti kichwani bila ya kusahau kujinyunyuzia unyunyu wa Kifaransa kisha akabeba simu yake na kutimka nje.

Malila njoo ufunge geti ndungu yangu usiku huu. Boss france alinyooka mpaka getini, akalifungua na kurudi kwenye gari kisha akatimka mara moja kuelekea New maisha club walipopanga kukutana na Boss france. Wakati huo naye Meneja Tinno alikuwa akimpigia simu Boss france ambaye hakusita kuipokea.

Boss France: Yes Boss, nipo njiani nimekaribia kufika.

Meneja Tinno: Ohooh! Sawa nimekupigia mda sana lakini simu iliishia kuita tu.

Boss France: Daah! Samahani sana, yaani huwezi amini tangu nimefika nyumbani hapa ndo ninashika simu kwa maana nilikuwa nimelala

Meneja Tinno: Basi sawa usijali. Mimi nimeshafika hapa nakusubiri

Boss France: Ok, chapu mara moja nitakuwa hapo

Meneja Tinno: Sawa.

Boss France alikanyaga mafuta haswa ili kuwahi ndani ya viwanja vya New maisha club. Ilimgharimu kiasi cha muda wa dakika 20 tu kuweza kufika hapo.

Alishuka kwenye gari, akaweka loki na kuelekea ndani. Nje ya mlango wa kuingia ndani ya New maisha club alikutana na mabamnsa waliokuwa wamesimaama kama mibuyu ya kale ya Mpwapwa. Lakini kwa muonekano wake wa kipedeshee hakuweza kupata kizuizi chotete kwani alipitiliza moja kwa moja hadi ndani.

Palikuwa pameanza kuchangamka ndani ya New maisha club kwa kuchagizwa na midundo mikali pamoja na taa zilizowakawaka kama vile vimulimuli. Alitizama kushoto na kulia, juu na chini nakwa bahati nzuri alibahatika kumuona Meneja tinno akiwa upande wa juu wa VIP.

Alitembea mpaka eneo la kaunta alilokuwa amekaa Meneja Tinno ambaye alining’iniza miguu yake kwenye kiti cha kuzunguka huku akipata kinywaji baridi.

Boss France alisogea karibu kabisa na kumshika begi Meneja Tinno.

Aaah! Boss la maboss, karibu sana. Karibu kiti ndugu yangu. Meneja Tinno alimkaribisha Boss France kwa mbwembwe kweli kweli na wakati huo kinywaji nacho kilianza kumpanda kichwani kwani alikuwa amefika mapema kabla ya Boss france.

Boss france alimshukuru Meneja Tinno lakini alimuomba wangehamia kwenye meza, ili wawili hao waweze kujadili mambo yao.

Basi sawa tusogee meza ile iliyokaribu na ukuta. Meneja Tinno aliendelea kwa kusema

Waiter naomba nisogezee hivyo vinywaji vyangu huku. Meneja Tinno alikuwa na dalili za kuvaa miwani na hata yeye mwenyewe alianza kujishtukia. Ikabidi ayagubike mdomoni kwa pupa maji yake makubwa aliyokuwa ameyashika mkononi.

Wakati huo waiter alikuwa akileta vinywaji naye Boss Tinno alikuwa akimkata jicho vilivyo.

Karibuni sana Maboss. Waiter alimsogelea Boss france na kumuuliza. Nikuletee kinywaji gani Boss?

Ahahaah! Niletee Maji makubwa tu kwa sasa.

Looh! Meneja Tinno alidakia. Hapana, hapana naomba umletee Hennesy huyu ni mtu mzito sana hapa mjini hahahaa...

Boss france naye aliishia kucheka na kusema Sawa lete kashasema Boss.  Ulikuwa ni urafiki mzuri sana kati yao kwani walikuwa ni watu walioelewana sana.

Pasipo kupoteza muda Boss france ilibidi aanze kuweka mezani agenda iliyoweza kuwakutanisha.

Ndugu yangu utanisamehe sana, maana siku ya leo sijachangamka kiivyo kwa sababu kuna mambo hayajaenda sawa kabisa. Naye Meneja Tinno alidakia tena Mmh! Embu ngoja ni mambo gani tena hayo? Maana kama ni pesa unazo za kutosha wala sina shaka katika hilo, Mmmh! Umefiwa labda. Hapana hapana sidhani au ni mambo ya mahusiano nini ndugu yangu mapenzi mahabuba,habuba huko?

Boss france alicheka. Hahaaa dah! Hapana ndugu yangu. Umenilimbikizia mambo mengi sana. Hayo yote siyo ila jambo lenyewe liko hivi.

Boss france hakuwa na budi kuanza kumsimulia Boss france madhila yote yaliyoweza kumkumba siku hiyo ofisini kwake.

Wakati huo waiter naye alikuwa akileta vinywaji vya Boss france. Aliviweka mezani na kumkaribisha Boss france huku akitabasamu.

Looh! Nguo yake fupi iliyaachia mapaja yake yote nje na kuanza kumchanganya Meneja Tinno aliyeanza kuchangamka.

Hivi Mrembo uliniambia unaitwa nani vile? Meneja Tinno aliuliza

Naitwa Fetty.. aaam.. Featty Mtakuja Boss. Mrembo yule alimjibu Meneja Tinno

Aaah! Sawa Fetty, basi chukua kiasi hiki nawewe upate kinywaji mrembo. Meneja Tinno alitoa wallet yake na kuvuta kiasi cha Elfu hamsini kisha akampatia Fetty

Eeeh! Wow! Asante sana boss

Meneja Tinno akaendelea. Basi sawa nitakuona badae, kuna mambo naweka sawa hapa na ndugu yangu.. na fetty mtakuja aliitikia sawa Boss. Kisha akaelekea kaunta.

Mrembo fetty aliembea kwa madaha sana naye Meneja Tinno aliongezea neno juu ya fetty

Aseee! Kweli wewe ndo fetty mtakuja na tutakuja tu mamaa siyo kwa mshepu huo, cheki na mwendo wake alaaah! Hahahaa

Alipomaliza ya Fetty akamgeukia Boss france na kumwambia. Ndugu yangu usijali tuko pamoja, nadhani hakijaharibika kitu? Naye Boss France alimjibu ni sawa kabisa naona tupo pamoja kisha akacheka na wakaendelea na mazungumzo yao.

Meneja Tinno: Ndugu yangu usiogope, wala usiwe na shaka kabisa kwa yote yaliyokukuta sababu ni mambo ya kawaida sana kwa sisi binadamu.

Boss France: Ni kweli kabisa ndugu yangu nimekuelewa.

Meneja Tinno: Sasa hivi wewe waza zaidi juu ya kikao chetu na safari yetu ya hapo kesho.

Boss France: Sawa kabisa, alafu vipi kuhusiana na yule mrembo Zeyna?

Meneja Tinno: Yule yupo na usijali na tutakuwa naye kwenye kikao Zanzibar.

Boss France: Sawa kabisa hapo umenena

Meneja Tinno: Yule ni sawa na kuku wako, sasa manati yanini, embu tuendelee kupata vitu

Waiter tuongezee vinywaji. Maneno na ushauri wa Meneja Tinno ulimpa nguvu sana Boss France na kusahau yote kwa wakati huo na zoezi kubwa likawa ni mwendo wa kunywa tu.

Walikunywa kiasi kingi cha pombe za wine na hatimaye Boss France ndiye aliyekuja kuibuka bingwa kwenye dizaini hiyo ya shindano la kunywa. Macho yake yalianza kuona mawenge, mawenge na kila aliyepita au kumuona mbele yake alihisi ni mrembo.

Baada ya muda kidogo alikurupuka na kusema. Nakuona mrembo Zeyna.

Meneja Tinno alishtuka na kugeuka nyuma akifikiri yakwamba Boss France alimuona Zeyna lakini hapakuwa na Zeyna wala picha ya Zeyna.

Meneja Tinno: Zeyna yuko wapi?

Boss France: Mbona nimemuona hapa muda huu au ilikuwa ni wewe.

Meneja Tinno: Hahahaa ushalewa wewe, kilichobaki ni kuondoka tu hapa.

Meneja Tinno alisimama na kuwaza namna ya kuondoka na Boss france kutokana na hali kunywa kupitiliza kwanj ilikuwa ni ngumu kumuacha Boss France aondoke peke yake.

Wakati hakifikiri hilo akili yake kwa upande mwingine ilifikiri kuhusu Fetty na akose la kufanya. Aliingiza mkono mfukoni ili kutoa funguo yake ya gari lakini hakuweza kuiona. Alishtuka na kuendelea kujisachi kila upande wala hakuweza kuiona akabakia kushangaa huku akiwaza ni wapi alipoiweka.

                                    ***MWISHO***

"ENDELEA KUFUATILIA MIENDELEZO YA TAMTHILIYA YA PESA ZA SHEMEJI KILA SIKU YA JUMAMOSI PIA USISAHAU KUTIA COMMENTS ZAKO HAPO CHINI"

NCHI YETU, TAMTHILIYA YETU, FURAHA YETU. PESA ZA SHEMEJI ON AIR

“KAMA ELIMU YETU ISIPOTUOKOA, BASI VIPAJI VYETU VITUOKOE”

EEH! MUNGU BABA TUSAIDIE.

 

MWANDISHI: SEBASTIAN S MASABHA


 

 

 

 

 

 

 

Post a Comment

0 Comments