PENZI LA NYOTA TANO                        

 ️       ❤️   

      ⭐️⭐️⭐️⭐️⭐️                         

A~story by Sebastian S. Masabha              +255 (0755-201677) 

Sehemu ya 01

Haya jamani muwe na siku njema wapendwa” Ilikuwa ni siku ya Jumapili majira ya saa sita mchana hivi, John aliagana na vijana wenzake Erick, Jennifa pamoja na Prisca waliokuwa wakitoka Ibadani kutimiza amri ya sita katika zile amri kumi za Mungu huku kila mmoja akishika njia yake na kurejea nyumbani. 


John kijana mwerevu tena mtanashati na mpenda maendeleo alifika nyumbani kwake baada ya dakika chache za kutembea njiani.

 Mbele yake karibu na mlango wa kuingia ndani aliona bahasha ya kawaida ambayo kwa haraka haraka hakuweza kufahamu ilikuwa na kitu gani ndani yake. 
Bila ya kusita John aliiokota ile bahasha na kuifungua kwa shauku kubwa sana na kukutana na barua iliyokuwa imepambwa kwa michoro ya maua pamoja na makopa kopa huku ikisindikizwa na jumbe nzuri za kimahaba zilizomfanya John aweke Biblia chini na kuitilia maanani ile barua.
“ Ajabu kweli huyu ni nani aliyefanya hivi?” Alijisemea huku macho yakimtoka.

John alionyeshwa kushangazwa na ile barua kwani baada ya kuisoma kwa umakini alitambua ya kuwa ule ulikuwa ni mwandiko wake na ile barua aliiandika yeye mwenyewe miaka kadhaa nyuma lakini hakuweza kumkumbuka mhusika aliyempatia ile barua.

John alifungua mlango na kuingia ndani huku akitafakari juu ya mtu aliyeweza kuifikisha ile barua nyumbani kwake bila ya yeye kuwa na kumbumbuku nzuri zaidi ya kuutambua mwandiko wake.
 
“Atakuwa ni Hilda, Phinner ama Doreen lakini hapana wamewezaje kupajua kwangu hadi kufanya kitendo kama hiki?” John alijiuliza sana.

Alitumia muda mwingi kufikiri zaidi kipindi alichokuwa akisoma kidato cha tano na cha sita na kuzirejesha kumbukumbu zake hasa kwa wale aliokuwa na ukaribu nao ili walau kujaribu kumkumbuka mhusika aliyempatia ile barua lakini ilikuwa ni ngumu kwake kukumbuka.

Jambo hili lilimuumiza kichwa na kuwa kama mtihani kwake alioshindwa kuupatia majibu kwa uwepesi, ikabidi ampigie simu rafiki yake wa karibu na kumualika nyumbani.

Rafiki wa karibu wa John alikuwa ni Hillary mtu ambaye walifahamiana kwa muda mrefu na kudumu katika urafiki wao uliopitia katika milima na mabonde.


Hillary aliwasili haraka sana nyumbani kwa John na kuingia ndani moja kwa moja huku akimkuta John ameshika tama na kujiegemeza kwenye kochi.


“Vipi ndugu yangu unaumwa au?”
Hillary aliuliza huku akiwa na wasiwasi.
“Hapana kaka”
“Nini hasa maana simu yako imenishtua”
“Kuna mambo tu siyaelewi elewi hapa nyumbani”
“Eeh.!! Nini hicho” Hillary alizidi kuuliza huku akiangaza kulia na kushoto”

John hakuwa na budi kumsimulia Hillary mambo aliyoyakuta pindi tu alipotoka kanisani na kufika nyumbani kwake.

“Hahaa…” Hillary alicheka.
“Unacheka nini sasa? hili limekuwa jambo la kuchekana tena!”
“ Linachekesha maana mimi nilidhani ni jambo la kutisha kumbe ni jambo dogo tu! Kiasi hicho”

“ Kwa hiyo ushamjua ni nani aliyefanya hivi?” 

“ Sasa mimi nitajuaje na wakati wewe ndo ulikuwa mgawa barua, tena kisirisiri mpaka umemsahau na mhusika uliyempatia”

Mazungumzo baina ya wawili hao yaliendelea huku Hillary akionekana kuwa mtu wa masihara mengi kitu ambacho kiliwafanya washindwe kupata ufumbuzi na kuamua kupotezea jambo lenyewe kisha Hillary akaondoka na kurudi nyumbani kwake.

**************************************
Wakati Hillary alipokuwa akirejea nyumbani kwake, njiani aliwaona wasichana wawili wakiwa wamesimama na kuwa na mazungumzo ya muda mrefu kwani pia aliwapita sehemu hiyo mara ya kwanza alipokuwa akielekea kwa John.
Aliwaza pengine labda apite njia nyingine lakini ghafla alibadili mawazo yake na kuelekea katika njia ileile huku akitembea kwa kunyata kuwasogelea wale wasichana.

Hillary aliwasogelea kwa ukaribu pasipo ya wale wasichana kuelewa jambo lolote kwani mazungumzo yao yalikuwa yamewanogea vilivyo

***************************************
Alitoa simu yake na kuiweka sikioni mithili ya mtu aliyekuwa akifanya mawasiliano bila ya kutoa sauti, ilhali masikio yake yalikuwa makini katika kusikiliza mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea baina ya wasichana hao.

“ Kwa hiyo unanishaurije shoga yangu maana ndo nimeshampenda hivyo” Prisca alizungumza.
“ Sijui hata nikushaurije shoga yangu maana yule jamaa ni kiboko ya warembo”

“Jamani Jennifa mbona unanivunja moyo no rafiki yangu”

“Mmh.. Nop, Siyo kwamba nakuvunja moyo ila ndo ukweli shoga yangu mimi nakuonea huruma usije ukazama alafu ukaishia kuteseka
“ Jamani shogaa.. wewe nipe tu! Mbinu ya kumpata maana hayo mengine wala sijali, alafu! mbona anaonekana ni mtu mstaarabu sana” Prisca alizidi kusisitiza.“ Yaani kiukweli nashindwa nianzie wapi shoga yangu maana nakuonea huruma si unajua ninagyokupenda eeh.. sitaki uteseke”
“ Sawa nimekuelewa basi nisaidie namba zake”
“ Hata namba zake mwenyewe sina shogaa” 

Baada ya Hillary kusikiliza kwa muda mrefu maongezi ya Jennifa na Prisca ilimbidi ajikoholeshe na kujifanya akiendelea na zoezi lake la kupiga simu huku mara hii akitoa sauti na kujifanya akiongea na mzungu.


Jennifa na Prisca walishtuka ingawa hawakujua kwamba Hillary alikuwa akiwasikiliza kwa muda mrefu.


Kwa hofu walianza kuondoka, lakini Hillary hakusita kuwasubirisha tena kwa kuwasemesha na kuachana na maongezi yake hewa ya simu.

 

“ Hello, Habari warembo”
“ Hi… Broh!” Jennifa alidakia.
“Pumbavu kabisa, mimi ni Broh! Wako” Hillary alijisemea kimoyomoyo na kuendelea na majibizano.
“ Samahani naomba kuwauliza, hivi hii njia ukinyooka nayo inaelekea mpaka wapi?” 
“ Inaelekea moja kwa moja mpaka sheli” Jennifa alidakia tena.
“ Mbona kama anakiherehere sana huyu dada” Hillary alijisemea tena kimoyomoyo.
“ Haya asanteni sana, mbarikiwe wapendwa”
“ Sawa na wewe pia”

Hillary alianza kuondoka lakini moyo wake ulijawa na dukuduku kubwa sana hasa alipokuwa akizungumza na kumtazama Prisca ingawa maswali yote aliyouliza yalijibiwa na Jennifa.
Alitembea kidogo akahisi moyo wake unafanya miguu iwe mizito kwenda mbele, ikambidi awageukie wale wadada waliokwisha kusogea kwa umbali fulani na kupaza sauti yake.

“ Hello, ladies” ikawa kimya.
“ Jamani nyie wapendwa” Hillary aliita tena naye Jennifa alisikia lakini akajikausha.
“ Hello, nyie warembo” Hillary hakuchoka kuita.

Looh! Mungu si athumani, juhudi za Hillary za kutapatapa kupiga kelele zilionyesha uhai baada ya Kisikika na Prisca na Kumfanya ageuze shingo na mwili wake nyuma, tena kwa madaha.

Kitendo cha Prisca kugeuka nyuma na kumtazama Hillary, kilimkera Jennifa ambaye hakutaka kuendelea kumsubiri Hillary. Kwa gubu na hasira alimvuta mkono Prisca kisha wakaondoka na kumwacha Hillary akiwa amesimama njiani kwa kuduwaa pasipo kuelewa tatizo lilikuwa ni lipi baina yao.

Itaendelea…