A story by Sebastian Masabha

0758-162527

Ujue nitakupiga hadi nikuue wewe mwanamke maana umekuwa mbishi sana siku hizi, kila kitu ni kubishana na mimi naona unapoelekea unataka kunipanda kichwani

-Hapana Mume wangu naomba tuondoke twende nyumbani embu angalia usiku wote huu nimekufuata hapa baa lakini bado hautambui umuhimu wangu mme wangu mbona unakuwa hivi lakini?

Yalikuwa ni mabishano yasiyokuwa na amani wala maelewano kati ya wanandoa wawili katika moja ya kumbi za starehe zilizoko Jijini Dodoma. Kumbi hilo lilifahamika kama Royal Village Hotel ambapo ni moja ya kitovu cha Starehe kilichosheheni kila aina ya burudani zikiwemo Live band, Dancing Club, Vyakula vya gharama na mivinyo ya kila aina hali kadhalika vyumba vya kupumzikia wageni.

Royal village Hotel ilijizolea umaarufu mkubwa na hii ni kutokana na watu wengi maarufu, wenye pesa pamoja na nyadhifa mbalimbali kupenda kuweka kambi ya kupumzisha akili na miili yao kwa kujipatia burudani na ladha tofauti tofauti ndani sehemu hiyo.

Wawili hao walianza kupishana kikauli na hii ni baada ya Julieth mke wa ndoa wa Chris kumpigia mme wake simu kwa muda mrefu na simu zake zote kukatwa kila mara bila hata ya jibu lolote lile. Suala ambalo lilimfanya Julieth kukosa furaha na amani kiasi cha kuchukua uamuzi wa kutoka nyumbani kwake na kwenda kumtafuta mumewe ambaye mara kadhaa amekuwa akirudi nyumbani akiwa amelewa mno.

Jambo hili lilizidi kushika kasi na hii ni baada ya wawili hao kufunga ndoa wiki kadhaa zilizopita.

Halaulaah ama kweli hata ndoa nayo ina makali yake”

Julieth aliendelea kumsihi mume wake waondoke wakati huo ndo kwanza Chris alikuwa ameanza kuikata chupa yake ya pili ya mvinyo kati ya chupa kumi alizokuwa amekwisha kuzilipia.

Ilikuwa ni ngumu sana kwa Chris kumuelewa mke wake kwa muda huo kwani pia aliyaelekeza macho yake kwa warembo mbalimbali waliokuwa wakizidi kumiminika ndani ya Royal Village Hotel.

Shenzi yaani huyu mwanaume sijui ananichukuliaje mbona hii kazi sasa, ndoa yenyewe ndo kwanza tumefunga majuzi tu na hapa sina hata ndugu wa karibu wa kumshirikisha jambo hili na hata nikisema niwajulishe ndunguze kwa simu bado hawataniamini maana yeye ndo kila kitu kwao. Oooh! Mungu wangu”

Julieth alinena maneno mazito na yenye uchungu mkubwa sana kichwani na moyoni mwake kwani hakutegemea kumuona mumewe akiwa katika hali ile hasa ukizingatia zaidi ilikuwa ni kama suprise ya mapema sana ndani ya ndoa yao.

Baada ya muda kidogo kupita idadi ya warembo na mapedeshee wenye vitambi vya kubebeka kwa matoroli ilizidi kumiminika ndani ya Royal Village Hotel huku Julieth akiendelea kufanya jitihada za kuhakikisha anaondoka na mume wake katika eneo hilo.

Alikuwa ni Janeth pekee mmoja kati ya wahudumu ndani ya Royal Village Hotel ambaye aliweza kuguswa na kile alichokuwa akikishuhudia kati ya wawili hao. Janeth alimsogelea Julieth na kumvuta pembeni kidogo, macho yake na uso wake vilijawa na huruma kiasi cha kufikiri pengine Julieth alikuwa ni nduguye aliyezaliwa naye tumbo moja.

Janeth: Dada, samahani yule ni nani kwako?

Julieth: Yule ni mume wangu?

Janeth: khaah! Ni mumeo kumbe, nimekuwa nikimuona mara nyingi hapa hasa siku za weekend.

Julieth: Ndiyo Chris ni mume wangu, tena wa ndoa kabisa yaani tuna wiki nne tu tangu tulipofunga ndoa yetu. (Julieth alizungumza kwa uchungu sana huku machozi yakimlengalenga)

Janeth: Pole sana dada yangu, najua siwezi kuvaa viatu vyako ila binafsi pia nimeumizwa na jambo hili nikiwa kama mwanamke mwenzako.

Julieth: Asante sana kipenzi, kwani wewe ni nani hapa?

Janeth: Mimi ni muhudumu tu, kazi yangu ni kubeba, kupeleka chupa kwa wateja zikiwa na mvinyo na kurudisha kaunta zikiwa tupu tena na opena yangu mkononi.

Julieth: ilikuwaje mpaka ukaipenda kazi hii? maana nakuona kuwa mtu wa tofauti na niwaonavyo wenzako hapa.

Janeth: Wacha tu dada yangu ni stori ndefu sana, wewe una maumivu yako na mimi vilevile tuyaache tu kwanza mpaka wakati mwingine.

Looh! Janeth aliongea kwa uchungu sana huku akitokwa na machozi kitendo kilichomfanya Julieth kuzidi kujisikia vibaya na kukosa cha kufanya kwani naye matatizo ndiyo yaliyomleta pale Royal Village Hotel. Hivyo wawili hao waliamua kubadilishana namba na kila mmoja kuendelea na jambo lake.

Julieth alirudi mkuku mkuku pale alipokuwa Chris. Alimtizama huku akiwa ni mwenye hasira sana na wala Chris hakutaka kujali kuhusu hilo kwani mvinyo ulizidi kumkolea kichwani mwake.

Chris alinyanyua chupa ya mvinyo na kumsogeza Julieth mdomoni mwake

Haya kunywa sasa na wewe siyo unaniangalia tu mimi”

Julieth hakuwa na muda wa kujibu lolote lakini aliipiga ile chupa kwa mkono wake wa kulia na kuiangusha chini kisha akamwambia

Sina muda wa kuendelea kukaa hapa kukubembeleza, wakati unazidi kunidhalilisha, hauthamini hata utu wangu hivyo utajijua mwenyewe ukiamua kurudi nyumbani ama lah!”

Hakukuwa na muda wa kupoteza kama alivyodai Julieth kwani aliamua kutoka nje akachukua usafiri wa tex na kurudi nyumbani kwake.

Chris alibakia na bumbuwazi, huku akijitwika ulimbo wa hasira za kumnasa ndege kasuku pasipo mipango.

“Hivi huyu mwanamke ananionaje, anathubutu kunimwagia pombe yangu kweli. Hajui hii ni pesa kabisa”

Walevi wenzake waliokuwa na pesa za kuchezea na hata wasiijue kesho yao itakuwaje walimcheka sana baada ya kushuhudia tukio lile. Naye chris aliendelea tu kulalama

Kendy mhudumu aliyekuwa kaunta akimjaza Chris chupa za mvinyo, alitoka na kitambaa cheupe na kwenda kulifuta shati la Chris lililokuwa limelowa na Pombe baada ya mtafaruku kati yake na mkewe.

“Pole Boss, mwanamke anathubutu vipi kukufanyia hivi? Mshenzi kweli hajielewi”

Kendy aliongea maneno ya kumkejeli Julieth huku  akiendelea kumjaza sumu Chris ambaye zilishachanganya kichwani.

“Yani kwanza ana bahati sana wewe ni mpole, ingekuwa ni mwanaume mwingine angeshachezea”

Kendy hakuonekana kuwa na nia njema kabisa na ndoa ya Chris kwani mara hii aliendelea kuzungumza huku akipeleka mkono wake kwenye kifua cha Chris na kufungua vifungo kadhaa vya shati lake huku akijidai alikuwa akimfutafuta na wala Chris asiseme chochote kile.

Mmoja wa wale walevi waliokuwa wakimcheka chris alisimama na kusogoe mpaka pale alipokuwa amesimama na Kendy na Chris kisha akamgusa Chris begani na kubwabwaja mawili matatu.

“Asee jamaa yangu, ngoja kwanza niingie maliwatoni nikirudi nakuja kwako tuongee kwa kina”

Chris alitingisha kichwa chake kuonesha ishara ya kumkubalia mtu yule wakati Kendy alishtuka na kuutoa mkono wake mara moja kwenye kifua cha chris na kurudi kaunta.

Hazikupita dakika mbili mlevi yule akawa amerudi, alipitiliza moja kwa moja mpaka kwenye meza yake na kuchukua chupa yake ya pombe kisha akaelekea kaunta alipokuwa amekaa Chris na kuanza mazungumzo.

Vp Boss, Mr. Jokeri hapa

Chris: Asee njema tu, karibu Mr. Jokeri

Kabla ya kuendelea na mazungumzo yao Chris alisikia ukipigwa moja ya nyimbo anazozipenda, alinyamaza kidogo na kuamza kutingisha kichwa chake, masikio yake yalipata ladha madhubuti, akaanza kuimba wimbo ule taratibu na mwishome akaamua kusimama na kuanza kucheza. Mr. Jokeri na Kendy walikuwa wakimtazama na kuzidi kuangua vicheko.

Wimbo ulikuwa mtamu kwelikweli kwani Chri aliucheza hadi ulipokwisha kisha akarejea kwenye kiti chake.

“Asee huu wimbo huwa naupenda sana, unanikumbusha mbali kwelikweli,

Wote walicheka na Kendy akaongezea-

“Tumekuona Boss, umeyarudi hatari”

Chris: Hahahaa, embu mpe Mr. Jokeri kinywaji anachokitaka maana inaonekana amekuja na mambo mazuri.

Kendy: Sawa Boss Chris

Chris: Eeh! Mara hii tu ushanijua na jina langu.

Kendy: Niliona jina lako kwenye moja ya vitambulisho vyako wakati nilipokuwa nikikufutafuta.

Chris: Ohooh! Hapo sawa, maana ulinishtua.

Baada ya hapo mazungumzo ya Chris na Mr. Jokeri yaliendelea

Chris: Ndiyo Mr. Jokeri, lete habari

Mr. Jokeri: Ujue bila yakupindisha maneno, wewe ni mtu safi sana.

Chris: Kivipi Mr. Jokeri?

Mr. Jokeri: Wala usijali mkuu, nitakwambia tu.

Wote walizidi kucheka na kuendelea kupata mvinyo. Wakati huu palizidi kuchangamka na kunoga ndani ya Royal Village Hotel kwani ulifika mda wa kila mtu na wakwake yaani wawili wawili huku wengi wao wakicheza mziki na kuburudika.

Chris alijimimina chupa yake ya saba ya mvinyo na kuanza kuzungusha macho yake kushoto na kulia na kila alipotazama aliona watu wote pale ndani wakiwa wawili wawili. Siyo wateja kwa wahudumu wala wahudumu kwa wateja wao hata wateja kwa wateja.

Chris aligeuza shingo yake pale kaunta akamtizama Kendy na kuachia tabasamu huku akifutafuta uso wake mara tatu tatu kwa mkono mithili ya kutoamini alichokuwa akikiona kwa Kendy.

Chris alifanya hivyo mara kadhaa kisha akaanza kutia maneno yake.

Chris: Hivi ina maana leo, ndiyo siku ya wapendanao “Valentine day”?

Mr. Jokeri: Mbona bado sana ndo kwanza hii December.

Chris: Kumbe... ua ninyi wenzangu hamuoni kama mimi vile, embu angalieni kila mahali hapa ndani.

Mr. Jokeri: Mbona hii kawaida sana ndani ya hili Jiji. tena ngoja weekend ijayo nikupeleke mahala pengine utashangaa zaidi.

Chris alicheka kidogo na kukubaliana na maneno ya Mr. Jokeri. Lakini  haikupita hata dakika akapokea Sms kutoka kwa mkewe Julieth na baada ya kuisoma alipeleka mikono yake kichwani macho yakamtoka na kubakia kinywa wazi.

MWISHO

ITAENDELEA SEHEMU YA PILI. PIA USIKOSE KUFUATILIA MIENDELEZO YA TAMTHILIYA MBALIMBALI KUTOKA KWA MTUNZI NA MWANDISHI SEBASTIAN S MASABHA

1.PESA ZA SHEMEJI

2. PENZI LA MASHAKA

3. SUKARI YA KIJIJI