Ilikuwa ni jioni majira ambayo jua lilionekana kuelekea
kuchwea, upepo nao ulivuma kwa kasi huku
ngurumo za radi nazo zikisikika kwa mpasua mkubwa. Kiza totoro kilianza kutanda
na mwanga wa radi uliosambaa na kumulika uligubika katika kijiji cha Korona.
Matone membamba na mepesi yaliyofuata mwelekeo wa upepo mkali nayo yalianza
kushuka ndani ya Kijiji cha Korona.
Siku hiyo ilikuwa ni siku ya tofauti ndani ya kijiji cha
korona kwani hapakusikika mtu wala kitu chochote tofauti na ngurumo za radi
zilizokuwa zikipasua mibuyu na mpingo hapo Kijijini. Baada ya muda kidogo mvua
ilizidi kuongezeka na kunyesha kwa kiasi kikubwa hali ambayo ilipelekea kujaa
kwa mto Yambwa, mto uliokuwa mkubwa na
maarufu sana hapo kijijini.
Ndani ya nyumba ya mzee Magoti ukimya ulitawala kwa kiasi
cha kukidhia, Familia ya mzee magoti ilikuwa ni familia ya wake wawili pamoja watoto
tisa. Ilikuwa ni moja ya familia maarufu sana na iliyoheshimika kwa upekee wake
ndani ya kijiji cha korona. Mzee magoti alikuwa ni mzee Mcheshi na mchangamfu
kwa kila mtu hapo kijijini na umaarufu wake ulitokana na busara, hekima na uwezo wake mkubwa wa kumiliki mali
nyingi na zenye thamani hapo Kijijini. kwani alikuwa akimiliki Ng'ombe wengi si
chini ya Elfu tatu pamoja na Mashine za kusagia mahindi, mtama na mashine ya
kukuboa ngano na mpunga.
Umaarufu na sifa kidekede alizokuwa nazo Mzee Magoti
hazikuishia hapo kwani alikuwa ni Mzee ambaye pia alimiliki mashamba makubwa ya
mikonge, karanga, mahindi miwa na michungwa yaliyokuwa yakizidi kumuweka karibu
na watu wengi hasa wasiojiweza hapo kijijini. Katika kijiji cha korona palikuwa
na tatizo moja kubwa la uvamizi na uwizi wa mali kama vile mifugo na mazao
lililokuwa likifanyika na watu wa vijiji vya jirani suala ambalo lilichangia
kuleta maafa mengi na kuwarudisha nyuma kimaendeleo watu wengi sana hapo
kijijini.
Lakini ilikuwa ni ngumu sana kwa mzee Magoti kukubwa na
hujuma hizo kwani alikuwa na ulinzi mkali na mkubwa wa mbwa wengi pamoja na
ulinzi wa kijadi. Hali ya ngurumo na mwanga wa radi iliyochanganya na mvua
kubwa bado iliendelea kufanya ukimya kwa watu wengi hapo kijijini. Ghafla! kwa
mbali zilisikika kelele za watu waliokuwa wakiashiria kuomba msaada. Alikuwa ni
Kijana zahera mtoto mdogo nawa mwisho wa Zuena mke wa kwanza wa Mzee magoti
aliyeweza kuwa wa kwanza kusikia sauti hizo kwa wakati huo.
Sauti hizo zilimshtua sana na kumfanya azidi kuogopa kwani
mapigo yake ya moyo yalimwenda mbio sana na kumfanya azidi kukumbatia shuka.
Sauti hizo ziliendelea kusikika tena kiasi kwamba hata naye mijanja mtoto
mkubwa wa zuena alikuwa akizisikia kwa mbali. Zahera alishindwa kuendendelea
kuvumilia akakurupuka na kukimbilia katika chumba walichokuwa wakilala wazazi
wake “ngo, ngo, ngo. ngo, ngo, ngo.” Aligonga mlango kwa
nguvu huku akihema kwa uwoga “nani wewe?” mzee magoti mwenye kibezi kizito cha kumtoa chura
matopeni aliuliza “Baba, baba ni mimi zahera kuna shida huku”
na papo hapo mzee Magoti alishtuka sana na kutoka nje akiwa na panga mkononi huku
taulo lake jeupe likiwa kiunoni. Alijitia ujasiri huku akionekana kuwa na
kimuhemuhe cha kutaka kujua ni nini kilichotokea.
Wakati huo mzee Magoti alimuona mwanaye akiwa katika hali
ya uoga sana na kabla hajaendelea kuhoji juu ya jambo lolote, ghafla mwanga mkali mweupe ulimulika na
uliofuatiwa na ngurumo kubwa ya radi na kumfanya mzee Magoti ajikute yumo chini
ya uvungu wa kitanda chake bila ya kujali alimuacha wapi mwanaye Zahera kwa
wakati huo. Alijimudu ndani ya sekunde chache na kutoka chini ya uvungu haraka
haraka kisha akaelekea tena nje ya chumba chake na mara hii alikuwa amebeba panga
pamoja na rungu kubwa. Zuena ambaye ni mke mkubwa wa mzee Magoti naye alishtuka
kutoka katika usingizi mzito ingawa tukio lile lilikuwa limeshampita na usiweze
kufahamu juu ya chochote kilichotokea kwa wakati huo.
Mzee Magoti naye alielekea katika chumba alalacho mwanaye
Zahera huku akitoa sauti ya chini chini tena iliyogubikwa na uoga kwa kuita “Zahera,
zahera, mwanagu huko wap..?” “Niko huku Baba” Wakati
Zahera akiyasema hayo kwa Baba yake mara ghafla zikasikika tena zile sauti
zilizikuwa zikiashiria kuomba msaada kwa mara ya tatu. Mzee Magoti hukuwa na
budi kuanza kunyata taratibu huku akielekeza nyayo zake kwenye chumba cha
mwanae mkubwa Mijanja. Mijanja alikuwa ni kijana jasiri na shupavu ambaye mara
kadhaa alikuwa akifanya matukio ya kishujaa yaliyowaacha vinywa wazi wanakijiji
wa kijiji cha Korona kwani umahiri wake na ujuzi wake wa kutumia mkuki, pinde za
mishale pamoja na kucheza na panga ulimpa umaarufu na kuzidi kuifanya familia
ya Mzee Magoti kuwa almasi ndani ya kijiji cha Korona.
“Ngo, ngo, ngo Mijanja... Mijanja” mzee Magoti
aliugonga mlango wa chumba cha kijana wake kwa nguvu huku akiita mara
mbilimbili kwa lengo la kutaka kupata msaada wa haraka. “Naam Baba kuna
jambo gani tena usiku huu mbona kijeshi namna hii” aliuliza mijanja
ambaye naye hakuonyesha kama alikuwa katika hali ya usingizi. “Kuna
kelele za watu zimesikika upande wa mto yambwa zikihitaji msaada” alijibu
haraka haraka mzee Magoti. “Ahaah! Hata mimi pia nimebahatika kuzisikia na
tena si mara moja ijapokuwa sikupata jibu la nini chakufanya” alisema
Mijanja ambaye alikuwa akifungua mlango wa chumba chake huku akiwa amebeba Kurunzi
yenye mwanga mkali, upinde mgongoni pamoja na podo iliyotiliwa mishale kadhaa.
Walifanya himahima kuanza kuelekea katika eneo la mto yambwa na hapo Mzee
Magoti hakuweza kuwa na wasi kwani kiburi cha tambo na ujasiri kilimjaa
kutokana na uwepo wa mwanae mwenye hadhi ya tuzo manuwari za kishujaa.
Wakati wakielekea katika mto yambwa Mtoto Zahera naye
aliyeamriwa kubaki nyumbani alikuwa akiwafuatilia kwa nyuma licha ya kujali
udogo wake pamoja na giza nene lililokuwa limetanda siku hiyo. Ilikuwa ni ngumu
kwa Mzee Magoti pamoja na mwanaye mijanja kuweza kutambua yakwamba kijana
Zahera alikuwa akiambatana nao kisirisiri. Njiani palikuwa kimya sana, kwani
ulikuwa ni mwendo wa mguu na njia, baridi nayo ilikolea katika miili yao kiasi
cha kufanya hata mikono yao kuhisi ganzi nayo makundi ya bundi waliokuwa
wametanda katika miti mbalimbali walikuwa wakiimba ukuti ukuti kwa ngurumo zao.
Walipoukaribia mto yambwa kwa mbele kidogo walibahatika kuona mwanga wa tochi
uliokuwa ukiangaza huku na kule, ikiwa ni ishara tosha yakwambwa palikuwa na
kundi la watu wachache waliokuwa wakiangazia juu ya jambo fulani. Mzee Magoti
na mwanaye Mijanja walijibanza pembezoni mwa mti mrefu naye mijanja aliokota
kipande cha jiwe na kukirusha kuelekea kwenye lile kundi la watu. Ebooh!
Kundi lile lililokuwa na watu watatu walioshindwa kujulikana walikimbilia na
kutokomea upande mwingine wa mto yambwa.
Waliendelea kusogea kwa ukaribu zaidi na mto yambwa
wakazunguka huku na kule wakati huo Mijanja aliliwasha kurunzi lake lililokuwa
likiachia mwanga mkali uliokuwa na uwezo na kummulika mnyama jamii ya simba na
kumfanya azimie kwa muda kutokana na ukali na wanga huo. Mara ghafla Zahera aliyekuwa
akiwafuatilia kwa nyuma alipiga kelele yenye mshtuko iliyoweza kuwashtua na
kutaka kumfanya Mzee Magoti atoke mafuta kukimbilia mtoni.
Mijanja aligeuka kwa ujasiri na kutaka kuanza kufoka kwa
hasira kwa uwepo wa Zahera katika tukio lile hatarishi. Lakini kabla ya kutaka
kufanya hivyo alimuona mtu aliyekuwa amelala chini huku akionyesha kuwa na hali
mbaya ya kuzidiwa. “Baba Baba kuna mtu hapa” aliongea Mijanja
huku akipiga magoti yake chini na kuanza kuanza kutoa msaada wa haraka haraka kwa
mtu yule. Alipomchunguza vizuri aligundua yakuwa mtu yule alikuwa niwa jinsia
ya kike. Looh! Mapigo ya moyo yalimwenda mbio mijanja kwa kuhisi huruma juu ya yule
msichana na asiwezejua ni kipi kilichokuwa kimemkuta. Kulingana na hali
aliyokuwa nayo msichana huyo Minjanja hakuwa na budi kumsaidia kwa namna yoyote
ili kuhakikisha anafanikiwa kuinusuru roho yake. Aliupeleka mkono wake wa kulia
na kuanza kumpapasa yule msichana. na kwambali aliweza kuyasikia mapigo ya moyo
ya yule msichana yakidundadunda. Looh! Aligundua yakuwa alikuwa
bado ni mzima. Mijanja alimsogelea msichana yule kwa ukaribu zaidi na kuelekeza
midomo yake katika pua na kuanza kuvuta na kumpulizia pumzi kwa haraka haraka
huku akiyasikilizia mapigo ya moyo ya msichana huyo aliyeonyesha kupigwa na
maji mengi yaliyomzidi uwezo.
Mijanja aliendelea kufanya hivyo kwa muda na mara hii
alimvika msichana yule koti alilokuwa amelivaa na kumkubatia kwa kumganda kama ruba ili aweze
kumpatia joto katika mwili wake.
Ilichukua mda
kidogo kwa msichana huyo ambaye hawakuweza kumfahamu kuanza kukohoa kama mtu
aliyepaliwa na maji yaliyoingia katika koo la hewa. Mijanja alitazamana na Baba
yake Mzee Magoti huku kila mmoja akiachilia tabasamu lililoonyesha dalili za
ushindi juu ya tukio lile. Nazo radi zilizokuwa zikitoa mwanga mkali
ziliendelea kunguruma kwa sauti kubwa na kukituliza tuli kijiji cha Korona. Mijanjaa
alimnyanyua yule msichana na kumweka juu ya bega lake kisha wakaanza safari ya
kuelekea nyumbani kwa Mzee Magoti.
Safari hiyo ilionekana kuwa ndefu kutokana na baridi
iliyokuwa ikizidi kupuliza. Mzee Magoti hakutaka kukaa mbele wala nyuma na hii
ni kutokana na tabia yake ya uoga uliopitiliza kiasi cha kwamba alizidiwa mbinu
na mwanaye Zahera aliyeonekana kuwa shupavu licha ya udogo wake.
Hatimaye baada ya safari kuwa ni hatua walifika ndani ya
boma la mzee Magoti huku wakiwa wametepeta kwa baridi kali. Mijanjaa
alimuingiza msichana yule katika moja ya chumba kilichokuwa hakitumiki kisha
akamlaza kitandani na kumfunika kwa blangeti zito. Mwili wa msichana yule
ulikuwa ukitetemeka sana mithili ya genereta lililokuwa limepungukiwa mafuta. Mijanja
alionekana kuwa mwingi wa huruma na mwenye huzuni kila alipokuwa akimtazama
msichana yule hata naye Zahera kijana mdogo jasiri alikuwa mwenye kujawa na uso
wa huzuni.
Wakati huo mzee Magoti aliyekuwa ni mwingi wa uchovu
alielekea kulala katika chumba chake, Mtoto zahera alijilaza pembeni ya msichana
yule na kupitiwa na usingizi mzito. Mijanja naye alionyesha kuchoka na kuhisi
maumivu mabegani mwake kutokana kazi kubwa aliyoifanya ya kumbeba yule msichana
kutokea mto yambwa. Baada ya kitambo kidogo alijisogeza karibu na msichana yule
kisha akambusu katika paji lake la uso na kuelekea chumbani kwake kulala.
Majira yalikwenda na kujongea sana, Jogoo nao walisikika wakianza kufokea kijiji
cha Korona nazo dalili za mawio zilianza kushamiri. Alikuwa ni Mijanja
aliyekuwa wa kwanza kushtuka kutoka katika usingizi na hapo hapo akili yake
iliwazia juu ya yule msichana. Akatoka ndani ya chumba chake na kuelekea katika
chumba alichomlaza yule msichana. Loooh! Mijanja alibaki kutoa macho kwa
mshangao mkubwa kwani aliambulia tu kumuona mdogo wake Zahera pale kitandani
akiwa amejifunika blangeti na yule msichana hakuwamo ndani ya chumba hicho. Alitoka
nje ya chumba kile huku akiita kwa nguvu “mgeni, mgeni wewe binti mgeni” na wala hapakuweza
kuwa na jibu lolote. Aliweka mikono yake miwili kichwani na kurejea katika
chumba chake huku mochozi ya uchungu yakimtoka.
***MWISHO***
ITAENDELEA, USIKOSE MIENDELEZO YA TAMTHILIYA HII KILA SIKU YA JUMAMOSI.
A
story by Sebastian Masabha:0758162527
2 Comments
Imekaa poaa sana Blood Jah Bless
ReplyDeleteShukrani sana blood, mbele tunasonga 💪
Delete