Chris aliendelea kuganda kwa mshtuko wa dakika kadhaa kutokana na ujumbe wa simu alioupokea kutoka kwa mkewe, lakini akili yake ilikosa cha kufanya kulingana na pombe nyingi alizokuwa amezinywa.

Hakuwa Kendy wala Mr. Jokeri walioweza kutambua kilichomsibu Chris kwa wakati huo, kwani Kendy alikuwa bize kuhudumia wateja wengine naye Mr. Jokeri alikuwa akijimimina pafu mmiminiko za mvinyo huku akiburudika na play list zilizokuwa zikipigiliwa misumari na Dj.

Monica lover, lover my sweet baby your love kill me”

Alooh! Wee..., Oya nyie... huyu Dj Anajua hatari, embu sikia kitu hicho.

Mr. Jokeri aliyeonekana kuwehuka na wimbo wa Tekno, alikuwa akiimba huku akigeuza macho yake kwa Chris aliyekuwa kimya bila ya kuzungumza chochote.

Mara ghafla Mr. Jokeri alipigwa na butwaa ya kumuona Chris akiwa amegandisha macho yake kwenye simu na bila kuongea, kucheka wala kulia.

Wakati chris akiendelea kuishangaa simu yake mara Paap! ukaingia ujumbe mwingine wa simu kutoka kwa mkewe Julieth na hapo Chris alijikuta akipiga kelele

Tafadhali mke wangu usifanye hivyo, tafadhali nakuomba Julieth

Kelele za Chris ziliwashtua na kuwaogofya watu waliokuwa karibu naye na kumfanya Kendy kuangusha glasi aliyokuwa akimpatia mteja na kuziba masikio yake huku akikimbilia alipokuwa Chris.

Ujumbe wa pili aliotumiwa Chris ulikuwa mzito sana kiasi cha kuzisisimua hisia zake na kumpanikisha kwani hata pombe nazo zilikata ghafla kichwani mwake.

Mume wangu, kwakua umeshindwa kunisikiliza, basi mimi nakunywa sumu niteketee na kiumbe chako tumboni, nakutakia maisha mema na yenye furaha”

Wee...... damu ni nzito kuliko maji Chris alisimama mkuku mkuku na  kuanza kuondoka huku akihangaika kumpigia simu mkewe bila ya simu zenyewe kupokelewa.

Kendy na Mr. Jokeri walijaribu kufanya jitihada za kumzuia Chris ili kutaka kujua kile kilichomkuta lakini jitihada zao ziligonga mwamba.

Jamani Chris mpenzi, kuna nini mbona hivyo?

Kendy alizidi kulalama lakini wapi, kwani ndo kwanza Chris alibadili mwendo wake kutoka kutembea hadi kukimbia kuelekea nje.

Chris alikuwa dhofulali wa akili na mwenye kupaniki sana kiasi cha kusahau ya kuwa alikuwa amekuja na gari lake ndani ya Royal Village Hotel.

Alifika getini na kumsihi mlinzi amwitie Boda boda ili aweze kuwahi

Mlinzi: Lakini Boss si ulikuja hapa na Harrier yako nyeupe, au nimekufananisha?

Chris: Ooh! Camong, asante nilijisahau kidogo.

Mlinzi: ila mbona haraka, haraka kiasi hicho Boss kuna nini?

Mlinzi alijikuta akiuliza swali lililoishia hewani kwani Chris hakuwa na hata sekunde za kuendelea kupoteza zaidi ya kutoa gari lake na kumuwahi mkewe nyumbani.

Hii mbona mpya, ndo kusema kwamba pombe zimemkolea kichwani au kuna pombe mpya leo imeingia hapa ama ndo nini sasa? Ndo maana mimi nilikataaga hizi habari za pombe-pombe, yaani kuja kuwa mwehu bila ya mpangilio Wooy....

Ulikuwa ni wasaa wa mlinzi kujiongelea na kutoa kila povu lililokuwa limemjaa mdomoni

Ama kweli jambo usilolijua ni kama usiku wa giza”

Mr. Jokeri na baadhi ya watu wengine walitoka nje kushuhudia kilichokuwa kikiendelea lakini wakati huo Chris alikuwa amekwisha kuondoka.

Oyaaah... Chuma kuna jamaa  katoka mda huu.

Mr. Jokeri aliuliza swali lililokatishwa na chuma, kumbe mlinzi yule alikuwa akiitwa chuma.

Embu ngoja kwanza Mr. Jokeri. Unamsemea yule mvaa suti na moka ambaye anakujaga hapa na gari yake ikiwa wima na kuondoka kama vile gari imekatika Centre-bolt?

Mr. Jokeri: Naam, Barabara kabisa huyohuyo.

Chuma: Huyo alikuja hapa mbiombio nusura asahau hata gari lake.

Mr. Jokeri: Aya bhana, mimi narudi zangu ndani mda wangu bado.

Chuma: poapoa, ila nawe kunywa jiangalie yasije yakakukuta.

Mr. Jokeri: Wee.. thubutu, mimi ni jemedari.

Mr. Jokeri alitembea na kurudi ndani huku miguu yake ikipiga mguu pande, mguu sawa. Lakini pia hakusita kuyakiri kimoyomoyo maneno ya mwisho ya Chuma japo kwa kishingo upande.

Ila kweli hizi pombe si chai, kuna siku zitakuja kunizulia balaa.. lakini bwana wee.. potelea pote”

Mr. Jokeri hakujali kabisa kuhusu hilo ila aliendelea kujilaumu kwamba, ilikuwaje alikaa muda wote ule bila hata ya kuchukua namba za Chris, alihisi ilikuwa ni kama pigo kwake, kwani yeye ndiye aliyeanza kuwa rafiki wa karibu wa Chris licha ya kuwa walifanya mazungumzo kwa mara ya kwanza.

Kendy alipata shauku ya kutaka kujua kile kilichokuwa kikiendelea juu ya Chris baada ya kumuona Mr. Jokeri akirudi katika eneo lake la kujidai.

Kendy: Embu naomba uniambie kilichomkuta mpenzi wangu.

Mr. Jokeri: Mpenzi wako?

Kendy: Ndiyo ni mpenzi wangu.

Mr. Jokeri: Mbona hakuniambia hilo kabla, wakati wote nilipokuwa naye.

Kendy: Sasa wewe, umeona kipi cha ajabu hasa. Nitashindwa kukutofautisha na watu wa kaliua huko.

Mr. Jokeri: Shauri yako, Chris ameondoka hapa akimtaja mkewe.

Kendy: Heeh! Mkewe tena! kumbe yule mwanamke aliyekuja hapa alikuwa ni mkewe.?

Mr. Jokeri: Ndiyo, wewe si ulikuwa bize na mambo yako wakati huo, yaani kila mwanaume anayekuja hapa na vijisenti vyake unamtaka.

Kendy: Wewe nae.. hovyo kweli, mimi nilidhani yule mwanamke alikuwa ni hawara wake tu.

Wawili hao walizidi kujibizana na kuropoka kwa muda kidogo, huku wasijue yakuwa kuna baadhi ya watu wengine waliokuwa wakifaidika na kunufaika kwa uropokaji wao.

Janeth alikuwa ni mmoja ya watu walioweza kusikia maongezi baina ya Kendy na Mr. Jokeri na kuweza kufahamu yakuwa aliyekuwa akiongelewa alikuwa ni mume wa Julieth mwanamke ambaye aliweza kukutana naye na wakazungumza kwa ufupi.

Mungu wangu, nimesikia wakimzungumzia Chris, yaani huyu Kendy ameanza kutembea na Chris wakati hali yake anaifahamu. Hii ni hatari jamani”

Janeth aliwaza na kuwazua na kuona ni bora ampigie Julieth na kumpa taarifa hizo haraka iwezekanavyo.

Janeth alisogea na kujibanza sehemu iliyokuwa na ukimya kisha akajaribu kumpigia julieth ili ampe taarifa zile lakini simu iliita mara kadhaa pasipo kupokelewa.

Jamani Julieth Dada angu, pokea simu basi”

Janeth alifanya jitihada za hapa na pale lakini haikuwezekana, mwishowe alikata tamaa na kuzidi kunyong’onyea.

Nifanye nini jamani, mbona kama nashindwa. Alizidi kufikiri huku akiwa amejishikia tama lakini “Mungu Si Athumani” kwani Janeth alipata wazo la kumuandikia Julieth ujumbe mfupi wa simu.

Habari dada julieth, naomba tuwasiliane haraka iwezekanavyo. By Janeth”

Wakati huo Chris aliyekuwa mwingi wa hofu na presha, alikuwa amekwisha kufika nyumbani kwake kisasa. Katika makazi ambayo alikabidhiwa na kampuni yake anayoifanyia kazi.

Julieth, Julieth, Julieth.. mke wangu fungua mlango

Chris aligonga mlango kwa nguvu na kumuita mkewe, lakini ukimya ndiyo ulioweza kumpokea. Alikimbilia upande wa dirishani na kuchungulia endapo kama angeweza kubahatika kuona chochote kile ndani lakini pia alishindwa.

Jasho jingi lilianza kumtoka na homa kumpanda kichwani mwake, kwani alikuwa ni mtu aliyezidi kuchanganyikiwa na kutapatapa huku na huko.

Chris aliamua kurudi mlangoni na kujaribu kusukuma mlango. Kwa bahati nzuri alifanikiwa kuingia ndani na kumkuta mkewe akiwa amelala chini huku vifaa vya simu ya mkewe vikiwa vimetawanyika.

OMG! Chris aliogopa sana kumuona mkewe akiwa katika hali ile na muda huu hakuwa hata na chembechembe za pombe kichwani mwake. Alipiga magoti na kupeleka mkono wake upande wa kushoto wa kifua cha Julieth ili kupima mapigo ya moyo wake.

Ilikuwa haitoshi kwa Chris kupata majibu sahihi endapo kama mkewe alikuwa ni mzima ama lah! Hivyo Chris aliamua kulaza kichwa chake na kutega sikio lake juu ya kifua cha Julieth na kugundua yakuwa Julieth alikuwa ni mzima.

Chris alichunguza kushoto na kulia, alifukua mashuka na kurusha vitu huku na huko kujiridhisha endapo kama Julieth alikuwa amejidhuru na sumu ama kitu kingine kile. Lakini hakukuwa na chochote alichoweza kukitilia machoni mwake.

Looh!  Walau Chris aliweza kuipata ahueni na kuzishusha pumzi zake taratibu. Papo hapo alianza kufanya kazi ya kumtikisa tikisa, kumpepea na kumrushia maji usoni mkewe kwa kuhisi pengine angeweza kuzinduka.

Mawazo na jitihada za Chris ziliweza kuwa na msaada kwa mkewe. Julieth alianza kukohoa na kupepesa macho yake. Kitendo hiki kilimfanya Chris kutoa tabasamu lake na  kuonekana mwenye kurejelewa na furaha yake.

Julieth alizinduka na kuona taswira ya mumewe usoni mwake. Alihisi kama ni ndoto vile kutokana na hali aliyokuwa nayo.

Chris alimvuta mkewe kifuani mwake na kumkumbatia. Machozi yalimbubujika taratibu ikiwa ni ishara ya kujuta kwa kile alichokuwa amemfanyia mkewe.

Chris aliendelea kumpapasa mkewe mgongoni huku maneno ya faraja na upendo yakimtoka mdomoni mwake.

Haukuwa na haja ya kupitia mateso haya, kwani hukukuwa na baya lolote ulilonitendea zaidi ya ujinga wangu, zile zilikuwa ni pombe wala hazikuwa akili zangu, nakiri nimekukosea sana. Nisamehe mke wangu, nakuahidi kwamba sitoshikamana na baya hili tena

Chris alitoa maneno mazito yenye upendo na faraja. yaliyoweza kupenya katika mishipa ya hisia za mkewe na kumfanya kutokwa na machozi. Julieth hakuweza kuwa na ubishi wowote ule zaidi ya kumsamehe mumewe.

Chris alijitahidi kufanya kazi kubwa ya kumtuliza mkewe na kuhakikisha anamrudisha katika hali yake ya kawaida.

Usiku ulikuwa ni mkubwa na mnene kwani mishale ya majira ilikuwa imeshatembea na kusogea vilivyo. Naye Julieth alianza kupata nguvu baada ya kupewa na kunywa glass moja ya kinywaji cha Lucozed chenye kuupa mwili nguvu.

Ilikuwa ni kitu kizuri sana kwake nakwa mumewe, kwani hata nguvu za kuongea zilimjia ghafla.

Julieth: Mume wangu, wacha nitandike kitanda tupumzike maana nakuona umechoka sana.

Chris: Hapana mke wangu usijali, wacha namimi leo nifanye jukumu hilo.

Julieth alimkubalia mume wake huku akionekana kuwa mwenye furaha na amani. Naye Chris alifanya jukumu hilo na kumsihi mkewe kuja kupumzika.

Kitanda chao kilikuwa ni kizuri kilichopambwa na duveti pamoja na mito iliyokuwa haifikirishi usingizi kusogea karibu yao.

Chris alivuta mto na kukilaza kichwa chake huku mwili wake ukiwa kitandani. Naye julieth alipanda kitandani na kujilaza kifuani mwa mumewe Chris.

Usiku nao ulizidi kuwa mtamu na wenye ladha isiyokwisha kwa wanandoa hao, kwani usingizi uliwachukua, ukawabeba na  kuwasafirisha hadi ng’ambo, kisha ukuwatua katika asubuhi ya siku nyingine.

MWISHO WA SEHEMU YA PILI

N.B- USISAHAU KUDONDOSHA COMMENT YAKO NI MUHIMU SANA.

 

ITAENDELEA SEHEMU YA TATU. PIA USIKOSE KUFUATILIA MIENDELEZO YA TAMTHILIYA MBALIMBALI KUTOKA KWA MTUNZI NA MWANDISHI SEBASTIAN S MASABHA

1.PESA ZA SHEMEJI

2. PENZI LA MASHAKA

3. SUKARI YA KIJIJI