.

Sehemu ya 01.

Ilikuwa ni siku ya tatu tu! Tangu niyaanze majukumu yangu katika kampuni mama ya usafirishaji. 

Sikuwa na uzoefu mkubwa sana kazini, kwani ndo ilikuwa mara yangu ya kwanza kuingia rasmi kwenye mfumo wa ajira.

Wafanyakazi wenzangu hawakuonyesha kunijali kwani muda wote walionekana kuwa na sura za ubize hata ilipokuwa ni muda wa mapumziko. Wala sikuwa na marafiki hata wa kunisaidia kunipa uzoefu zaidi lakini nilipambana kivyanguvyangu kuhakikisha natekeleza majukumu yangu ipasavyo.

Katika siku zangu zote za kuwepo kazini sikuwahi kumwona Boss mwenye kampuni wala kulisikia Jina lake likitajwa na mfanyakazi yoyote yule ila zaidi sana nilimfahamu tu! Mkurugenzi wa kampuni aliyeniajiri kwa makubaliano ya kula robo ya mshahara wangu wa kila mwezi.

Hatimaye Ikafika siku ya ijumaa ambayo ilikuwa ni ya tano tangu kuyaanza majukumu yangu. Walau vilindi vya moyo wangu vilifurahi kwa kudhani kwamba ningepata muda wa kulifuta jasho langu la wiki nzima katika siku za akiba za mwisho wa wiki.

Kazi ilikuwa ni ngumu na yenye kuchosha kutokana na pilikapilika kuwa nyingi mno. Ilipofika saa tisa alasiri nilianza kuona wafanyakazi wenzangu wakianza kuondoka makundi kwa makundi huku wengi wao wakiwa ni wanawake.

Nilizidi kujipa matumaini kwamba ulikuwa ni wasaa wa kwenda kuianza weekend na kujipumzisha. Licha ya matumaini yote niliyokuwa nayo lakini moyo wangu ulikuwa ukinienda mbio pasipo kujua sababu ilikuwa nini.

Sikujali sana kwani nilihisi ulikuwa ni uchovu tu wa majukumu. Yalifika majira ya saa kumi huku nami nikifanya hima kukamilisha majukumu niliyopewa ili niweze kuondoka kwenda nyumbani, maana nilisham-miss sana mke wangu niliyemuacha tangu Asubuhi.

Siku hiyo mkurugenzi alikuwa akipitapita na kufoka kila mara katika ofisi zetu zilizokuwa wazi kiasi cha kwamba nilikosa hata muda wa kujibu SMS za mke wangu. 

Wakati nikielekea katika tamati ya jukumu langu. Nilipata shaka na hofu kidogo kwa kuzidi kuona waliokuwa wakiruhusiwa kuondoka kwenda nyumbani walikuwa ni wanawake tu! na baadhi ya wafanyakazi wanaume waliokuwa wakimiliki magari.

Kwakuwa nilikuwa mgeni pale kazini hivyo nilikuwa sielewi utaratibu ulivyokuwa ukienda ikabidi nijitutumue na kumuuliza mfanyakazi mwenzangu aliyekuwa karibu yangu lakini sikupewa jibu lolote zaidi ya kutizamwa tu!.

Yule bwana alifahamika kwa Jina la kaoneka alinitazama usoni kwa masikitiko na kutikisa kichwa chake kisha akasema “ wewe piga kazi, pambania tonge lako” kisha akakaa kimya na kuendelea na majukumu yake.

Moyo wangu ulidunda sana huku nikizidi kumkumbuka mke wangu aliyekuwa ni mzuri na mwenye mvuto sana.

Nilifanikiwa kukamilisha jukumu nililopewa na muda huo ilikuwa ni saa kumi na mbili jioni. 

Ulisikika mlio wa dharura uliotutaka tukusanyike eneo la matangazo. Wote tulifika mara moja huku tukiwa na shauku ya kujua tulichokuwa tumeitiwa pale.

Haikupita dakika, akaja mwanamke mmoja mrembo lakini aliyekuwa amevalia uso wa chumvi ambaye ilisemekana alikuwa ni awara wa mkurugenzi na kutoa matangazo.

Hakuwa na salamu wala pongezi yoyote ya kazi tuliyofanya bali alianza moja kwa moja na matangazo yake.

“Kesho kila mmoja anatakiwa kuwepo hapa kuanzia saa moja Asubuhi kwani Boss mwenye kampuni atakuwepo na atakayekiuka lolote litamkuta” 

Mwanamke huyo aliondoka pindi tu! Alipokuwa amemaliza kutoa tangazo kwa lugha ya ukali na wala hakuna aliyemuhoji kwa lolote.

Nilijisikia hasira kutokana na uchovu niliokuwa nao. Na kila nilipowatazama wenzangu tuliokuwa nao hapo wengi wao walikuwa ni walala hoi wenzangu.

Niliondoka na kuelekea nyumbani, Mfukoni nilikuwa na noti ya Elfu tano nikapitia gengeni kwa ajili ya kununua mboga na kuendelea na safari yangu.

Nilipofika nyumbani mke wangu alinipokea kwa furaha sana na kuchukua kifuko kidogo nilichokibeba mkononi. Alinikumbatia na kunipiga mabusu licha ya jasho lililokuwa limekaukia mwilini mwangu.

Aliniandalia maji ya kuoga na kunisindikiza hadi bafuni akanisubiri nje hadi nilipomaliza kuoga kisha tukaongozana kuelekea ndani.

Mke wangu aliandaa chakula na kisha tukala kwa furaha. Hata baada ya kula alininawisha mikono na kunisihi tufanye sala ili tupumzike kwani kwa macho yake tu! aliona uzito wa uchovu niliokuwa nao.

Baada ya kumaliza kusali nilijilaza naye akalala juu ya kifua changu. Wakati huo nilifikiri kwamba angeweza kunihoji kwamba ni kwanini sikujibu SMS zake alizonitumia mchana nilipokuwa kazini.

Ilikuwa ni hofu yangu tu! Kwani mke wangu hakuuliza jambo lolote zaidi ya kunipa pole ya majukumu na kuniambia kwamba ananipenda sana.

Usingizi ulianza kunilemea nikajikuta nimelala bila hata ya kumjuza mke wangu kwamba kesho yake nilipaswa kwenda kazini.

Nililala na kulala wewe.. lakini ikawa ni majaliwa yangu kuiona siku mpya. Nilishtuka majira ya saa kumi na mbili Alfajiri baada ya kuota ndoto ya muda mrefu kwamba nilikuwa nimetajirika vilivyo na kuwa na pesa pamoja na mali nyingi.

Nilikurupuka na kukimbilia kwenye mfuko wa shati langu nililokuwa nimelitundika kwenye msumari nyuma ya mlango, nikaanza kulikagua kwani niliota nikiwa nimejaza kibunda cha noti za thamani katika mfuko wa shati hilo.

Looh! Ilikuwa ni ndoto tu! Sikuambulia chochote zaidi ya kuona mende akitimua mbio kutoka kwenye mfuko wa shati pamoja na kikaratasi kidogo nilichoandika namba ya simu ya mkurugenzi.

Wakati huo naye mke wangu alishtuka na kushangaa kwanini niliamka mapema wakati ilikuwa ni siku ya Jumamosi akiamini kwamba ilikuwa ni siku ya mapumziko.

“Habari za Asubuhi mume wangu”

“Salama mke wangu, umeamkaje”

“Nimeamka vizuri mume wangu”

“Mbona umeamka mapema sana, kwani unataka kwenda wapi?”

Sikuwa na budi kusogea mpaka katandani na kumueleza mke wangu kile tulichoamuriwa na awara wa mkurugenzi siku ya jana.

Mke wangu alishangaa sana na kunionea huruma sana. Machozi yalimlengalenga na kuhisi kama ajira yangu ilikuwa ni ngumu mno. Ikiwa hata na hivyo nilimficha juu ya makubaliano tuliyoafikiana Mimi na mkurugenzi ili kupata ajira.

Wakati nikitoka nje kwenda kuswaki, naye mke wangu aliamka na kuniandalia kifungua kinywa. 

Nilipomaliza maandalizi yangu, nikapata kifungua kinywa huku macho ya huzuni ya mke wangu yakinitazama usoni.

Nilikuwa nikisikitika ndani ya nafsi yangu kwani nilitambua moja kwa moja kwamba mke wangu alitamani muda wangu zaidi wa kuwa pamoja naye hasa ukizingatia ilikuwa ni weekend, lakini sikuwa na chaguo zaidi ya kutimiza agizo tulilopewa kwakuwa ajira hiyo ndo ilikuwa tegemeo la kuendesha maisha yetu.

Wakati nikimalizia kupata pafu la mwisho la kifungua kinywa changu, mara ghafla mke wangu alianza kulia kwa sauti huku akiwa amejishika tumbo lake.

“Mungu wangu” Mapigo ya moyo wangu yalinienda mbio nikaogopa sana kiasi cha kuachia kikombe kikaanguka chini. Sikujua ni kipi kilimkuta mke wangu maana hata hakuwa na ujauzito.

“Mke wangu, mke wangu, mke wangu” nilimwita kwa nguvu huku nikimtikisa tikisa kwa kuwa mara hii alikuwa ameanguka na kupoteza fahamu.

Nilizidi kuogopa sana, nikachota maji kidogo kwenye bakuli na kum-mwagia usoni huku nikimpepea na kuyafungua madirisha yote ili upepo upite. 

Baada ya kufanya hivyo nikaona hali ya mafanikio kwani mke wangu alijaribu kuyafungua macho yake ingawa yalikuwa malegevu.

Haraka, haraka nilimkagua mwili mzima kuona kama alipata majeraha yoyote wakati alipoanguka na sikuona jeraha lolote.

Hofu ilipungua kwa kiasi fulani na ghafla kumbukumbu zikanirejea kwamba nilipaswa kuwa maeneo ya kazini kwa muda huo. 

Kichwa changu hakikutulia, niliwaza kuhusu hali ya mke wangu lakini pia niliwaza kuhusu kazi yangu. 

Akili yangu ilitaabika sana kuwaza ni kipi cha kufanya, nikaona ajira haina thamani ya uhai wa maisha ya mke wangu.

Mlio wa alamu ya saa moja kamili ulisikika katika saa yangu ya mkonyezo iliyokuwa mkononi.

Hofu ikanipanda tena na kuwaza kuhusu ajira niliyoihangaikia kwa miaka tisa hadi kuipata. Sikuwa na moyo wa kiburi kwani nilitambua pia nikiikosa tena hiyo ajira nitazidi kutaabika sana mimi pamoja na mke wangu.

Nilichemsha maji ya vuguvugu nikachanganya sukari na chumvi kidogo kisha nikamnywesha mke wangu.

Matumaini yalirejea tena baada ya kumsikia akiliita Jina langu. Macho yetu ya huzuni yalitazamani lakini ghafla mke wangu aliachia tabasamu na kuzidi kunipa matumaini.

Pamoja na hali aliyokuwa nayo, aliwaza na kujali kuhusu mimi, alishatambua moja kwa moja kwamba nilikuwa na hofu ya kupoteza ajira yangu.

Alijikaza na kuniambia niende kazini lakini nilisita wala sikutaka kulisikia hilo. Nikakumbuka kwenye mfuko wa shati kulikuwa na karatasi niliyoandika namba ya mkurugenzi.

Niliihamishia kwenye simu na kumpigia lakini haikupokelewa.

Baada ya muda kidogo simu yangu iliita nikapokea na kutoa salamu, nilitambua ni namba ya mkurugenzi ikabidi nijitambulishe.

Nilipotaka tu! Kuanza kumueleza changamoto iliyonisibu na kuomba ruhusa mambo yalinibadilikia.

Bila ya hekima wala busara mkurugenzi alinifokea kwa hasira na kunikaripia huku akinitaka niwahi kazini la sivyo atanifukuza kazi.

Mke wangu alianza kutoa machozi baada ya kusikia maneno mabaya aliyonitolea Mkurugenzi.

Nilijisikia vibaya na wala sikujali kuhusu maneno yake, nilijikaza kiume na kwenda kwa mama mmoja jirani yangu kumuomba aniangalizie mke wangu ili niende kazini.

Mama huyo alikubali na sikuwa na budi kumuachia kiasi chote cha pesa kilichobaki kwenye elfu tano ya jana niliyonunulia mboga.

Nilirudi ndani nikamuaga mke wangu na kuondoka wepesi kuelekea kazini.

Licha ya uchovu ulionikumbatia, nilikimbia njia nzima hadi kufika kazini. Nilikuwa nimechelewa na jasho jingi lilinitoka.

Wakati huo wafanyakazi wenzangu walikuwa wameshayaanza majukumu yao.

Nilinyata kinyakimya na kuelekea kwenye eneo langu la kazi.

Baada tu! Ya kufungua mlango wa jengo la ofisi na kuingia ndani, nilimuona mkurugenzi akiwa amesimama na wageni watatu waliovalia suti.

Nilitambua kabisa katika jopo hilo palikuwa na Boss mwenye kampuni lakini sikuweza kumtambua kwani sikuwahi kuiona sura yake kabla hata japo kwa picha.

Kwa bahati mbaya, nilijikwaa na kuanguka, kishindo kilisikika. Mkurugenzi na wale wageni walishtuka na kunitazama hata hivyo hawakunitilia maanani sana wakaendelea na ratiba zao.

Nilikuwa na hofu sana na kuona kwamba nilikuwa na asilimia chache za kuilinda ajira yangu.

Nilijua fika kwamba mkurugenzi alitambua kwamba ndo nilifika kazini kwa muda huo wakati Maboss zangu wote walikwishakufika.

Nilifika kwenye ofisi yangu, nikawasha kompyuta yangu na kuanza majukumu. 

Sikumaliza hata dakika tano mara ghafla! tukasikia mlio wa alamu ya dharura ukituhitaji kwenda eneo la ukumbi wa vikao na matangazo.

Bila ya kupoteza muda wote tulifika mara moja, na mara baada ya salamu kutoka kwa mkurugenzi. Alimtambulisha Boss mwenye kampuni.

Hakukuwa na mambo mengi. Kila mmoja alaamriwa kutawanyika na kwenda kufanya majukumu yake kwa ukamilifu.

Mkurugenzi alinitaka nionane naye kabla ya kuelekea kwenye eneo langu la kazi. Nilihofu sana na nikajua nilikuwa naenda kufukuzwa kazi.

Mkurugenzi alianza kunifokea tena na wala hakutaka kunipa hata dakika ya kunisikiliza. Aliniambia kwamba Boss hakufurahishwa na kile kitendo changu cha kuchelewa kufika kazini hivyo alinipa onyo kali na kuniamuru niondoke.

Sikutaka kujali ingawa roho iliniuma. Niliona kama yote yalikuwa ni makosa yangu ingawa haikuwa hivyo kwani hakutaka kunisikiliza kabisa. nikaondoka na kurudi kwenye eneo langu la kazi.

Nilizidi kuwaza kuhusu kazi lakini pia nilimuwaza sana mke wangu hasa nilipokumbuka hali niliyomwacha nayo nyumbani.

Niliendelea na majukumu yangu, kazi ilikuwa ni ngumu sana siku hiyo hakukuwa na muda mwingi wa kupumzika. 

Kichwa kiliniuma sana lakini sikuwa na budi kujikaza nikawaza muda wa mapumziko nitafanya juu chini niwasiliane na mke wangu.

Ilikuwa ni ngumu sana kupata wasaa huo tofauti na nilivyofikiri mwanzoni kwani Mkurugenzi alikuwa akituharakisha hata ilipofika muda wa kula.

Baada ya mapumziko na kupata chakula cha mchana tulirejea kwenye majukumu. Nilihisi kuchoka sana na maumivu ya mwili mzima. Kichwa kilizidi kuniuma na kuanza kupata usingizi.

Ilikuwa ni siku mbaya sana kazini. Licha ya kujikaza kwa muda mrefu.

Yalipofika majira ya saa nane na nusu wafanyakazi wengi walianza kusinzia na wakati huo Boss alikuwa akipita kwenye kila ofisi.

Mimi sikuwa na taarifa yoyote muda huo niliona niutumie haraka haraka kuwasiliana na mke wangu.

Wakati nikifanya hayo kumbe Boss alikuwa nje ya ofisi yangu na kunisikiliza ingawa hakuweza kuelewa nilichokuwa nikiongea na mke wangu.

Naye alisogea pembeni na kufanya mnawasiliano na mkurugenzi kwa muda huo pasipo mimi kufahamu.

Punde kidogo nikiwa bado nawasiliana na mke wangu, simu ya ofisini kutoka kwa Mkurugenzi iliita.

Sikujali kuhusu simu yake nikaendelea na muzungumzo baina yangu na mke wangu.

Nilipata wazo la kuelekea uwani ili nipate kisingizio cha kutokupokea simu ya mkurugenzi kwa wakati huo.

Looh! Kumbe ni kama nilikuwa nikijitengeneze shimo ili nizame kwani wakati natoka nje nilikumbana na Boss akiwa nje ya ofisi yangu kisha akacheka na kuniambia “Hongera kwa kazi nzuri”

Nilishindwa hata kuitikia na Mapigo ya moyo yakaanza kunienda mbio kwa mara nyingine. Haja ndogo ilinibana ghafla ingawa nia yangu ilikuwa ni kwenda uwani ili kuzuga tu! Na kupata kisingizio cha kutokupokea simu ya Mkurugenzi.

Baada ya kutoka uwani nilimkuta Boss ndani ya ofisi yangu huku akiniangalia kwa macho ya hasira. Mara hii ndo nilijua kabisa sikuwa na bahati yoyote zaidi ya kwenda kufukuzwa kazi.

Nilishikilia simu yangu mkononi na baada ya muda mfupi nilijikuta nikiwa nimeiweka mezani na kwenye screen kulikuwa na picha ya mke wangu.

Nilisali kimoyomoyo na kujiombea nisipoteze ajira yangu huku wakati huo Boss alikuwa akiitazama sana ile picha ya mke wangu kwenye simu na kisha akanena.

“Hivi unaipenda ajira yako?”

“Ndiyo Boss.”

“ Sawa, hiyo picha kwenye simu yako niya nani?”

“Ni picha ya mke wangu Boss”

Baada ya tu! Ya kutoa jibu langu la mwisho. Ghafla Boss alitabasamu na kuonyesha uso wa furaha, aliniambia niendelee na majukumu yangu kisha akatoka nje.

Nilistaajabu sana kwani sikutegemea jambo kama hilo tofauti na kuwazia kufukuzwa kazi. Lakini baadae nilitafakari tena na kuanza kujipa maswali kwamba kwanini Boss atabasamu na kuonekana kubadili maamuzi yake baada ya kumwambia ile picha ilikuwa niya mke wangu.

Itaendelea….

By Sebastian s. Masabha.