Mbona kama sielewi ina maana
sikulifunga gari langu, ila sidhani au nitakuwa nimelewa sana, Mhhh!...
hapana.
Boss France alikuwa akimshuhudia rafiki
yake akitapatapa kutafuta ufunguo wa gari bila ya mafanikio.
Sasa ina maana unatafuta nini? Funguo
wa gari unatafuta kama vile umedondosha akili kwenye katani.. Boss france alizungumza kilevi
mno na maneno yake hayakuwa na msaada wowote kusaidia kuupata ufunguo wa gari.
Meneja Tinno alikaa chini kwa mda na
kuendelea kufikiri alipoweka funguo wa gari lakini bado fikra zake hazikuweza
kufua dafu hata chembe.
Weweee nichukulie poa rafiki yangu
lakini mimi ni Standard, Quality, professional yaani
niko Comfortably.. lakini embu ngoja kwanza, wewe si
nilikukuta pale kaunta na yule muhudumu. Haujaacha kweli pale funguo?
Boss France alizungumza tena, ingawa
alikuwa amelewa sana lakini muda huu alizungumza jambo la maana kwa Meneja
Tinno.
Ahaaaaah! Kweli hapo umenena sasa. Kwa
maneno haya nimeamini kwamba wewe ni Standard, Quality and professional. ama mlewaji mwenye akili...
Meneja Tinno alikubaliana na maneno ya
Boss france na kujiaminisha yakuwa lazima funguo wa gari lake utakuwa pale
kaunta. Alisogea mpaka pale kaunta na kupaza sauti yake iliyogubikwa na ladha
shayiri.
Fetty, Fetty, Fetty... wewe Fetty..
Abeee Boss... Fetty mtakuja aliitika haraka kama
vile sumaku ya ngomani ivutavyo mchanga
Meneja Tinno alizidi kuipaza sauti yake
kwa ujasiri mkubwa. Haya nipatie funguo zangu
nilizoziacha hapa. Bila ya ubishi Fetty mtakuja alimpatia
Meneja tinno funguo hizo huku akimtizama machoni na kuilamba midomo yake.
Eeeh! Wewe mwanamke wewe.., Wallah
utakuja kuniuwa bure na vile sina mke hohohooo.. kauli za uropokaji zilizidi uzito
fikra za Meneja tinno na kuendelea kumpamba Fetty Mtakuja kwa kubwabwaja
sheheni ya Maneno.
Waooh! Kumbe hauna mke jamani na ulivyo
pedeshee.. Fetty naye
aliona ameanza kupata mlango wa kumwingilia Meneja tinno, huku mawazo yake
akiyaelekeza zaidi juu ya pesa za Meneja tinno kwa kuhisi kwamba alikuwa ni mtu
mwenye pesa nyingi mjini.
Fetty mtakuja alianza kumteka Meneja
tinno kihisia. Na hii ni baada ya kutambua moja ya udhaifu wake uliotokana na
kunywa pombe nyingi.
Sasa Boss, hivi unajishughulisha na
kazi gani vile? Fetty
mtakuja alizidi kumuhoji Meneja tinno, ili azidi kujipatia upenyo zaidi.
Hahahaaa.. hilo ni swali gani la
kuuliza mrembo kama wewe, ulipaswa kuuliza jinsi gani utaweza kutumia pesa
zangu... Meneja tinno
aliendelea kujisahau na kushindwa kufahamu makosa aliyokuwa akiyafanya kwa
mhudumu huyo wa kaunta kwa kuendelea kusema.
Kwa vile umeniuliza basi na mimi
nitakujibu mrembo Fetty. Ujue mimi nina pesa nyingi, alafu kazi yangu, kazi
yangu, kazi yangu... Mmmh!
Mimi nafanya kazi ndani ya Seren..., mara ghafla aliguswa bega na sauti
nzito ya kumkemea ikitua katika masikio yake na kumfanya akatishe kile
alichokuwa akimwambia Fetty.
Hakuwa mwingine bali alikuwa ni Boss
France aliyezinduka kule alipokuwa amekaa na kumsitisha rafiki yake kwa kile
alichokiona kilikuwa ni upuuzi, kwa kutaka kuvujisha siri zake kwa mwanamke
aliyefahamiana naye kwa mara ya kwanza.
Mazungumzo baina ya wawili hao yalikuwa
ya mvutano kidogo huku naye fetty akijaribu kutia lake neno katikati ya wawili
hao.
Boss France: Tafadhali naomba tuondoke eneo
hili, muda siyo rafiki na tumeshakunywa kupitiliza.
Meneja tinno: Sawa ila nipe dakika kama mia tano hivi
kidogo tu niongee na huyu mwanamke.
Boss France: Dakika mia tano looh!. Hivi
akili yako ya kawaida inazijua dakika mia tano, ama ni akili za pombe hizi?
Hahahaaa..
Fetty Mtakuja: Lakini si umuache mwenzako, azungumze
anachojisikia.
Boss France: Wewe, funga domo lako,
unamjua huyu ni nani?.. au unazungumza tu sababu mna
mdomo.
Meneja tinno: Haya
inatosha sasa, wote nimewaelewa, basi tutaondoka.
Boss France: Hapana
tena Hapana, Siyo tutaondoka, ndo tuondoke sasa, umesahau kwamba kesho
tutatakiwa kwenda wapi na vipi kuhusu maslahi ya kazi yako?
Meneja
tinno: Dah! Ila kweli, Kweli kabisa tunapaswa kuondoka
eneo hili.
Meneja tinno
aliweza kushawishika na maelezo ya Boss France ambayo yalikuwa na tija ya
kulinda na kuendeleza heshima ya kazi zao. Aliona hakukuwa na sababu ya
kuendelea kubishana na kuvutana kwa ajili tu ya mwanamke ambaye alimfahamu kwa
mara ya kwanza bila ya kuuelewa undani wake zaidi.
Boss France
alivuta wallet yake na kutoa kiasi cha pesa kulipia gharama zao walizotumia,
akamshika rafiki yake mkono kisha wakaondoka. Fetty mtakuja aliishia
kuwatolea macho na kukosa kufanya lolote la ziada, kwani fikra zake na mawazo
yake juu ya Meneja tinno kwa usiku huo, ziligonga mwamba.
Walipotoka nje,
Boss France aliendelea kugomba sana na kuwa mkali kwa rafiki yake. Ilikuwa ni
wazi kwamba hakufurahishwa na kitendo alichotaka kukifanya Meneja tinno.
Boss France: Hivi kumbe
ukinywaga pombe kupitiliza, unakuwa kama mweu ndugu yangu.
Meneja Tinno: Kwanini wasema hivyo.?
Boss France: Unawezaje kutaka kutoa siri
zako mbele za watu, au kisa yule mwanamke uliyeweza kuoanana naye kwa siku moja
tu?. Alafu pia, hawa wanawake wa baa siyo wa kuwaamini kabisa kwani wengi wao
huwa ni machangudoa kupitiliza, wanachokijali wao huwa ni pesa tu kuliko hata
afya zao.
Meneja Tinno: Nisamehe bure ndugu yangu, ujue
sikuliwaza hilo kabla na pengine ni hizi pombe tu.
Boss France: Angalia pombe zisiwe zinazidi
uwezo wako wa kufikiri, mwishowe uje kugeuka kituko na matatizo mbele za watu.
Meneja Tinno: Hili nalo neno kwakweli, lakini mbona
wewe mwenyewe ulilewa sana wakati ule mpaka ukaona kama vile Zeyna anapitapita
machoni mwako.
Boss France: Ni sawa ila tusianzishe ligi,
wewe ni zaidi ya rafiki kwangu hivyo tunaelewesha pale mmoja wetu anapojaribu
kukosea lakini pia huwezi jua kama nilikuwa nakuchora kwa wakati ule.
Meneja Tinno: Sidhani labda unieleweshe
vizuri.
Boss France: Sikuwa nimelewa kiasi hicho,
alafu ningekuwa mtu wa hivyo nadhani ningeshatembea na wafanyakazi wangu wengi
tu.. akiwemo hata huyu aliyefanya tukutane usiku huu.
Meneja Tinno: Sawa nimekuelewa, lakini waweza endesha
gari kwa utulivu kweli?
Boss France: Ondoa shaka kuhusu mimi, kwani Mimi
ndiye niliyetakiwa kukuuliza swali hilo.
Meneja Tinno: Usijali kabisa mimi nitafika salama
ndugu yangu.
Wawili hao waliweza kufikia maridhiano
na kila mmoja aliingia katika gari lake na kutimka kuelekea nyumbani kwake.
Boss France: alikanyaga mafuta vilivyo na
kufika mapema nyumbani kwake ingawa alikuwa amechoka sana.
Piiiii piiiii piiiiii honi za gari zilisikika kwa fujo nje ya
nyumba. Malila mwanajogini alitoka nje wepesi ili kufungua geti kwani
alishabaini honi zile zilikuwa niza gari la Boss wake.
Baada ya geti kufunguliwa Boss France
aliingiza gari kwa fujo sana nusura amgeuze nduguye kuwa bamsi la chalinze
Daaah! Boss mbona hivi, wataka
kunigeuza chapati mara hii. Alilalamika sana malila na bila shaka aligundua
yakuwa Boss wake alikuwa ameshatinga vitu vya London ya buza.
Boss France alishuka huku akipepesuka
na kupiga hatua mbili mbele, tatu nyuma na hata asieleweke kama alikuwa
akielekea ndani au kutoka nje ya geti. Hakuishia hapo bali aliendelea
kubwabwaja maneno yaliyokuwa hayana kikomo. Weeee tulia bwana siwezi kukufanyia
lolote baya ndugu yangu
Malila mwanajogini: lakini
umenikosakosa hapa ujue
Boss France: Kwani huoni niko fiti ndo maana
nimekukosakosa, ningekuwa sielewi-elewi ningeshakugonga hahahaa..
Malila Mwanajogini: Dah! Kwakweli utafika mbinguni
umechoka sana..
Boss France: Unasemaje weee.. neno la mwisho
umesemaje?
Malila Mwanajogini: Hamna mkuu, nimesema leo umetisha
sana Boss kama kawaida yako. Alisogea na kumshika Boss wake kisha akamsindikiza
hadi ndani ya chumba chake.
Kwa hali aliyokuwa nayo Boss France
haikumruhusu hata kuvua viatu vyake kwani alijiangusha kitandani kama mzigo na
kuanza kukoroma. Halikadhalika kwa Meneja tinno alifika nyumbani kwake na
kujitupia kitandani moja kwa moja na hata asipate muda wa kumfikiria Fetty
mtakuja yule mhudumu wa Baa.
Usiku ulionekana kuwa mrefu lakini kwa
Boss France alihisi kama ulitawaliwa na dakika chache za kumfanya yeye
kupumzika kwani palikucha haraka pasipo yeye kuumaliza uchovu aliokuwa nao.
Yalikuwa ni majira ya saa mbili kamili
asubuhi. Boss France alinyanyua simu na kumpigia rafiki yake Meneja Tinno ili
kumjulia hali.
Boss Tinno alipokea simu ya Boss France
na kuanza kusikika akipiga mihayo
Aawwagghhh... Asee vipi mkuu?
Boss France: Njema, natumai kumekucha
salama ndugu yangu. Vipi kuhusu jana ulifika
salama?
Meneja
Tinno: Hilo siyo la kuuliza nilifika salama kabisa. Vipi
kuhusu wewe?
Boss France: Salama vilevile.
Alafu utaondoka na Boti ya muda gani au umechukua ndege Sultan mzee wa
kukwea... hahahaa..
Meneja Tinno: Looh!
Kweli umenikumbusha jambo la maana, nilikuwa sielewi nawaza nini hasa kumbe leo
kuna safari ya muhimu. Kuhusu usafiri Sekretari wangu alifuatilia jana nadhani
atanijuza mapema tu.
Boss France: Ooh! Sawa Basi ngoja mimi
nikaserebuke na maji mara moja.
Meneja Tinno: Khaaa!! Unataka kuangusha
chupa tena na hali hiyo mkuu.
Boss France: Hapana
haujanielewa, namaanisha naenda kuoga mara moja. Kwa hali hii nikiongeza tena
mvinyo nitakuwa mgeni wa nani.
Meneja Tinno: Basi sawa...
Boss France alichukua mswaki na taulo
yake na kuelekea bafuni. Aliswaki na kuoga huku akiyafurahia maji. Kwa sauti ya
mbali alisikia Sms zikilindima kwenye simu yake.
Alitoka bafuni na kujinyoosha kulia na
kushoto kisha akajipangusha maji mwilini mwake. Hazikupita sekunde alisikia Sms
nyingine ikiingia kwenye simu yake. Naye bila ya kupoteza muda alianza
kuzifungua na kuzisoma moja baada ya nyingine.
Meseji ya kwanza ilikuwa niya sekretari
wake Esther. “Hello Boss! habari za asubuhi, natumai umeamka salama.
Nitafika hapo kwako muda wa saa nne ili tuondoke pamoja” Boss
France alitingisha kichwa na kujibu ujumbe ule kwamba “Sawa, karibu sana”
Kisha akaendelea kusoma meseji
nyingine. Na hii ya pili ilikuwa niya Meneja Tinno “Mkuu nimepata
ujumbe kutoka kwa sekretari wangu kwamba tutaondoka na Azam Marine ya saa sita
bila shaka nawewe jana ulinijuza kitu kama hicho”
Boss France alilazimika kujibu ujumbe
kutoka kwa meneja Tinno. “Ooh! Vizuri basi tutakuwa pamoja Boss”
Meseji zilikuwa nyingi lakini baada ya
kupitisha macho yake kwa haraka haraka akagundua yakuwa tayari amekwisha
malizana na zile za muhimu. Boss France aliendelea na maandalizi yake ya safari
kwa kuanza kupanga nguo na vitu vingine vya muhimu alivyoona vitamfana huko
aendapo.
Lakini ghafla akakumbuka yakuwa Esther
alimtaarifu yakwamba atampitia nyumbani kwake ili waondoke kwa pamoja. Boss
france alipaza sauti yake kumtaka Malila mwanajogini afike mara moja kupokea
maelekezo.
Naam Boss malila mwanajogini aliwasili
mapema kama alivyohitajika
Boss France: Kuna
mgeni atakuja mda si mrefu sasa.. ahahaa...
Malila mwanajogini: kwani
vipi Boss, ni nani huyo?
Boss France: Ni yule sekretari
wangu
Malila mwanajogini: ahaah!
Esther siyo, ama mwingine Boss?
Boss France: Ndiye, kwani
umemjuaje? Boss
france alifanya mazungumzo yawe ya swali juu ya swali.
Malila Mwanajogini: Hahahaa Boss mbona huwa
unamzungumziaga mara nyingi pamoja na yule nani... sijui...
Boss France: Nani huyo tena?
Malila mwanajogini: Yule mwingine.. aaahh .. ngoja
nimkumbuke kidogo. Malila mwanajogini alifikiri kwa sekunde kadhaa na kuendelea
na mazungumzo baada ya kupata majibu kamili. Anaitwa Vicky kama sijakosea
Boss France: Hahahaa Vicky... hahahaa embu
tuyaache haya. Sasa embu andaa chochote kwa ajili ya Esther
Malila mwanajogini: Vipi kuhusu wewe
Boss France: Usijali kuhusu mimi, unaweza
ukaendelea
Malila mwanajogini: Sawa Boss.
Wakati Boss France akiendelea na zoezi
lake la kupanga vitu. Mawazo yalimjia juu ya safari yao itakavyokuwa papo hapo
akasitisha jukumu lake la kuendelea kupanga vitu.
“Nadhani itakuwa safari nzuri sana japo
niya masaa machache, bila shaka nitaenjoyi sana na wenzangu kwani sijawahi
safiri kwa usafiri wa kutumia chombo cha maji, Azam marine hiyo kama naiona
vile alafu mara ndo paap pembeni amekaa Zeyna hahahaaa...” Boss France alijiwazia huku mawazo yake
yakienda mbali zaidi ya fikra zake. Hakika ilikuwa ni moja ya safari iliyotaka
kumpa kiwewe licha ya yeye kusafiri mara nyingi hadi kwenye nchi za ughaibuni
kuiwakilisha kampuni yake.
Boss France alitaka kuendelea na mawazo
yake ya kusadikika lakini mara ghafla alishtushwa kusikia sauti ya Esther
aliyekuwa akikaribishwa Sebuleni na malila mwanajogini.
Eheeh! Huyo ni Esther ashafika, yuko
moto kweli kwani ratiba zake huwa anazipangilia vilivyo
Boss, Boss mgeni wako ashafika huku alikuwa ni malila mwanajogini akitoa
taarifa yenye harufu nzuri iliyokwisha kumfikia Boss France mapema sana.
Nakuja, nakuja namalizia jambo kidogo
hapa. Boss
france alijibu huku akitizama saa yake na kugundua yakuwa muda ulikuwa siyo
rafiki sana. Alimaliza kupanga vitu na kuvaalia kwa uharaka suti nyeusi
iliyomkaa vilivyo huku akiyatikisa kidogo mabega yake. Mahojiano ya kupendeza
kwake yalikuwa ni kati yake na kioo chake cha ukutani. Alijitazama na kujipa
maksi zilizouridhisha moyo wake.
Alitoka ndani ya chumba chake baada ya
kujipalilia na marashi yaliyokuwa na manukato ya kunukia kiasi cha kuwavutia
njiwa kuja kizipiga filimbi.
Boss france alitembea kwa madaha
kuelekea alipokuwa amekaa Esther ambaye alishindwa kujizuia kuonyesha tabasamu
lake na kushindwa hata kuficha furaha yake aliyokuwa nayo siku hiyo kwani
alisimama na kumkumbatia Boss wake.
Woow.. Boss umependeza sana...
Naye Boss france alicheka kidogo na
kuonyesha tabasamu la aina yake kisha akasikika akisema “Asante sana Esther,
nawe umependeza vilivyo kama ilivyo kawaida yako”
Wakati hayo yakiendelea Malila
mwanajogini alibakia kuwa kushuda na kushindwa kujua ni wapi angelielekeza
tabasamu lake kati ya wawili hao zaidi ya kubakia kujichekesha.
MWISHO
ENDELEA KUFUATILIA SEHEMU ZIJAZO ZA
TAMTHILIYA HII. BILA YA KUSAHAU KUFUATILIA ORODHA ZA TAMTHILIYA ZA MTUNZI NA
MWANDISHI SEBASTIAN S. MASABHA.
1. PENZI LA MASHAKA
2. SUKARI YA KIJIJI
3. KONEKNESHI ZA VALENTINE
Na shairi la
DIMBA LA
MKAPA
0 Comments