Facebook

Pesa za Shemeji

SEHEMU YA KWANZA 01.

Ilikuwa yapata majira ya saa moja kasoro jioni, Ambapo ilisikika sauti mithili ya mtu aliyekuwa akitafakari na kujihoji mwenyewe juu ya jambo fulani huku akisema “Zey..zey..! Aah! Kumbe ndo binti yule mrembo ama kweli wapo walioumbwa wakaumbika” Sauti hiyo ilikuwa ikitaja jina la msichana aliyeonekana kuwa mrembo sana pasipo kulimalizia kiasi cha kufananishwa na mtu mwenye ukakasi katika ulimi wake na mwenye kigugumizi kikali. Huyu alikuwa ni France Meneja mkuu wa moja ya Five star hotel “HYATT REGENCY. The Kilimanjaro Hotel” ya Jijini Dar-es salaam. Pia alikuwa ni kijana mcheshi wa makamo hivi, mtanashati sana na aliyeishi maisha ya kifahari. Kwani mbali na kuwa na nafasi ya umeneje mkuu pale Hyatt Regency. Alikuwa na miradi mbalimbali na mmiliki wa nyumba tatu kubwa ikiwemo moja ya ghorofa ambayo ndiyo aliyokuwa akiishi ndani ya eneo la Oyster bay. Sambamba na hilo ua wa nyumba yake ulipambwa na magari ya kifahari kama vile Range Rover, Land cruiser Vx V8 na Toyota Harrier New model. Kwa ufupi alikuwa ni mtu aliyejikamilisha kwa kina na aliyeishi maisha ambayo vijana wengi wa kisasa wangetamani kuyaishi. Basi kutokana na uchovu wa majukumu ya kiofisi aliyokuwa akiyatekeleza kila siku, yalimfanya ajitupe kitandani na baada ya mda mfupi alichukuliwa na usingizi mzito uliomfanya aote ndoto sukari usiku wa manane kiasi kwamba alihamishwa katika dunia nyingine. Hatimaye palipambazuka na aliamshwa kutoka kwenye wimbi kubwa la usingizini na mwanga wa jua uliokuwa ukimulika upande wa dirisha lake. “Ahaah! Kumbe kumekwisha kucha” alijisemea France. Alichukua mswaki wake akaweka dawa kisha akautia kinywani mwake na kufunga taulo lake akaelekea bafuni. Wakati akiendelea kuswaki kunako sinki alielekeza macho yake yalioonekana kuwa na dalili za ugairi katika kioo kilichokuwa sehemu ya juu ya sinki. Na hali hii ilitokana na mwanga wa taa uliokuwa ukionekana katika kioo hicho. Baada ya kumaliza kuswaki alifungua taulo na kuliweka kando kisha akaitanguliza miguu ndani ya bafu lake la kukaa (sitting bathroom) lililokuwa na mng’ao wa kupendeza wa rangi ya dhahabu. Alifungua koki zote mbili zilizokuwa zikitolea maji moto na maji yenye ubaridi na kuanza kusafisha sehemu zake za mwili. Wakati akiendelea na zoezi hilo ghafla zilimvaa kumbukumbu na taswira za yule mwanamke aliyekuwa akimtaja kwa kigugumizi “Zey, Zey” mapema ya usiku wa jana. Lakini alitikisa kichwa kulia na kushoto kuashiria kutokubaliana na hali ile. Mara akakurumuka katika maji mithili ya mbwa aliyechomoka salama katikati ya kundi la wahehe. Looh! Jambo lile lilionyesha ishara yakuwa France alishanza kuzidiwa na uzito wa mawazo ya mara kwa mara juu ya mtu fulani aliyehisi kuanza kuzama kwake taratibu kihisia na kumpenda. Baada ya kutoka bafuni aliingia ndani ya chumba chake kilichokuwa na mahadhi ya kifalme na kuanza kuvaa nguo kwa ajili ya kuelekea kazini. Siku hiyo alivalia suti yake ya rangi ya Dark blue  iliyonyongewa na tai ya rangi nyeusi yenye vidotidoti vyeupe na chini aligongelea moka ya rangi ya maroon iliyowakaka kama ngozi ya chatu. Looh! Mitupio na mikato hiyo ya kipapaa ndiyo moja ya sababu ya vitu vilivyompa heshima kubwa na kupendwa na watu wengi wakiwemo wafanyakazi wenzake. Punde baada ya zoezi hilo France alipulizia perfume ya Mirace katika pande zake mbili za kwapa na hapo akawa na imani ya kujiridhisha kwamba yuko tayari kwa ajili ya kuelekea ofisini. Kuja kutizama katika saa yake ilikuwa imekwisha kutimia majira ya saa mbili 8:00 am asubuhi akashtuka kidogo na kujisemea Aghaa! “Kumbe muda umeshasogea kiasi chake hivi acha niwahi kwenye kula yangu” kisha akaachia tabasamu lake lenye uwezo wa kumshibisha mwanamke yoyote mwenye njaa kali ya kutokuwa na furaha. Alielekea nje kutoka ndani ya mjengo wake wa thamani na kuyatupia macho moja kwa moja katika gari zake kisha baada ya sekunde chache akawa amekwisha kupata majibu ya kwamba na gari lipi lingemfaha zaidi katika shughuli zake za siku hiyo. Alichagua gari lake la land cruiser Vx V8 na ambalo alionekana kulipenda zaidi maana ndilo alilokuwa akilitumia mara kwa mara. Akapanda ndani ya chuma cha Mjapani na kisha safari ya kuelekea kazini kwake ikaanza. Wakati akiwa njiani alikuwa akiyashibisha masikio yake kwa ladha tamu ya mziki asali wenye mahadhi ya kimambele. Ilimchukua takribani muda wa nusu saa hivi kuwasili katika eneo lake la kazi na hapo ilikwishakutimia majira ya saa mbili na dakika thelathini na tano 8:35 am asubuhi. Mara tu baada ya kushuka katika gari lake akapokelewa na sauti iliyosikika “Hello! Boss France” Akaitikia “Hello” kisha kimya cha muda kidogo kikatawala baina ya wawili hao. Sauti hiyo ilikuwa ni nyororo sana na tamu zaidi katika masikio ya Boss France kiasi cha kwamba ingeweza kutumika kama Bank Card ya kuchomolea rundo la pesa katika mashine ya ATM. Bila shaka sauti hiyo ilikuwa niya mmoja wa wafanyakazi wenzake katika Hotel hiyo ya Hyatt Regency na aliyetambulika kwa jina la Vicky. Vicky alikuwa ndiye mhasibu mkuu katika Hotel hiyo na pia alikuwa na msichana mrembo na mcheshi wa aina yake. Baada ya salamu ile Boss France alianza kupiga hatua kwa mwendo wa madaha na kuelekea ndani ya lift iliyompeleka moja kwa moja karibu na ofisi yake. Alifungua mlango na kuingia ndani ya ofisi kisha akavua koti lake la suti na kuwasha Air condition A/C iliyotoa upepo wenye ubaridi mwanana. Aliketi katika kiti chake cha kuzunguka na kujizungusha mizungusho miwili huku akigonganisha vidole vyake viwili na kutikisa kichwa chake upande wa kulia na kushoto. Baada ya kufanya zoezi hilo kwa muda mchache Ghafla simu yake ya mkononi ikaita naye alisita kuipokea na mara baada ya kukata ikaita kwa mara ya pili na Boss Fance akajisemea “Huyu atakuwa ni Fausta mpenda mizinga” lakini baada ya kuitoa aliona namba ngeni na kuipokea Looh! Boss France alizizima ghafla na kuganda kwa mshangao ulioonekana katika uso wake mithili ya mtu aliyepigwa na butwaa zito, kwani sauti ile ilikuwa ikifanana na sauti ya mrembo aliyehisi kuanza kumtawala katika mawazo yake. La hasha! Sauti hiyo ilikuwa tamu zaidi na yenye ladha ya aina yake kwani ilipenya mpaka kwenye mishipa ya visigino vya Boss France. Ilikuwa ikisema Hello! Big Boss naomba leo tuonane kwa ajili ya maongezi muhimu sana kama hautojali kisha simu ikakata ghafla. Wakati huo Boss france alikwisha shikwa na kimuhemuhe cha kutaka kujua ile ilikuwa ni sauti ya nani na wangekutana wapi na kwa muda gani lakini ikashindikana kwa muda huo kwani aliponyanyua simu yake na kuipigia namba ile alipokelewa na majibu ya wahudumu wa voda “Namba unayoipigia haipatikani kwa sasa tafadhali jaribu tena baadae”...............................

Mwisho wa sehemu ya kwanza.

Je nini kitakachoendelea baada ya Boss France kubahatika kuipigia namba ile na kupokelewa na mhusika?

 Endelea kufuatilia mwendelezo wa tamthiliya hii katika sehemu ya pili 

Mwandishi: Sebastian Masaba.
Mawasiliano 
Phone: 0746445197
            0758162527





Post a Comment

0 Comments