Facebook

PESA ZA SHEMEJI ( SEHEMU YA KUMI NA MBILI 12)


Sehemu ya 12

Esther alitawaliwa na uoga lakini usingizi nao ulimzidi kimo na hatimaye alijikuta akilala pasipo kutegemea. Upande wa vicky hapakuwa na shauku yoyote kwani toka alipovuta blanketi lake aliupiga mwingi mpaka palipokucha.

Boss france aliyekuwa amelala fofofo alishtuliwa na ujumbe wa simu kutoka kwa Esther uliosomeka Habari za asubuhi Boss umeamkaje? Alijinyoosha kidogo na kupiga mihayo kisha akalazimika kujibu ujumbe ule. “Nimeamka salama, leo nitakuwa kazini kwa ajili ya kikao”  baada ya hapo alitazama saa yake ya ukutani na kugundua kwamba ulikuwa ni muda wake sahihi wa kuanza kujiandaa kuelekea kazini.  

Alifanya maandalizi ya muda mfupi na kuhakikisha kwamba amependeza kama ilivyokuwa kawaida yake. Alikamatia begi lake la mkononi nakuelekea nje akaagana na mlinzi wa nyumba kisha akapanda gari na kuelekea kazini.

Wakati Boss france alipokuwa katika maandalizi yake ya kuelekea kazini naye Esther vilevile alikuwa katika maandalizi kwa wakati huo. Na kama ilivyokuwa kawaida kwa mabinti wa kisasa Esther naye alikuwa ni mmoja ya wanawake ambao walikuwa wakienda na wakati kwani suala hili lilijidhihirisha kuanzia kwenye muonekano wake wa ndani na wa nje. 

Chumba cha mavazi cha Esther kilikuwa na muonekano wa kuvutia sana kwani mavazi yake ya nguo, viatu n.k yalipangwa katika makabati ya kisasa yaliyoweza kuonekana dizaini ya yale yaliyopo kwenye maduka ya nguo ya Mlimani City.  Meza yake ya kuvalia (Dressing table) ilikuwa pambe kwelikweli iliyojaa vikorombwezo kibao na vyenye thamani Kwani ilikuwa imesheheni vitu kama Losheni, mafuta ya nywele, lipstick, lipshine, poda, pafyumu n.k.. kiasi cha kuweza kubadili uso wa tumbili na kuonekana wa mwanadamu. 

Esther mara baada ya kutoka kuoga alisogea katika kabati lake la nguo, akalifungua kisha akapepesa macho yake kulia na kushoto kutizama kwamba ni nguo gani ingemfana zaidi kuivalia siku hiyo ya kikao. Alijaribu kuvaa seti ya nguo ya kwanza, ya pili na ya tatu vilevile na kuhisi kwamba bado hazikumpendeza kwa kadri ya matamanio yake.  Alifikiri kidogo huku kidole chake cha ada kikiwa mdomoni na haikupita hata dakika moja akawa amepata jibu ya kwamba ni vazi gani lingempendeza zaidi kwa kulivalia siku hiyo.  Alitabasamu na kunyoosha mkono kabatini akatoa sketi yake nyeusi, blauzi nyeupe na koti la suti la pinki liĺiloonekana kuwa na fasheni ya kikorea alikadhalika mguuni mwake alipendelea kuvaa kiatu cheusi ambacho kilikuwa na kisigino kirefu na chembamba. 

Looh! Kutokana na mwonekano wake wa kuwa mzuri na mrembo kupitiliza mavazi hayo yalionekana yangeweza kumkaa vema na kwa bahati nzuri mawazo yake hayakuweza kupishana na uhalisia kwani baada ya kuuvisha mwili wake mavazi hayo alipendeza mno mithili ya walimbwende mashuhuri wa kimataifa.  Alijitizama katika kioo huku akigeuza kiuno na shingo yake mashariki na magharibi kwa kuambatanisha na mapozi tofauti tofauti kuendelea kuuhakikishia moyo wake juu ya uzuri na mvuto wa aina yake aliokuwa nao. 

Ilikuwa ni wazi kwamba siku hiyo Esther ndiye ambaye angeweza kuteka akili na hisia za wafanyakazi wenzake mbali na agenda muhimu ambayo ilikuwa ikienda kuwakutanisha katika kikao mapema ya siku hiyo. 

Alitizama saa yake na kugundua ya kwamba alikuwa nje ya wakati na jambo hilo lilimshtua kidogo Eeeh! Mungu wangu mpaka sasa nipo nyumbani na mimi ndiye sekretari  alizungumza hayo huku akifunga cheni nyembamba shingoni mwake, akavaa na hereni zake harakaharaka, akabeba pochi yake na kuelekea kwenye gari.  Licha ya uzuri na muonekano  wa kuvutia aliokuwa nao Esther vilevile alikuwa ni dereva mzuri wa magari na mwenye kuendesha kwa kasi mno na hilo alilifanya siku hiyo ili kuwahi kazini mwake.

Boss France alikuwa amekwisha kufika kazini na moja kwa moja alielekea ofisini mwake huku akionekana kuwa mwenye haraka kwa kutembea mwendo wa bandika mguu bandua mguu na kuwapungia mkono wafanyakazi wanzake waliokuwa wameshafika katika eneo la ujira wao. 

Boss france baada ya kufika ofisini mwake alijionea utofauti ambao hakuwahi kuuzoea kabla na utofauti huo ulikuwa ni namna ambavyo ofisi yake ilikuwa imepangwa kwenye mahadhi yenye kuvutia zaidi. 

Mmh! Ni nani huyu mwenye kunijali kiasi hichi? Licha ya kufanya kazi kwa miaka kadhaa ndani ya ofisi hii sijawahi kuona hata sekretari wangu akinitendea ubora huu. Ama pengine ni yeye?  Boss France alianza kwa kutabasamu kisha akaanza kujiuliza maswali kichwani mwake pasipo kupata mwafaka lakini aliendelea kuunadi ubongo wake kwamba ipo siku atakuja kujua ukweli juu ya suala hilo.

Muda wa kuelekea katika chumba cha makutano ya vikao ulikuwa umekwisha karibia na wafanyakazi wote waliopaswa kuudhuria katika mkutano walianza kuwasili.  Lakini jambo ambalo lilikuwa sio la kawaida ni kwamba mpaka muda huo Esther hakuwa ameshafika kazini. 

Boss france alitoka ofisini mwake nakuelekeza hatua zake hadi kwenye ofisi ya sekretari wake, alisogea karibu zaidi ya ofisi hiyo na kuanza kuita Esther.., Esther..., Esther... akifikiri labda pengine asingeweza kuwa mbali na eneo hilo lakini ukimya ulitawala. Mmh! Inakuaje mpaka muda huu ajaweza kufika kazini?, mbona siyo kawaida ama kuna jambo limems.... lakini hata kabla ya kukamilisha sentensi zilizotoka ndani ya kinywa chake, shingo yake iligeuzwa nyuma na mlio wa honi ya gari iliyokuwa ikiingia getini kwa kasi na hapo alitambua yakwamba alikuwa ni Esther na siyo mwingine. 

Aliondoka na kurudi ndani ya ofisi yake huku akiwa na imani yakuwa Esther alikuwa amekwisha kuwasili. Criiiiiii..., Criiiiii..., Criiiiii....  ulikuwa ni mlio wa simu ya mezani na moja kwa moja Boss france aliweza kutambua kwamba simu ile ilipigwa kutoka SERENA HOTEL. Ohh! Bila shaka atakuwa ni Meneja Tinno sultan  alizungumza hilo huku akielekeza mkono wake wa kushoto kupokea simu ile

Boss france: Hello! Boss

Meneja Tinno: Naam Boss wa maboss. Na kisha wote walicheka kicheko cha dhahabu “Hohohoo”

Meneja Tinno: umekuwa kimya sana Boss, hivi uko bongo hii ninayoijua mimi.?

 Boss france: Nipo Sultan, nipe ratiba za jiji. 

Hahahaa... Meneja Tinno alicheka huku wawili hao wakiendelea kusukumiana gozi Kwamba ni nani angefaa zaidi kumualika mwenzie. 

Lakini wakati wakiendelea na mazungumzo yao, baada ya kuanza tu kwa muda mfupi ilisikika sauti laini, sauti kinanda ndani ya ofisi ya Meneja Tinno. 

Hi.. Boss mafaili yote haya hapa. Sauti mali hiyo iliyotoka kwenye kinywa cha mwanamke aliyesadikika kuwa mrembo na mwenye madaha ya kiafrika, ilizungumza huku akiyaweka mafaili juu ya meza ya Meneja Tinno. 

Alahaulaah..! Sauti hiyo nyororo ilikuwa ni rahisi sana kupenya katika ngoma ya sikio la Boss france kuliko hata Meneja Tinno ingawa Boss france alipata mwaliko wa kuvinjari sauti hiyo kupitia simu ya mezani. Ubongo wa Boss france ulikuwa ni mwepesi sana kuyumbishwa na sauti za walimbwende na warembo mbalimbali. Na fahamu zake zilifikiri zaidi kwamba mwanamke yeyote yule mwenye sauti nzuri ni dhahiri shairi yakwamba angeliweza kuwa ni mzuri. 

Boss france hakusita kumuuliza Meneja Tinno ya kwamba sauti hiyo ilikuwa niya nani maana siyo siri iliweza kupenya hadi kutekenya na kusisimua ngoma ya sikio lake, ijapokuwa kuuliza kwake kulikuwa nikwa kupindisha pindisha maneno kama vile alikuwa akimtania Meneja Tinno

Boss France: Sultan, hivi bado unajilia vinono, haujapoaga tu tangu enzi hizo?

Meneja Tinno:  Hahahaa.. Boss France, Boss France, Boss France nadhani utakuwa umetafsiri sivyo mbona siku hizi nimekuwa mnyonge sana kwenye hayo mambo.

Meneja Tinno alijibu huku akivuta glass yake ya maji, akapooza koo na kuendelea na mazungumzo yao

Meneja Tinno: Bila shaka nahisi utakuwa na shauku ya kutaka kujua ni nani, ama sivyo?

Naye Boss France hakutaka kupoteza hata sekunde kumjibu Meneja Tinno

Boss France: Ndivyo, vivyo hivyo. hahahaa... akacheka kidogo na kuendelea mimi na wewe ni ndugu toka enzi na huwa hatufichani haya mambo kabisa

Meneja Tinno: Swadaktah.. sauti hiyo uliyoisikia niya sekretari wangu, anaitwa Zeyna.

Wakati Meneja Tinno alipokuwa akitayarisha jibu la kumpa nduguye, haikuwa kheri sana kwa Boss France kwani mapigo ya moyo wake yalipata kimuhemuhe kwa kudhani yakuwa meneja Tinno angeweza kumjuza kwamba sauti ile ilikuwa niya mpenzi wake.

Boss France: Kheheheee.. hapo sawa kabisa, sijawahi kuwa na shaka kabisa nawewe ndugu yangu nadhani ni namna gani unavyoelewa tulivyotoka mbali. Lakini haikumtosha kuishia hapo kwani alizidi kuchomekea taratibu matamanio yake.

Vp waweza niruhusu walau nisalimiane naye?

Meneja Tinno: Nadhani siyo busara sana kutumia simu ya kazi kwa masuala yasiyo ya kikazi, ila kama hautakuwa na haraka sana nitakupigia kwa simu yangu baada ya dakika mbili.

Boss France alijibu kwa shauku kubwa sana. Hapana shaka ni radhi kusubiri. Alikuwa yu pomoni wa husda na kutojali yakuwa wafanyakazi wenzie walikuwa wakimsubiri katika kikao kwani aliendelea kujifariji kwamba wangeweza kuendelea kusubiri kwakuwa yeye ndiyo aliyekuwa Boss wao. Alisogea karibu na mlango wa ofisi yake na kuufunga kabisa ili kuepuka usumbufu na kuendelea kusubiria masharti aliyopewa na Meneja tinno. 

Alizunguka kwenye kila kona ya ofisi yake huku macho yake yakikodolea saa iliyokuwa ukutani na kwenda na mapigo ya mshale uliokuwa ukizipunguza sekunde ili kukamilisha dakika mbili alizosubirishwa. Mkono wake wa kulia ulifanya kazi ya kukuna kichwa chake  ambacho hakikuwa na hata chembe ya muwasho wowote.

Ghafla tendo la uaminifu lilidhihirika baada ya Meneja tinno kutimiza ahadi iliyokuwa ikimweka mahewa Boss france. Simu yake iliita naye aliipokea kwa pupa.

Boss France: Hello Mrembo Zeyna. Mimi ni Menej...

Ghafla alitulia kama maji ya mtungi

La hasha! Lilikuwa ni wenge la uzito wa masumbwi maana alikurupuka ilihali meneja tinno alikuwa bado hajamuunganisha na sekretari wake Zeyna..

Meneja tinno: Kwani Boss una mdudu gani siku hizi?  Hahahaaa.. 

Meneja tinno akaishia kucheka na kuendelea na mazungumzo yaliyosikika “Zeyna rafiki yangu anataka kukusalimia ni Meneja wa Hyatt Recency The Kilimanjaro Hotel”

Zeyna: Owky!.. sawa Boss..

Hi. Boss

Boss France: Hello! Zeyna, mamb vp?

Zeyna! Salama tu chifu, kumbe unanifahamu kwa jina? Za wewe...

Boss France: Njema sana, na usijali kuhusiana na jina wewe ni maarufu sana.

Zeyna: Hahahaa.. haya bhana, vp majukumu.?

Kimya cha ghafla kikatawala, mzungumzo yao yalipata itilafu baada ya mlango wa ofisi ya Boss france kugongwa. Boss..., Boss..., Boss... unasubiriwa huku tuko nje ya muda sana. 

Alikuwa ni Esther aliyekuja kutoa taarifa na Boss france hakuwa na budi kutoa majibu “Sawa nakuja nilikuwa nakamilisha taarifa muhimu ya kikao”  Alijaribu kuendelea na mazungumzo ya simu Hello Zeyna.. Hey!  Lakini akagundua mawasiliano yalikuwa yameshasitishwa baada ya ukimya.

Aghaa! Shenzi sana, mambo yalishaonekana kuwa kamsererereko, shenzi kweli. Alifoka kweli kweli na kugonga gonga meza kutokana na uroho wa kiihisia uliokishwa kuanza kumpanda kichwani kama fisi aliyeona ujazo wa nyama katika himaya yake.

Hakukuwa na namna tena kwa wakati huo ila zaidi sana alifikiri kumtafuta kwa muda mwingine. Alimbidi abebe nyaraka zake za muhimu na kuelekea katika chumba makutano. Alipofika mlangoni iliwabidi wafanyakazi wote kusimama na akasogea mpaka kwenye meza kuu na kuketi ndipo na wengine wakaketi. 

Kimya kilitawala katika ukumbi wa kikao na kidogo kidogo zikaanza kusikika sauti za kiatu “khoh! Khoh! Khoh!”  hakuwa ni mwingine bali alikuwa ni Esther ambaye kiutaratibu alichelewa kuwasili kwenye chumba cha kiko baada ya Boss wake kuwa ameshaingia. 

Looh! Kuchelewa kwake pengine kuliweza kuwa kwa makusudi kabisa kwani watu waliokuwemo ndani ya ukumbi waligeuza shingo zao na kumtizama mrembo aliyekuwa amependeza na kuvutia vilivyo kiasi cha kuzifanya mboni za watazamaji zisiishiwe nishati ya kuendelea kufanya uchambuzi wa kina wa kifasihi.

Ebwanaeeh! Mwee, Mwee, Mwee, hivi Bwana kichuya na Msodoki mnaona vema kama mimi ninavyoona ama hii ni ndoto? 

Mazungumzo hayo yalikuwa ni ya Bwana jeshi rafiki mkubwa na bwana kichuya na Msodoki ambaye aligeuza shingo yake kulia na kushoto kama manati huku akiusifu mwonekano wa Esther ambaye alikuwa akiwasili katika ukumbi wa kikao. Mazungumzo ya kundi la utatu huo unganishi yalizidi kupamba moto na kuchagizwa na ujio wa Esther ilihali jambo lililowateta kwenye ukimbi huo lilikuwa la tofauti kabisa

Bwana kichuya: Hivi vitu vya kawaida sana, enzi zetu tulivichezea mno.

Msodoki: Hahahaa wapi wewe ushaanza tambo zako mimi si nakujua toka enzi za chuo.

Kichuya: Lakini tukiachana na masihara huyo binti ni wamoto, au unasemaje Bwana jeshi?

Mazungumzo yao ya kikao kipya ndani ya kikao maalumu yaliendelea huku kila mmoja akirusha jiwe na gizani na asijue linaenda kutua wapi.

Bwana Jeshi: Kichuya.., kichuya.., kichuya.. ndugu yangu mali kama hizi zina wenyewe, Za wakubwa hizi Ohoo!

Kichuya: Mali za wakubwa wapi? Bwanawee.. hata mimi mwenyewe nikiamua navimba nazo tu.

Bwana Jeshi: Wapi wewe. “umeshazoea vya kunyonga, vya kuchinja hauviwezi ng’o”

Hahahaa... wote walicheka kwa pamoja na ilikuwa si sehemu ya maisha yao kwani walishazoea kutaniana.

Baada ya Esther kufika kwenye meza kuu, alionyesha ishara ya kuinama mbele ya Boss France France ishara ya kuomba radhi kwa kitendo cha kuchelewa katika kikao ilihali kikao chenyewe kilikuwa bado hakijaanza.

Boss france alitikisa kichwa kuonyesha kwamba aliridhia na kikao kilianza mara moja.

 Kikao hicho kiliweza kuwakutanisha wakuu vitengo mbalimbali na wasaidizi wao ndani ya  Hyatt Recency The Kilimanjaro Hotel na lengo kuu ilikuwa ni kupongezana na kujadili zaidi juu ya mwenendo mzima wa mafanikio ya Hotel hiyo yenye hadhi ya nyota tano.  Lakini sambamba na hilo kikao hicho kilikuwa ni sehemu ya maandalizi ya kikao kingine cha kuwakutanisha Mameneja na Masekretari wa Hotel zote zenye hadhi ya nyota tano pamoja na wafanya biashara wakubwa na mashuhuri nchini na waliowekeza ndani ya nchi.

Esther ambaye ni Sekretarieti mkuu alisimama na kuwasalimu wahusika wote kisha akafanya utambulisho mfupi ulioendana na cheo cha kila mmoja ukumbini hapo, aliendelea kwa kusoma agenda za kikao na kumkaribisha moja kwa Meneja mkuu maarufu kama Boss france ambaye alifungua kikao hicho na kila mwakilishi wa kitengo husika aliweza kuzungumza. 

Kikao kilipamba moto na hatimaye ikafika zamu ya kitengo cha uendeshaji na usimamizi wa burudani ndani ya Hyatt Recency The Kilimanjaro Hotel. Kitengo hicho kilikuwa kikiwahusisha wazee wa mbaga na udambwu, udambwu na hawakuwa wengine zaidi ya lile kundi la Bwana Jeshi, Msodoki na Bwana Kichuya.

Bwana Jeshi ndiye aliyeweza kusimama na kuwakilisha kitengo hicho ndani ya kikao na kama kawaida yake alitawaliwa na Mbwembwe, tambo, vituko na mizaha ya hapa na pale katika maongezi yake.

Nikiwa kama mwakilishi na mkuu wa kitengo cha uendeshaji na usimamizi wa burudani ndani ya Hotel yenye hadhi kubwa duniani napenda nitoe shukrani zangu na pongezi kwa uongozi mzima pamoja na wafanyakazi wenzangu wa vitengo vyote. 

Kitengo chetu kiko imara katika kuhakikisha kwamba burudani haziishiwi chaji na hazikati wala kupungua ndani ya Hotel yetu ikiwa ni semehu ya kuhimiza na kushawishi wateja wetu waendelee kuipenda Hotel yetu zaidi na zaidi. 

Na mwisho ningependa kuwatakia viongozi wetu kikao chema na chenye mafanikio huko zanzibari kwa maslahi ya ustawi wa Hotel yetu pamoja na nchi yetu kwa ujumla

Alewiiiii.....  Wote walicheka  huku wakimpigia makofi kwa mazungumzo yake mazuri. Lakini Bwana jeshi akuishia hapo kwani alipaza tena sauti

Naomba kuongezea jambo kidogo kabla sijarudisha kijiti kwa uongozi. Basi watu wote wakakaa mkao wa kupokea dhahabu wakihisi yakuwa Bwana Jeshi alikuwa na jambo jingine la muhimu.

Nilikuwa nataka tu kuchomekea kwamba Sekretari wetu amependeza sana ila asitusahau na sisi watu wa tabaka la kati ni hilo tu.

Hahaha.... Vicheko vilizidi kunoga ndani ya ukumbi wa kikao kutokana na masihara ya Bwana jeshi na hatimaye Bwana jeshi aliamuriwa kuketi ili waendelee na kikao. 

Boss france aliendelea kuendesha kikao na kuwapongeza wafanyakazi wake wa juhudi walizokuwa nao katika ufanisi wao wa kazi. Baada ya hapo aliendelea mbele zaidi kwa kuwataja baadhi ya washiriki ambao watahusika katika kikao kikubwa ambacho kitaenda kufanyika Zanzibar kwa siku kadhaa.

Ndugu zangu kama nilivyokwisha kusema tutakuwa na kikao kikubwa Zanzibar kitakacho wahusisha Mameneja na masekretari wa Hotel zenye hadhi ya nyota tano ikiwemo yetu pamoja na SERENA  HOTEL.  Lakini pia wafanyabiashara wakubwa na wenye makampuni kama vile PRINCE COMPANY LIMITED inayomilikiwa na PRINCE na huyu ni mwekezaji mkubwa sana anayeishi nje ya nchi. Bila ya kusahau tutakuwa na mfanyabiashara mkubwa mwanadada mbichi kabisa hapa nchini anayetambulika kwa jina la TRICIE’

Looh! Wafanyakazi wote walibaki vinywa wazi na kuonekana kuwa na alama za mshangao baada tu ya kusikia kwamba kuna mfanyabiashara mkubwa na tena mashuhuri na maarufu ambaye ni mwanamke hapa nchini. Boss france alionekana kuanza kuingiwa na masihara ya Bwana Jeshi kwani naye alichomeakea Vipi Bwana Jeshi nawe tukujumuishe kwenye msafara kikao hicho?.. Naye akusita kujibu kwamba itapendeza zaidi.

Wakati kikao kilipokuwa kikielekea ukingoni mara ghafla ikasikika sauti za viatu vikigonga chini kwah.. Kwah.. Kwah.. dizaini ya vile vya Esther alivyokuwa akiwasili katika ukumbi wa kikao. Sauti hizo zilivuma kuja upande wa ukumbi na ikabidi watu wote wageuke kutizama ni nani aliyekuwa akija kwenye ukumbi wa kikao kwa muda huo ilihali kikao chenyewe kilikuwa ukingoni.

Alahaulah! Macho ya wazee wa mbaga ndiyo yaliyokuwa makini sana katika kufanya uchambuzi wa kina wa kisayansi na kisanaa juu ya kile kilichokuwa kikitaka kujiri ndani ya ukumbi. Uchambuzi wao ulianzia chini kwende juu ambapo walianza kuona miguu ya mwanamke mweupe, yenye ujazo wa chupa ya bia mithili ya kilimanjaro. 

Mavazi yake yaliyomkaa vema yenye kutiwa nakshi,nakshi yaliwafanya wazee wa mbaga kuendelea kuyapandisha macho yao juu zaidi ili kutaka kujua yakwamba mwanamke huyo mrembo alikuwa ni nani.

Watu wote waliokuwa ndani ya ukumbi walistaajabu baada ya kumtambua mwanamke yule aliyekuwa akitembea kwa madaha kuingia ndani ya ukumbi wa kikao alikuwa ni vicky

Haah! Huyu si Vicky.?  Msodoki alikuwa wa kwanza kunena.

Bwana Kichuya: Ni yeye kabisa wala haujakosea

Msodoki: Asee.. Bwana kichuya upo makini sana kwenye hizi mambo

Bwana kichuya: Naachaje kuwa makini, Jambo hili ni kama maji ya mto yakienda uelekeo mmoja hayajirudi tena. Naza chinichini nikwama Vicky na Esther ni maji na mafuta.

Bwana jeshi: Eeh! Kumbe, sasa leo kitaumana na anavyoingia sasa utadhani yeye ndiye mmiliki wa Hotel

Msodoki: Yetu macho wacha tujionee..

Vicky alizidi kusogea ndani na wakati huo naye Esther alianza kujisemea moyoni mwake.

Ama kweli! mwanamke huyu kama mchawi vile Mfyuuu. Alijikuta akisonya

Boss france alijikuta akitoa macho kama vile panya aliyeingia kwenye chumba cha paka na kubakia kuduwaa.

MWISHO

ENDELEA KUFUATILILIA MIENDELEZO YA TAMTHILIYA YA PESA ZA SHEMEJI KILA SIKU YA JUMAMOSI.

NCHI YETU, TAMTHILIYA YETU, FURAHA YETU. PESA ZA SHEMEJI ON AIR

“KAMA ELIMU YETU ISIPOTUOKOA, BASI VIPAJI VYETU VITUOKOE”

EEH! MUNGU BABA TUSAIDIE.

 

 

 

 

Post a Comment

2 Comments

  1. Tunapenda vitu vizuri na hakika hii ni story nzur pia🙏

    ReplyDelete
    Replies
    1. Asante sana, endelea kufuatilia miendelezo ya tamthiliya hii nasi tutazidi kuuwasha moto

      Delete